Maana ya Tanzania kuingia uchumi wa kati

0
1048

Na MWANDISHI WETU-DAR ES  SALAAM 

BENKI ya Dunia (WB) Julai 1 mwaka huu ilitangaza Tanzania kuwa miongoni mwa nchi saba zilizoingia kwenye orodha ya nchi za uchumi wa kipato cha kati.

Wakati Tanzania ikionja mafanikio hayo, nchi nyingine tatu ziliporomoka kutoka kwenye orodha hiyo kutokana na hali zao za uchumi kwa mwaka 2019.

Benki ya dunia imegawa uchumi wa dunia katika makundi manne, uchumi chini, chini kati,juu-kati na wa juu katika kila nchi.

Uainishaji huo  huwa unatangazwa kila mwaka Julai 1,  na unatokana na pato la Taifa (Gross National Income –GNI), hii ina maana ni pamoja na  jumla ya fedha inayopatikana kwa watu wa taifa husika na mgawanyo wa biashara kwa kulingana na idadi ya watu wake.

Kutokana na hayo inaelezwa Tanzania imepata hadhi ya kuingia kwenye kipato cha kati baada ya GNI  kupanda kutoka Dola 1,020 mwaka 2018 hadi kufikia Dola 1,080 mwaka 2019.

Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani ilikuwa na mikakati yake ambayo ilianza kutekelezwa huko nyuma kuhakikisha inaingia kwenye nafasi hii ya sasa.

Ili kufika hapa Tanzania ilianzisha kitu ilichokiita ‘Tanzania  vision 2025’  au Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025  hii ilikuwa ni wakati wa Serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Mstaafu, Benjamin William Mkapa.

Ikiwa na maana kwamba ifikapo mwaka 2025 nchi iwe imeingia kwenye uchumi wa kipato cha kati, jambo ambalo limefanyika sasa ikiwa ni miaka mitano nyuma.

Serikali ya Awamu ya nne, chini ya Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete  ilitafuta njia  yake ya  kutekeleza ‘Tanzania Vision 2025’ambapo ilituma watalaamu wake kwenda kujifunza kupitia mafanikio ya nchi ya Malaysia.

Miongoni mwa watalaamu hao alikuwa ni Waziri wa sasa wa Fedha, Dk. Philip Mpango ambapo baadae serikali ya Kikwete ilikuja na kitu kinaitwa Big Result Now (BRN) ‘Matokeo Makubwa sasa’ ambayo iliundiwa ofisi kwa ajili ya kuangalia miradi ya kimkakati ya kuitekeleza ili kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kipato cha kati.

Alipoingia Rais Dk. John Magufuli mara moja aliivunja ofisi ya BRN na baadhi ya watumishi wake kuhamishiwa mahala pengine akiwamo Msemaji Mkuu wa sasa wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi.

Yeye alikuja na staili au kile alichokiona namna bora ya kutekeleza ‘Tanzania Vision 2025’ na mafanikio yake ni hasa katika upande wa utekelezaji wa miradi mikubwa kama  ya ujenzi wa reli ya kisasa, SGR, Ujenzi wa bwawa la kufua umeme katika Mto Rufiji,  ujenzi wa barabara za juu, kuongeza huduma za afya, maji safi  na mingine.

Muda mfupi baada ya WB kutangaza hatua hiyo, Rais Dk. John Magufuli kupitia ukurasa wake wa mtandao wa twitter, aliwapongeza Watanzania kwa mafanikio hayo na kusema hatua hiyo ni ushindi na kazi kubwa iliyofanywa na taifa.

“Benki ya Dunia leo (juzi) tarehe 01 Julai, 2020 imeitangaza Tanzania kuingia uchumi wa kati. Nawapongeza Watanzania wenzangu kwa mafanikio haya. Huu ni ushindi mkubwa na kazi kubwa tumeifanya, tulipanga kuingia uchumi wa kati ifikapo 2025, lakini tumefanikiwa 2020. Mungu ibariki Tanzania,” aliandika.

WACHUMI WANACHOSEMA

Wachumi wameelezea hatua hiyo ya Tanzania kuingia katika uchumi wa kati wakisema ina faida na hasara.

Mtaalamu wa uchumi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe tawi la Dar es Salaam, Profesa Honest Ngowi, akizungumza na gazeti dada la hili la MTANZANIA wiki hii alisema ni fahari ya nchi kwani siku zote kuwa nchi maskini si sifa nzuri, hivyo ni jambo la kujivunia.

“Nchi hata siku moja haiwezi kuwa na lengo la kuelekea mahali ambapo si pazuri, tunavyoingia kundi hili kuna maana nzuri. Mfano kwenye uwekezaji, wawekezaji wanavyokuja hutizama je, hiyo nchi iko kwenye kundi gani, maana yake wanajua vipato viko juu kiasi fulani, huduma za jamii ziko katika hali bora zaidi, hivyo inaweza kuwa ni msaada kuvutia wawekezaji.

“Lakini lazima ujue pia kuna hasara zake kwa kiasi fulani, ambacho mara nyingi huwa hakizungumzwi. Unapoingia kwenye kundi hili ni mtoto umekua, utaacha sasa kubebwa na mama, itabidi utembee mwenyewe.

“Kuna baadhi ya misaada ‘hatuta–qualify’ kuipata, kuna baadhi ya mikopo hatutaipata tena kwa masharti nafuu, tutaipata kwa masharti ya kibiashara ya mtoto aliyekomaa,” anasema Profesa Ngowi. 

Anafafanua kuwa pato la nchi huhesabiwa kwa kutazama ongezeko la bidhaa na huduma na kwamba hapa nchini kuna sekta ambazo zinakua kwa tarakimu mbili kama vile madini na usafirishaji ambazo zimechangia kuongeza pato la taifa.

“Benki ya Dunia hugawanya nchi katika makundi mbalimbali. Kuna nchi za uchumi wa chini, kati na juu. Lazima tujiulize tulikuwa wapi, maana yake tulikuwa kwenye uchumi wa chini, lengo letu la kisera ukiangalia ‘Vision 2025’ ilikuwa kwamba ifikapo 2025 tuwe kwenye uchumi wa kati, sasa ni kama vile tumefika miaka mitano kabla.

“Lakini lazima tuelewe hili kundi la uchumi wa kati lina makundi mawili tena; kuna uchumi wa kati wa chini na uchumi wa kati wa juu. Kwahiyo tulichopewa na Benki ya Dunia ni kuingia kwenye uchumi wa kati ngazi ya chini, kwa maana kwamba wastani wa pato la kila Mtanzania kwa mwaka ni kwenye Dola 1,036 hadi Dola 4,045.

“Ukizidisha mara Sh 2,316; 2,310 kwa maana ya bei ya Dola moja kwa shilingi ya leo maana yake tunazungumzia milioni zaidi ya mbili na zaidi ya milioni nne kwa mwaka, ndiyo tafsiri yake.

“Huu ni wastani na kitakwimu maana yake hapa tumechanganya wastani wa kipato cha Mo, Mzee Bakhressa, matajiri wote unaowafahamu hapa Tanzania na yule mwenye kipato cha chini zaidi, ukajumlisha wote na kugawanywa kwa Watanzania milioni 50 ndiyo unapata huo wastani.

“Kwahiyo kuna mtu wala hii hataisikia mahali popote wala haitakuwa na maana, kwa maana kwamba mlo mmoja aliokuwa akiula jana, ataula kesho na kesho kutwa, lakini kama nchi tumeingia kwenye hilo kundi,” anasema Profesa Ngowi. 

Anashauri kuwe na mikakati ya kudhibiti kasi ya ongezeko la idadi ya watu kwa sababu pato la taifa litagawanywa kwa idadi ya watu na kama itaendelea kukua kwa kasi nchi inaweza kurudi kwenye kundi la chini.

“Muhimu kama tunataka kubaki hapa na kwenda juu zaidi kuongeza pato la taifa na tunatakiwa kuhakikisha kasi ya ukuaji wa idadi ya watu haiendi juu sana,” anasema Profesa Ngowi. 

Kwa upande wake, Mtafiti na Mchumi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), Profesa Samuel Wangwe, anasema jambo la muhimu ni kuhakikisha uchumi unaendelea kukua na kuwafaidisha watu wote. 

“Kwanza uchumi tulitegemea uwe unakua kwa asilimia nane kila mwaka, lakini haukufikia hapo, kwahiyo tungekuwa tumefika asilimia nane tungefika hata miaka mitatu nyuma. Kwahiyo si kwamba tumevuka ‘target’ ya asilimia nane, bado tuko chini, tunacheza kwenye sita na nusu, saba.

“Kitu muhimu sasa ni kuhakikisha uchumi unaendelea kukua, lakini kama ‘vision’ ilivyosema uchumi ukue kwa namna ambayo wote wanafaidi hata wadogo, yaani uchumi jumuishi. 

“Uchumi jumuishi unaanzia hasa hasa kwenye kilimo ndiyo kuna watu wengi, ili tija, kipato kiongezeke kwenye kilimo, kitachangia uchumi wa viwanda kukua ili tupate uchumi mkubwa.

“La pili ni huu uchumi wa watu wadogo wadogo wa ‘informal sector’, uchumi uwanufaishe kwa nguvu zaidi,” anasema Profesa Wangwe.

Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Hassan Abbasi, amesema waliweka malengo kupitia Dira ya Maendeleo ya Taifa kuwa ifikapo mwaka 2025 umasikini uwe umepungua.

Anasema licha ya kuweka malengo hayo, Benki ya Dunia ilisema Tanzania imeingia katika uchumi wa kipato cha kati kabla ya mwaka huo.

“Leo ni siku ya furaha, tunatakiwa kufurahi kwani tumeingia katika uchumi wa kati rasmi, tufurahi, ni rekodi,” anasema Dk. Abbasi ambaye amewahi kuwa katika ofisi ya BRN. 

Akifafanua kuhusu uchumi wa kipato cha kati, anasema ni mwananchi kuweza kutumia Dola za Marekani 1,036 hadi 4,045 huku uchumi wa kipato cha juu ukiwa ni kuanzia Dola 4,046 hadi 12,535.

SABABU ZA KUINGIA UCHUMI WA KATI

Dk. Abbas anayataja mambo yaliyosababisha Tanzania kufikia uchumi wa kati kuwa ni pamoja na amani na utulivu, mipango thabiti ya maendeleo tangu awamu ya kwanza ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mengine ni kutekeleza mipango ambayo Serikali imeipanga, kanuni ya maamuzi magumu ambayo imesaidia kuifanya nchi kufika ilipofikia na kuwekeza kwenye misingi ya kujitegemea.

“Pia nidhamu katika matumizi ya fedha za umma, miiko ya uongozi, uamuzi wa Serikali kuwekeza kwenye miradi mikubwa na kimkakati, kuwekeza kwenye maendeleo ya watu pamoja na uwekezaji wa sekta binafsi,” anasema Dk. Abbasi.

Anasema licha ya nchi kuingia katika uchumi wa kati, ni muhimu kujitathmini katika mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuchangamkia fursa za uwekezaji.

“Tuwe Jamhuri ya wapambanaji, jiongeze, jifunze mambo mapya, mimi najua hata hii dhana wataipotosha, sasa bishana na Benki ya Dunia,” anasema Dk. Abbasi.

NCHI NYINGINE

Tanzania sasa ni miongoni mwa nchi tano duniani zilizoingia kwenye kundi la nchi za kipato cha kati kwa kundi la chini, nyingine ni Algeria, Sri Lanka, Benin na Nepal. 

Katika Afrika kundi hili lina nchi 22 ambazo ni Angola, Algeria, Kenya, Benin, Senegal, Lesotho, Cameroon, Tunisia, Comoro, DR Congo, Ivory Cost, Morocco, Djibout, Misri, Zambia, Eswatin, Nigeria, Zimbawe, Ghana na Cape Verde.

WAZIRI WA FEDHA

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ambaye amekuwa katika utekelezaji wa hatua ya sasa kwa miaka mingi anasema hatua hiyo ina manufaa mengi kwa nchi kama vile kuongezeka kwa wigo wa upatikanaji wa fedha za mikopo ya kibiashara kwa utekelezaji miradi ya maendeleo, kuwa na uhuru wa kupanga matumizi na kuondokana na kadhia ya utegemezi.

“Ninaona fahari kwamba historia hii inaandikwa nikiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Nawashukuru wakulima, wavuvi, wafugaji, wafanyabiashara, wachimbaji madini, mabenki na wananchi wote kwa ujumla kwa mchango wao mkubwa katika mafanikio tuliyoyapata,” anasema Dk. Mpango.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here