29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Afrika Kusini yavunja rekodi ya vipimo vingi zaidi vya corona

 GAUTENG, AFRIKA KUSINI

JIMBO la Gauteng lililopo Kaskazini Mashariki mwa Afrika Kusini limekuwa kitovu kikuu kipya cha ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona nchini humo huku maofisa wa afya wa nchi hiyo wakivunja rekodi ya kuchukua vipimo zaidi ya 50,000 vya corona kwa siku moja.

Taarifa zinasema kuwa maambukizi ya kirusi cha corona ni mabaya na makubwa mno katika jimbo hilo la Gauteng ikilinganishwa na maeneo mengine yote ya bara la Afrika.

Ingawa watu wa afya wanafanya juhudi mbalimbali, lakini kumekuwa na malalamiko ya kutochukuliwa hatua za kweli za kupambana vilivyo na ugonjwa hatari wa Covid-19 nchini humo. 

Mapema wiki hii, wafanyakazi wa afya wa Afrika Kusini walifanyia uchunguzi vipimo 56,000 vya Covid-19 kwa siku moja na kufikisha idadi ya watu wote waliochukuliwa vipimo vya corona nchini Afrika Kusini kufikia milioni mbili. 

Hadi kufikia juzi jioni, watu 250,687 walikuwa wamegunduliwa kukumbwa na ugoinjwa wa Covid-19 nchini Afrika Kusini. 

Kati ya hao wagonjwa 3,860 walikuwa wameshafariki dunia na 118,232 walikuwa wameshapata afueni na kuruhusiwa kurudi nyumbani nchini humo. 

Marekani ndiyo inayoongozwa duniani kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wagonjwa wa corona na vifo vilivyotokana na ugonjwa huo. Hadi jana jioni watu 3,306,407 walikuwa wamethibitishwa kukumbwa na Covid-19 nchini Marekani, huku watu 136,839 wakiwa wameshafariki dunia kwa ugonjwa huo nchini Marekani hadi kufikia jana jioni.

Mbali na hayo, uchunguzi wa hivi karibuni unaonesha kuwa, Waafrika miolioni 50 huenda wakatumbukia kwenye lindi la umaskini wa kupindukia kutokana na makali ya janga la corona. 

Hayo yalikuwemo kwenye ripoti mpya ya Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) ambayo imebainisha kuwa, maeneo ya magharibi na katikati mwa Afrika ndiyo yaliyoathiriwa zaidi na hali mbaya ya uchumi iliyosababishwa na janga la Covid-19.

Nchini Nigeria pia, Waziri wa Sayansi na Teknolojia Dk Ogbonnaya Onu alisema kifaa cha kupima virusi vya corona kimetengenezwa na wanasayansi wa Nigeria.

Akizungumza na wanahabari mjini Abuja, waziri huyo alisema kifaa hicho kinaweza kupima virusi vya corona haraka na kwa gharama za chini. Alisema katika miezi ijayo wakulima milioni 5 watafanyiwa kipimo, na vifaa milioni 10 vitatengenezwa katika awamu ya kwanza.

Mkurugenzi wa Wakala wa Kitaifa wa Teknolojia za Kibaiolojia wa Nigeria, Alex Akpa alisema kifaa hicho kinachojulikana kama RNA Swift kitaongeza sana uwezo wa Nigeria kufanya upimaji.

Alisema kifaa hicho kina vipimo vyenye ustadi wa hali ya juu na kinaweza kushindana na vifaa mshabaha vya kigeni.

Hadi kufikia sasa Nigeria imeripoti kesi 30,748 za maambukizi ya Covid-19 na miongoni mwao watu 689 wamefariki dunia. 

Hayo yanajiri wakati ambao kesi za Covid-19 zilizothibitishwa katika nchi za Afrika zilifika nusu milioni siku ya Alhamisi.

Hayo ni kwa mujibu wa takwimu mpya za Shirika la Afya Duniani (WHO) ambazo zinaonyesha pia kuwa, idadi ya vifo vilivyosababishwa na maradhi hayo barani Afrika imefikia 11,930.

John Nkengasong, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) ameonya kuwa, janga la corona barani humo linashika kasi na kuna haja ya nchi za bara hilo kufanya vipimo zaidi vya ugonjwa huo wa kuambukiza.

Katika hatua nyingine, Kamisheni ya Umoja wa Afrika imesema ina matumaini ya kudhibitiwa janga la Covid-19, na kwamba majaribio ya chanjo ya maradhi hayo kwa binadamu yanaendelea kufanyika hivi sasa katika nchi za Misri na Afrika Kusini.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,609FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles