22.6 C
Dar es Salaam
Saturday, May 21, 2022

Uamuzi Rais Uhuru wahusishwa mabadiliko baraza la mawaziri

NA ISIJI DOMINIC 

USHIRIKIANO wa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na kiongozi wa Chama cha ODM, Raila Odinga na makubaliano ya ushirikiano wa chama cha Jubilee na vyama vya upinzani hususan Wiper, Kanu na Chama cha Mashinani (CCM) kuliibua mjadala wa dalili za mabadiliko makubwa baraza la mawaziri. 

Hata hivyo, mabadiliko ambayo Rais Uhuru ameyafanya kwenye baraza lake ni madogo huku Wakenya wakisubiri mabadiliko makubwa zaidi hususan kipindi hiki ambacho zimebaki takribani miaka miwili kabla ya Kenya kufanya uchaguzi mkuu. 

Mara ya mwisho Rais Uhuru kufanya mabadiliko madogo katika baraza lake la mawaziri ilikua Januari mwaka huu akimundoa Mwangi Kiunjuri kama Waziri wa Kilimo na nafasi yake kuchukuliwa na Peter Munya wakati Henry Rotich anayekabiliwa na kesi mahakamani inayohusu ufisadi aliondolewa na mikoba ya Wizara ya Fedha kukabidhiwa Ukur Yattani.

Wiki iliyopita, Rais Uhuru aliagiza mawaziri wake wote kuchukua mapumziko ya siku 11 iliyoanza Jumatatu Agosti 17, uamuzi uliozua tetesi ya mabadiliko katika baraza la mawaziri. Ni agizo ambalo pia alilitoa kwa Makatibu Wakuu, Makatibu Wakuu Wasaidizi na Mkuu wa Sheria. Hii inamaanisha kikao kijacho cha baraza la mawaziri kitafanyika Septemba 3 mwaka huu. 

Ikumbukwe hii haitakua mara ya kwanza Rais Uhuru kuchukua uamuzi huo kwani mwaka 2018, aliamuru mawaziri, Mkuu wa Sheria na makatibu wakuu kwenda mapumziko ya Krismasi ambapo Mkuu wa Utumishi wa Umma, Joseph Kinyua, alisema mapumziko hayo yatawapa muda kusherehekea na familia na marafiki zao sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Swali linabaki, je, agizo la Rais Uhuru ni kutoa mapumziko ya siku hizi 11 hususan kwa mawaziri au ni kweli Wakenya watarajie mabadiliko tena makubwa katika baraza lake la mawaziri?

Taarifa kutoka Ikulu bado inasisitiza uamuzi huo ulichukuliwa na Rais Uhuru ili kuruhusu mawaziri kuwa na muda wa kupumzika baada ya kujihusisha na pilkapilka za shughuli za kila siku wizarani mwao tangu mwaka uanze. 

Licha ya likizo hiyo ya siku 11, kikao kidogo cha baraza la mawaziri kinachofanyika kila Jumanne ambacho kinatambulika kama Kamati ya Utekelezaji wa Maendeleo ya Taifa na Habari chini ya mwenyekiti ambaye pia ni Waziri wa Usalama, Fred Matiangi, yatakua ya lazima kuhudhuria. Tafsiri yake ni kwamba mawaziri hawataweza kuwa nje ya jiji la Nairobi kwa muda mrefu. 

“Mawaziri hawajapumzika tangu mwaka uanze. Nao pia wanahitaji muda kuwa na familia zao. Ni mapumziko ya kawaida na hata majaji pia wanaenda mapumziko,” alinukuliwa moja wa kiongozi mkubwa Serikalini.

“Wakati wa mapumiko ya kufanya kazi, mawaziri wataruhusiwa kuchukua likizo pindi tu itakapoidhinishwa na Rais na pia kwa waziri yoyote atakayehitaji kusafiri nje ya nchi, atahitaji kibali kutoka kwa Rais.” 

Uvumi umezidi kutanda huenda Rais Uhuru akafanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri kama alivyofanya kwa mabunge yote mawili; Bunge la Taifa na Bunge la Seneti. 

Tetesi zinadai watu wa karibu wa kiongozi wa ODM, Raila, wapo mbioni kunufaika na mapatano baina ya viongozi hawa wawili huku pia wanasiasa kutoka Wiper, Kanu na CCM wakisubiri uteuzi hususan baada ya vyama vyao kuingia makubaliano ya ushirikiano na Jubilee. 

“Kuna dalili za mabadiliko katika baraza la mawaziri kufanyika kipindi ambacho mawaziri wapo mapumiko,” moja wa mtoa habari alinukuliwa huku Beatrice Elachi aliyejiuzulu nafasi ya uspika katika kaunti ya Nairobi akitajwa miongoni mwa watakaonufaika na uteuzi wa baraza jipya la mawaziri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
191,647FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles