23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Matarajio kampeni Uchaguzi Mkuu Oktoba 28

Na MWANDISHI WETU

KIU ya Watanzania kushiriki kampeni za uchaguzi mkuu wa urais, ubunge, udiwani inatarajiwa kukatwa ifikapo Agosti 26 mwaka huu, ambapo uzinduzi utafanyika kwa vyama mbalimbali na kudumu kwa takribani siku 60.

Dalili zinaonesha kuwa kutakuwa na ushindani mkali katika nafasi ya urais ambapo jumla vyama vya siasa 16 vimeweka wagombea wao hadi kufikia sasa.

Duru za kisiasa zinaonesha kuwa ushindani mkali utakuwa katika kampeni za wagombea watatu ikiwa watateuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Agosti 25; ambao ni Dk. John Magufuli (CCM), Tundu Lissu (Chadema) na Bernard Membe (ACT Wazalendo) kwa upande wa Jamhuri, huku Maalim Seif (ACT Wazalendo) na Dk. Hussein Mwinyi (CCM) wakitoana jasho upande wa Zanzibar.

Vyama pinzani vina agenda zao ambazo ni dhahiri zinaonekana zitawasilishwa kwenye kampeni za uchaguzi kubwa ikiwa ni ghadhabu za kunyimwa fursa ya mikutano ya hadhara. Wakati mgombea wa CCM Dk. Magufuli akionekana kujivunia maendeleo makubwa aliyoyafanya katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.

Kampeni hizo zitafika tamati tarehe ya uchaguzi mkuu Oktoba 28 ambapo mamilioni ya Watanzania watapiga kura kuchagua viongozi wapya watakaopokea kijiti cha uongozi cha miaka mitano ijayo. Huu ni uchaguzi wa sita tangu Tanzania irejee kwenye mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 1992.

“Hakika huu ni uchaguzi wa vijana. Vyama vyote na wagombea wao wakiweza kuwashawishi vijana wana nafasi kubwa zaidi ya kushinda. Kundi la wapigakura wapya zaidi ya milioni saba ni kubwa mno. Mbinu zitategemea matamanio ya kundi hili. Hapa maana yake iwapo wamejiandikisha kupiga kura wengi wao walizaliwa miaka ya 1990. Kundi jingine waliozaliwa mwanzoni mwa miaka 2000. Hayo ni mabadiliko, ni sura mpya ya wapigakura, kampeni zinagusa hao kwenye uchaguzi wa mwaka huu,” anasema Francis Daudi, mhadhiri wa historia wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino tawi la Tabora na mchambuzi wa siasa na utawala bora.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mkutano wa 19 wa Bunge jijini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema idadi ya wananchi waliojiandikisha kupiga kura imeongezeka ambapo wapigakura halali ni 29,804,992 ikilinganishwa na 23,161,440 kwa mwaka 2015.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Semistodes Kaijage wakati wa ufunguzi wa ratiba ya uchaguzi, alisema takwimu za awamu ya kwanza na pili zinaonesha kuwa wapigakura wapya walioandikishwa ni 7,326,552, walioboresha taarifa zao ni 3,548,846 na 30,487 wamepoteza sifa.

Kumbukumbu za mwaka 2015 zinaonesha wapigakura wanawake ni asilimia 53, wanaume walikuwa asilimia 47. Wapigakura vijana waliokuwa na umri kati ya miaka 18 na 35 walikuwa asilimia 57 ya wapigakura wote. Wapigakura waliokuwa na umri zaidi ya miaka 50 walikuwa asilimia 18 huku wengine asilimia 25 wakiwa na umri kati ya 36 na 50. Hata hivyo, waliopiga kura mwaka 2015 ni watu 15,589,639 sawa na asilimia 67.31.

Kutumia mitandao ya kijamii

Eneo hili linahusisha mabadiliko ya upashanaji habari kati ya vyama vya siasa na wagombea wao kwa upande mmoja na wanachama na wapigakura kwa upande mwingine. Kufungwa kwa baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vilikuwa vikitoa fursa kwa upinzani kuwasiliana na wafuasi wao, kumewafanya wapinzani kuhamia mitandao ya kijamii kama nyenzo yao ya kufanya kampeni katika uchaguzi ujao.

“Bila shaka tutakuwa na kampeni za mitandaoni. Wagombea wa upinzani wanaamini vyombo vya habari havitatoa habari zao kwa ukamilifu iwe redio au Televisheni. Naona zitakuwa kampeni za swali na jibu. Wanasiasa watajikita katika kurusha vijembe na kujibu. Upinzani badala ya kueleza sera zao wataeleza walivyoteseka miaka mitano, na CCM badala ya kusema watafanya nini wataeleza walivyofanya,” anaongeza Francis Daudi.

Katika hatua za awali vyama vya ACT, Chadema na sasa NCCR Mageuzi ni vinara wa kutoa hotuba zao kupitia mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter, YouTube na Instagram. Viongozi Zitto Kabwe, Tundu Lissu, Maalim Seif na Katibu wa Uenezi CCM, Humphrey Polepole wamekuwa wakitoa hotuba kupitia mitandao ya kijamii.

Nyenzo hiyo inatarajiwa kutikisa zaidi katika uchaguzi huu.

Katika hatua nyingine, baadhi ya vyama vilianzisha utaratibu wa kusajili wanachama wao kwa njia ya mtandao. Mwanachama amepewa fursa ya kujisajili mwenyewe na kupunguza usumbufu kwa kwenda kwenye tawi la chama au kupishana muda wa kazi na mwandikishaji wa wanachama, mathalani wa Chadema na CCM.

Aidha, usajili huo kwa njia ya Simujanja (Smartphone) unasaidia kumwezesha mwanachama kupata taarifa za chama kupitia simu yake ya mkononi.

Kwahiyo, kampeni za mwaka huu zinaweza kufanyika kwa kuwasiliana na wanachama wa chama moja kwa moja kupitia simu zao. Badala ya kutegemea magari ya matangazo kupita mitaani kuwatangazia wanachama kuhusu mkutano wa chama husika. Hii ni njia ya kufanya kampeni kumweka mwanachama karibu na mapambano kwa njia ya faida ya teknolojia, pamoja na kupunguza utegemezi kwenye vyombo vingine vya upashaji habari.

Upinzani kugawana kura

Vyama vya upinzani vinaweza kuingia katika kampeni kila kimoja kikifanya mambo yake. Mwaka 2015 palikuwa na muungano wa vyama vya upinzani kupitia mwamvuli wa UKAWA (Umoja wa Katiba ya Wananchi) ambapo ulikuwa na mshikamano zaidi kuliko wa mwaka 2020. Muungano huo ulihusisha vyama vikubwa na vidogo ambapo ushirikiano wao uliwaletea zaidi ya wabunge 100.

Uchaguzi wa mwaka 2020 mambo yanaelekea kuwa tofauti na 2015 ambapo kulikuwa na mgombea mmoja mwenye nguvu kwa upande wa upinzani Edward Lowassa, ambaye alikuwa akiungwa mkono na Ukawa dhidi ya John Magufuli wa CCM. Mwaka huu, licha ya kuwa na zaidi ya vyama 15 vinavyotaka kumng’oa madarakani Magufuli, upinzani mkali utakuwa unatoka kwa Tundu Lissu (Chadema) na Bernard Membe (ACT Wazalendo).Kushindwa kwa vyama hivyo kukubaliana kutoa mgombea mmoja kutamaanisha kuwa kura za wafuasi wa upinzani zitagawanyika.

Kwa upande wa Zanzibar, mgombea wa upinzani ambaye atampatia wakati mgumu Dk. Hussein Mwinyi wa CCM bado ni Maalim Seif (ACT Wazalendo), ambaye anarejea ulingoni kwa mara ya sita, ikiwa ni mara ya kwanza nje ya chama cha CUF ambacho alibidi akihame kutokana na migogoro ya ndani.

Ukimya utafiti kura za maoni

Mwaka 2020 Tanzania kampeni za uchaguzi zinawadia pasipo utafiti wowote tofauti na ule wa mwaka 2015. Mathalani utafiti unaofanywa na taasisi kama Twaweza au IPSOS, kuelekea uchaguzi huu hakuna taasisi iliyojishughulisha na utafiti wa kisiasa kupima kukubalika kwa wagombea.

Mwaka 2015 UVCCM walifanya utafiti ulionesha mgombea wa CCM John Magufuli angeshinda kwa asilimia 85. Nao utafiti wa timu ya kampeni ya CCM uliosomwa na Januari Makamba ulionesha kuwa Magufuli ageshinda kwa asilimia 69.

Utafiti wa asasi ya Twaweza nao ulisema mwaka huo Magufuli angeshinda kwa asilimia 65. Taasisi ya IPSOS ilisema Ukawa wangepata asilimia 31 katika uchaguzi huo. Mwaka 2018 Twaweza walitoa utafiti wa kushuka umaarufu wa Rais Magufuli ambapo alifikia asilimia 56.

Hata hivyo, kampeni za mwaka huu zinaelekea kuanza pasipo kuona utafiti wa kura za maoni kukubalika vyama vya siasa, wagombea na wapigakura wao. Duru za kisiasa zinasema taasisi nyingi za utafiti ni kama vile zimegoma kufanya kazi hiyo licha ya kulindwa na Katiba ya Tanzania Ibara ya 18 (1 na 2) inatoa haki ya kikundi cha watu au taasisi yoyote kukusanya na kutoa habari bila kuvunja sheria. Aidha, sheria inayoagiza taasisi au mtu binafsi akitaka kufanya utafiti aombe kibali kwa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) imekuwa kikwazo.

CCM na kampeni inayojitegemea

Uchaguzi wa mwaka 2015 CCM ilinufaika na mgogoro uliokuwapo Chadema na Ukawa. Dk. Wilbroad Slaa alijiuzulu nafasi ya Ukatibu Mkuu Chadema. Naye mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, alijizulu wadhifa huo. Matukio yote mawili yalisababisha mgogoro ndani ya muungano wa Ukawa.

CCM mwaka huu wataingia katika kampeni bila kutegemea mgogoro wa upinzani. Ukweli mmoja ni kwamba CCM wanajivunia serikali waliyounda ambayo imejikita katika kuanzisha na kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo. Kwamba, miradi hiyo inajinadi na kuwapa imani kuwa watapata kura nyingi katika uchaguzi huu.

Kuna majimbo ambayo upinzani ilichaguliwa mwaka 2015 na mwaka huu mchuano mkali unatarajiwa kutokea kwenye majimbo hayo. Matahalani majimbo sita kati ya 10 ya jijini Dar es Salaam, yalichukuliwa na wabunge kutoka upinzani. Nje ya Dar es Salaam majimbo kadhaa kama Iringa Mjini, Tanga Mjini, Arusha Mjini, Mbeya Mjini, Kigoma-Ujiji na Tarime (Mjini na Vijini) yanatarajiwa kushuhudia upinzani mkali zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles