BARAZA la Mitihani Taifa (NECTA) limetoa matokeo ya mitihani ya Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne (SFNA) ambako asilimia 88.87 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo wamefaulu huku shule binafsi zikiongoza dhidi ya zile za Serikali.
Akitangaza matokeo hayo Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde alisema wanafunzi 869,057 kati ya 977,886 (asilimia 88.87) ya waliofanya mtihani huo wamefaulu kwa madaraja ya A, B, C na D.
Alizitaja shule 10 bora zilizofanya vizuri kuwa ni Alliance Mwanza ikifuatiwa na Waja Spring Geita, St. Peter Kagera, Tumaini Mwanza, Furaha Mwanza, Acacia Land Tabora, Tusiime Dar es Salaam, Imani Kilimanjaro, Kaizirege Kagera na Ebenezer ya Kilimanjaro.
Mikoa 10 iliyofanya vizuri ni Dar es Salaam ukifuatiwa na Iringa, Kilimanyaro, Njombe, Arusha, Tanga, Geita, Kagera, Mwanza na Shinyanga.
Kuhusu wanafunzi 10 walioongoza kufaulu mtihani huo, Dk. Msonde aliwataja na shule zao kwenye mabano kuwa ni Frank Mgeta (Twibhoki), Slim Rashid (Hazina), Musa Christian (Alliance), Ezekiel Gilu (Waja Spring) na Martha Mkwimba (Tusiime).
Wengine ni Lameck Nsulwa (Rocken Hill), Rajab Mhoja Hamis (Rocken Hill), Charles Luhumbika (Kwema), Mathias Amos (Alliance) na Idd Masudi (Alliance).
Wanafunzi 108,829 ambao ni asilimia 11.13 ya waliofanya mtihani huo wameshindwa kwa kupata alama za daraja E na watalazimika kukariri darasa.
“Ikumbukwe kwamba aina ya mitihani hii iliyofanyika Novemba 25 na 26 mwaka jana ni mara ya kwanza.
“Takwimu za matokeo ya upimaji huu zinaonyesha asilimia 88.87 ya wanafunzi wamefaulu kwa kupata alama zenye madaraja ya ufaulu wa A, B, C na D huku asilimia 11.13 wamepata alama za daraja E lenye ufaulu usioridhisha,” alisema Dk. Msonde.
Mchanganuo wa ufaulu kwa madaraja unaonyesha kuwa asilimia 1.58 wamepata wastani wa daraja A, asilimia 18.49 daraja B, asilimia 41.92 daraja C , asilimia 26.82 daraja D na asilimia 11.13 wamepata daraja E.
Alisema matokeo ya jumla ya mitihani hiyo yanaonyesha wanafunzi wamefanya vizuri zaidi katika somo la Sayansi ambako wamefaulu kwa asilimia 89.44 huku walifanya vibaya zaidi somo la Kiingereza kwa ufaulu wa asilimia 65.67.
Dk. Msonde alizitaja wilaya zilizofanya vizuri kuwa ni Ilala Mjini , Moshi Mjini, Mji Njombe, Arusha Mjini, Mji Makambako, Tanaga Mjini, Arusha, Mufindi, Hai na Manispaa ya Bukoba.
Alisema lengo la upimaji huo kuwa ni kutoa tathmini endelevu ya mwanafunzi inayoweza kubaini umahiri wa juu wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) na kubaini maarifa, ujuzi na mwelekeo waliopata wanafunzi katika madarasa ya mwanzo (darasa la kwanza hadi la nne).