30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Hussein Mwinyi kumstaafisha siasa Maalim Seif?

NA MARKUS MPANGALA

OKTOBA 28 mwaka huu wananchi watapiga kura ya urais, ubunge na udiwani kutoka vyama mbalimbali vya siasa kama vile CCM, CUF, ACT Wazalendo,CHADEMA, NCCR Mageuzi na kadhalika. Joto la uchaguzi wa mwaka huu limeonekana kupamba moto zaidi kuliko miaka ya nyuma. 

Kwanza, utaratibu wa CCM katika kura za maoni za watia nia za ubunge zimesisimua na kuvutia wengi. Namna watia nia walivyoshikishwa kura zao, namna walivyoshiriki kwa uwazi ni mambo ambayo yamechochea mvuto.

Pili, ndani ya CCM wamejitokeza watu wengi kutia nia. Bila shaka hili linajitokeza pia kwa  vyama vingine ambavyo baadhi ya vijana na watu wazima wamejitokeza kwa wingi kushiriki siasa. 

Kama ilivyo ada kwa Maalim Seif unapowadia uchaguzi mkuu, naye anakuwa miongoni mwa wanaotia nia ya kugombea urais. Maalim ni mwanasiasa ambaye amekuwa akigombea urais bila mafanikio dhidi ya wagombea mbalimbali wa CCM.

Kabla ya kuangalia rekodi zake, ni dhahiri safari hii Maalim ana matumaini kugomnbea urais wa Zanzibar kupitia chama kipya cha ACT Wazalendo. Hadi sasa yeye ni mgombea pekee kutoka ACT wazalendo ambaye ana uhakika wa kupeperusha bendera ya chama hicho visiwani Zanzibar. 

Katika chaguzi mbalimbali za mwaka 1995, 2000, 2005,2010, na 2015 zinaonyesha kuwa kiongozi huyo ni hazina ndani ya chama hicho, hususani anavyojizolea kura kila uchaguzi. 

Maalim alikuwa kiongozi CUF kwa muda mrefu. Cham cha CUF hakijawahi kuwa na Katibu mkuu mwingine tangu kilipoanzishwa mwaka 1992. Jambo hilo kisiasa linaleta changamoto kwake ni kiongozi ambaye hayupo tayari kuachia ngazi ili wengine wachukue nafasi.

Matokeo ya kutokuwapo katibu mwingine kulitengeneza dhana kuwa visiwani na Bara kuwa Cuf ni Maalim na Maalim ni Cuf.

MAALIM VS SALMIN AMOUR

Jina la Maalim Seif Sharrif Hamad lina rekodi katika uchaguzi mkuu. Amegombea urais wa Zanzibar kwa mara ya kwana mwaka 1995. 

Ni mwanasiasa aliyegombea urais wa Zanzibar mara nyingi zaidi kuliko mwingine yeyote nchini. Hadi sasa amegombea urais wa Zanzibar mara 5, na iwapo mwaka 2020 atapitishwa itakuwa ni mara ya 6. 

Safari ya Maalim Seif kugombea urais ilianza mwaka 1995 alipopambana na mgombea wa CCM, Salmin Amour. Kwa mujibu wa Tume ya uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) matokeo ya urais mwaka 1995, Salmin Amour alishinda kwa asilimia 50.24 dhidi ya 49.76 alizopata Maalim Seif. Hata hivyo Cuf ilitangaza kutoutambua ushindi huo, lakini kama walivyo wanasiasa wa upinzani kwa kutoa msimamo huo, ukweli ni kwamba alitakiwa kukubali kushindwa.

MAALIM SEIF VS AMANI KARUME 

Uchaguzi mkuu wa urais,ubunge na udiwani mwaka 2000 Maalim Seif aliingia ulingoni kupambana na Amani Karume mtoto wa rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume. Kwa mara nyingine matokeo ya ZEC yalionyesha Seif aliangushwa baada ya kujikusanyia asilimia 32.96 ya kura dhidi ya asilimia 67.04 alizopata Amani Karume. Uchaguzi wa mwaka 2000 alipata asilimia chache (32.96%).

Hata hivyo kama walivyo wanasiasa wa upande wa upinzani naye hakukubali kushindwa, kwani aliamini uchaguzi huo uliuwa na matokeo mazuri upande wake. Lakini ukweli ni kwamba matokeo ya ZEC ndiyo rasmi na yanatambulika kuwa Maalim Seif aishindwa uchaguzi. Rekodi ikawekwa kuwa Maalim Seif alishindwa uchaguzi kwa mara pili dhidi ya mgombea mwingine tofauti wa CCM.

MAALIM SEIF VS KARUME 

Uchaguzi wa mwaka 2005 aliteuliwa tena Maalim Seif kupambana na Amani Karume  wa CCM. Uchaguzi huo ulipokamilika, matokeo ya ZEC yalimtangaza Amani Abeid Karume kuwa mshindi baada kujikusanyia asilimia 53.18, huku Seif Hamad akijipatia asilimia 46.07 ya kura zote. Kama ilivyo ada na ilivyotarajiwa chama cha Cuf walipinga matokeo hayo. 

MAALIM SEIF VS MOHAMMED SHEIN

Mwanasiasa Maalim Seif alirudi tena kinyang’anyironi mwaka 2010 akiwakilisha CUF dhidi ya Dk. Ali Mohammed Shein wa CCM. Dk. Shein alikuwa mgombea wa tatu kupambana na Maalim Seif. Vile vile ulikuwa uchaguzi wa nne kwa Maalim Seif dhidi ya CCM na wagombea wake.

Matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 31, mwaka 2010 ZEC ilimtangaza Dk. Mohammed Shein kuwa mshindi wa kiti cha urais wa Zanzibar kwa kupata asilimia 50.1 dhidi ya 49.1 za Seif ya kura zote zilizopigwa visiwani humo. 

Kutokana na makubaliano ya vyama hivyo kumaliza mgogoro wa muda mrefu visiwani humo, Maalim Seif alitakiwa kuwa sehemu ya serikali ambapo aliteuliwa kuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, huku Balozi Seif Ali Iddi akiwa makamu wa pili wa Rais. 

MAALIM SEIF VS CCM 2015 

Matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2015 yalifutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) chini ya Mwenyekiti wake Jecha Salum Jecha. Tume ya ZEC ilitangaza pia uchaguzi wa marudio kufanyika mnamo Machi 20, mwaka uliofuata yaani 2016. 

Licha ya kufutwa matokeo ya uchaguzi huo, Maalim Seif aliitisha mkutano wa waandishi wa habari mnamo Oktoba, 2015 na kusema yeye ndiye mshindi wa kiti cha urais Zanzibar na alikataa kushiriki uchaguzi wowote wa marudio. Baada ya kugomea kushiriki uchaguzi wa marudio, Dk. Shein aliibuka mshindi kwenye uchaguzi huo na kumpa kumbo jingine la kisiasa Maalim Seif. 

MAALIM SEIF VS MWINYI

Uwezekano wa Maalim Seif kupitishwa na chama chake cha ACT Wazalendo kuchuana na mgombea wa CCM, Dkt. Hussein Mwinyi ni mkubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa 6 kwa Maalim Seif. Pia utakuwa uchaguzi wa kupambana na mgombea mwingine wa CCM ambaye kimahesabu ni mgombea wa nne. Tayari Maalim Seif ameshapambana dhidi ya Salmin Amour, Amani Karume, Dkt. Shein, na sasa anaelekea kuchuana na Dkt Mwinyi.

Lakini je, safari hii atafua dafu mbele ya Dk. Hussein Mwinyi? Hilo ndilo swali la msingi kwa sasa. La pili je, uchaguzi wa mwaka huu, iwapo Dk. Hussein Mwinyi ataibuka mshindi, je atamstaafisha siasa Maalim Seif? Majibu ya maswali haya tutapata baada ya uchaguzi mkuu mwaka huu 2020.

Baruapepe; [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles