Na Abdallah Amiri, Igunga
JESHI la Polisi Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, linamshikiria mwalimu Keby Aron (32) wa Shule ya Sekondari Nanga kwa tuhumua ya kumuweka kimada mwanafunzi wa miaka 17 anayesoma kidato cha tatu B kwa zaidi ya miezi saba.
Baba wa mtoto aliyejitambulisha kwa jina moja la Joseph, alisema mwanae alikuwa anaishi na bibi yake Kata ya Nanga ambaye hakumtaja jina lake, alipokea taarifa hizo kutoka wasamalia wema.
Alisema bibi yake alianza kuona tabia ya mjukuu wake ikibadilika na kuanza kumfuatilia kwa karibu na ndipo alipobaini mjukuu wake anatembea na Aron.
Hata hivyo, aliamua kumuuliza mjukuu wake ambaye alimweleza amekuwa na uhusiano a mwalimu huyo kwa muda mrefu.
“Bibi yangu mimi sina jinsi, mwalimu amekuwa king’ang’anizi wa kunitongoza, nimekubali yaishe na ndiyo maana nimeamua kutembea nae na tuna muda mrefu na matumizi ananipa kama kimada wake,” alisema.
Baada ya kuona hali hiyo, bibi aliamua kumpigia simu baba yake ambaye anaishi mkoani Mbeya,alipofika Igunga alikwenda kumshtaki kwenye vyombo vya dora na hatimae kukamatwa na kuwekwa mahabusu.
Baadhi ya wazazi wanaosomesha watoto wao katika shule hiyo, Haruna Juma alilipongeza jeshi la polisi kumkamata mwalimu kwani kitendo hicho ni cha aibu kinarudisha nyuma juhudi za serikali.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Revocatus Kuuli alithibitisha Aron kukamatwa na polisi kwa tuhuma ya kufanya mapenzi na mwanafuzi.
“Ndugu zangu waandishi wa habari,ofisa elimu sekondari yuko Tabora, kuhusu tuhuma ya mwalimu nimepata taarifa amekamatwa yuko polisi,siwezi kulizungumzia zaidi suala hili tuviachie vyombo vya sheria.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora,Barnabasi Mwakalukwa alipoulizwa juu ya kukamatwa Aron alisema bado hajapata taarifa hiyo, “mimi sijapata taarifa hiyo naona polisi Igunga bado wanafanya uchunguzi wakinitumia nitatoa taarifa kwa umma” alisema.
Mtuhumiwa anategemewa kufikishwa mahakamani jana kutokana na taarifa za ndani ambazo gazeti hili lilizonazo.