Na KULWA MZEE -DAR ES SALAAM
MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi inatarajia kuanza kusikiliza siku tano mfululizo kesi ya kusafirisha dawa za kulevya inayomkabili Abdul Nsembo na mkewe Shamim Mwasha ambayo ilihamia huko hivi karibuni.
Kesi hiyo ilitajwa jana katika mahakama hiyo ambapo washtakiwa walisomewa maelezo ya tuhuma zinazowakabili mbele ya Jaji Elinaza Luvanda.
Baada ya kusomwa kwa maelezo hayo, kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa mfululizo kuanzia Mei 25 hadi 29.
Hivi karibuni katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, washtakiwa walisomewa maelezo ya mashahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai Jamhuri ina jumla ya mashahidi 12.
Vielelezo ni maelezo ya onyo kwa watuhumiwa wote wawili, hati ya ukamataji, ripoti ya uchunguzi wa maabara ya Serikali, fomu ya kuwasilisha sampuli maabara, taarifa ya usajili wa gari kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na bahasha zilizokuwa na dawa za kulevya.
Wankyo akisoma maelezo alisema inadaiwa Mei mosi, 2019 wakaguzi walikagua katika nyumba ya mfanyabiashara Nsembo iliyopo Mbezi Beach, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Alidai kuwa kwa mujibu wa maelezo ya mkaguzi, walifika eneo la tukio muda wa saa 2 usiku na kugonga geti ambalo lilifunguliwa na mlinzi aliyejitambulisha kwa jina la Bakari Senkokwa na baada ya kujitambulisha na kumweleza kilichowapeleka, aliwaeleza wasubiri amuite mwenye nyumba ambaye ndiye mwenye ufunguo.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, baada ya muda mfupi alitoka mama ambaye alijitambulisha kwa jina la Shamim Mwasha ambaye alikiri kuwa ndiyo mama mwenye nyumba na mke wa Nsembo.
Inadaiwa Shamim alipoulizwa kuhusu mume wake, alisema hakuwa anajua aliko kwani walikuwa na ugonvi wa kifamilia na hajui angerudi muda gani, lakini wao walimwomba awaruhusu wafanye ukaguzi naye akawaruhusu.
Kabla ya ukaguzi walimruhusu Shamim awakague, alifanya hivyo na kujiridhisha kwamba hawakuwa wamebeba kitu chochote hatarishi kwake.
Wankyo alidai kuwa walipofanya ukaguzi katika maeneo kadhaa hawakufanikiwa kupata chochote wala kumuona yeyote hadi walipoingia katika moja ya chumba na kukuta vipande vya Gypsum vikiwa vimeanguka, na alama ya mguu ikionyesha wazi kuwa kuna mtu alipanda darini muda mfupi uliopita.
Alidai mkaguzi alimwagiza mmoja wa askari alioongozana nao aliyemtambulisha kwa jina la Brown apande darini kuangalia kama kuna mtu, lakini hakuona mtu, na baada ya kurudi mara ya pili aligundua kulikuwa na mfuniko unaotokea upande wa nje kwa kupitia kwenye paa, hivyo aliufunua na kutoka nje kwenye kibaraza cha kuwekea tanki la maji ambalo Nsembo alikuwa amejificha nyuma yake.
Wankyo alisema maelezo hayo yaliendelea kudai kuwa Brown alimshusha Nsembo chini na kuendelea na upekuzi ambapo walifanikiwa kukamata vitu kadhaa ikiwemo pasi ya kusafiria, cheti cha kuzaliwa cha Nsembo, vifaa mbalimbali vya mawasiliano kama simu, kifaa cha kuhifadhia picha za CCTV na kifaa cha kuhifadhia nyaraka za kompyuta (external backup).
Mbali na vifaa hivyo, walikuta pia vikopo vinne vyenye unga ambao baadaye ulibainika kuwa ni dawa za kulevya na waliendelea na upekuzi katika magari ambapo katika gari moja aina ya Landrover Discovery lenye namba T 817 BQN nyuma ya kiti walikuta mfuko wa kitambaa uliowekwa kwenye mfuko laini wenye unga ambao baadaye ulibainika kuwa ni dawa za kulevya.
Alidai waliweka kumbukumbu ya vielelezo vyote na katika fomu maalumu na kuwekwa saini na wahusika wote wakiwemo washtakiwa.
Maelezo hayo pia yalithibitishwa na maelezo ya mashahidi wegine 11 waliobaki ambao maelezo yao yalishabihiana na maelezo ya Paschal.