Na MASHIRIKA YA HABARI YA KIMATAIFA
REKODI mpya ya idadi ya virusi vya corona imeweka wingu mwanzoni mwa sherehe za uhuru nchini Marekani wakati ongezeko la maambukizi lailazimisha Uingereza kuwaweka wasafiri kutoka Marekani kwenye orodha mbaya.
Wakati fukwe zimefungwa kutoka eneo moja la pwani hadi jingine na maofisa wakiwataka Wamarekani kubakia majumbani mwao, hali isiyokuwa ya furaha kuelekea katika kile ambacho kwa kawaida ni mwishoni mwa juma kunakochomwa nyama na hali ya hewa ya jua imelemea mapambano ya kudhibiti ugonjwa wa COVID-19 katika kitovu cha janga hilo duniani.
“Ni idadi usiyoweza kuamini,” amesema Faisal Masud , mkurugenzi wa matibabu katika hospitali ya Methodist mjini Texas, ambayo maofisa wamesema inakaribia kabisa kuzidiwa na wagonjwa.
Ukigusa karibu kila nchi duniani tangu kujitokeza kwa ugonjwa huo nchini China mwishoni mwa mwaka jana, virusi vya corona vimewaambukiza kiasi ya watu milioni 10.9 na kuwauwa watu 522,000 duniani, na kuzima uchumi uliokuwa hapo kabla ukikua kwa kasi na kusababisha maisha ya watu kuzimika.
Lakini wakati Ulaya na sehemu nyingi za Asia kwa kiasi kikubwa zimeweza kudhibiti virusi hivyo vya corona , kwa upande wake Uingereza inajitayarisha kufungua biashara zake, migahawa na kumbi za sinema, lakini nchini Marekani ugonjwa huo umewauwa karibu watu 130,000 huku kukiwa na ongezeko kubwa la kesi mpya za maambukizi ambapo mtaalamu wa ngazi ya juu wa magonjwa ya kuambukiza
Anthony Fauci amesema; “unaiweka nchi nzima katika hatari.”
REKODI YA MAAMBUKIZI
Nchi hiyo yenye uchumi mkubwa duniani imevunja rekodi yake ya maambukizi mapya kwa siku ya tatu mfululizo hadi Ijumaa wiki hiii, kwa kuwa na zaidi ya maambukizi 57,000 katika muda wa masaa 24.
Inatarajiwa kufikisha maambukizi milioni tatu wiki ijayo, ambapo kesi zinaongezeka hususan upande wa kusini na magharibi.
Rais wa Marekani Donald Trump , akiwa katika eneo la Mount Rushmore kwa ajili ya sherehe za kurusha fashifashi pamoja na maelfu ya wahudhuriaji wakikaribiana na barakoa si lazima, hadi sasa amepuuzia ongezeko hilo la maambukizi mapya.
Lakini mtangulizi wake Barack Obama amewataka Wamarekani kujiweka “salama na kuwa wajanja.”
Sura za Marais wa zamani wa Marekani zilizochongwa katika Mlima Black South Dakota
“Itatulazimu kuchukua hatua kwa pamoja kudhibiti virusi hivi. kwa hiyo vaa barakoa. Safisha mikono yako. Na wasikilize wataalamu , sio watu ambao wanajaribu kutugawa,” aliandika katika ukurasa wa Twitter.
Shirika la afya ulimwenguni WHO limezitaka nchi ambazo zimeathirika kwa kiasi kikubwa, “kuamka” na kuona hali halisi.
“Watu wanapaswa kuamka. Data hazidanganyi,” Mkurugenzi wa masuala ya dharura wa WHO Michael Ryan aliwaambia waandishi habari mjini Geneva.