Mkurugenzi wa zamani K’ndoni, wenzake kortini

0
656
Mussa Natty aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni

Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni, kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, jana imewafikisha mahakamani waliokuwa maofisa wa Manispaa ya Kinondoni  kwa makosa ya rushwa. 

 Waliofikishwa mahakamani ni Mussa Natty aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Baraka Mkuya aliyekuwa Mhandisi, Ismail Mafita aliyekuwa mhandisi wa Barabara na Ernest Ngolofu aliyekuwa Mkadiriaji  Majenzi.

Akitoa taarifa hiyo jana, Mkuu wa Takukuru Kinondoni, Pilly Mwakasege, alisema watu hao wanashtakiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka  kinyume na kifungu cha 31 Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  Na 11/2007  na kula njama kutenda kosa kinyume cha kifungu 32  cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Na 11/2007.

“Awali ofisi ya Takukuru ya Mkoa wa Kinondoni  ilipokea malalamiko yanayohusu Manispaa ya Kinondoni  kuwa kumefanyika ubadhilifu wa fedha  katika miradi ya ujenzi wa barabara za Journalism yenye urefu wa 0.53 km,  Feza/Senga yenye urefu 0.75 km na Serengeti yenye urefu 0.6 km  zilizopo katika manispaa hiyo  ikiwa ni pamoja na kumwongezea mkandarasi  kazi bila kufuata  taratibu za manunuzi,” alisema Mwakasege.

Alisema uchunguzi  dhidi ya tuhuma hizo  umebaini mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na  kuwa Manispaa ya Kinondoni iliingilia mkataba wa Kampuni ya Skol Building Contractor Ltd  wa Sh 2,006,532,500 kwa ujenzi wa barabara zilizopo katika manispaa  hiyo.

“Katika utekelezaji wa mkataba huo kuliongezeka kazi zenye nyongeza za jumla ya Sh 1,077,189,040 ambapo jumla ya kiasi cha Sh 959,756,769 kilishalipiwa kwa kazi  zilizoongezeka  na b do mkandarasi alidai Sh 117,432,271.

“Kazi hizi ni za nyongeza zilizofanyika na kulipwa,  hazikutolewa  kwa kufuata kanuni, sheria  na taratibu za manunuzi, idara ya ujenzi haikupata kibali cha bodi  ya zabuni ya manispaa hiyo cha kuendelea na kazi hiyo ya nyongeza ,” alidai Mwakasege.

Alidai watuhumiwa wametumia mamlaka yao vibaya  kinyume na kifungu  cha 31  cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Na 11/2007  na kwenda kinyume na  kanuni namba 61(2) na 61(4) na tangazo la Serikali namba 446 la mwaka 2013 kwa kuruhusu kazi ya nyongeza  kufanyika bila kupata kibali  cha Bodi ya Zabuni  ya Manispaa.

“Uchunguzi umekamilika na watuhumiwa watafikishwa mahakamani,  watafunguliwa mashtaka kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka  kinyume na kifungu  cha 31 cha Sheria  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na 11/2007  na kula njama  kutenda kosa kinyume  na kifungu cha 32 cha sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa  Na 11/2007,” alieleza Mwakasege.

Aidha alitoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano  ikiwa ni pamoja  na kutoa taarifa  za vitendo  vya rushwa kupitia mitandao ya simu  kwa kupiga  au kutuma ujumbe mfupi  kwa namba 113 na kufuata maelekezo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here