Asha Bani
Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uchaguzi na Uongozi, chini ya uratibu wa Mfuko wa Udhamini wa Wanawake Tanzania ( WFT) washauri kuwepo na mabadiliko katika sheria mbalimbali za uchaguzi.
Pia wamefanya uchambuzi wa sheria tano za uchaguzi kwa mrengo wa jinsia na kuzielezea mapungufu yake ambayo yanapaswa kufanyiwa marekebisho hayo.
Kwa mujibu wa mtandao huo malengo mahususi ya uchambuzi ni kutoa muhtasari wa mambo yaliyojitokeza kwenye baadhi ya Sheria za uchaguzi ili kubainisha mapengo yanayoweza kuwa kikwazo katika kutekeleza azma ya ujenzi wa demokrasia shirikishi kwa mrengo wa jinsia.
Mwenyekiti wa WFT ,Profesa Ruth Meena akizungumza kwa njia ya mtandao na waandishi wa habari alisema lengo la uchambuzi huo ni kutoa mapendekezo mahususi yatakayoongoza wadau mbalimbali katika kuchukua hatua stahiki zenye kukabiliana na sheria za ubaguzi wa aina zote hususani ubaguzi wa jinsia kwenye mchakato wa uchaguzi.
Alizitaja sheria zilizochambuliwa kuwa ni pamoja na sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 ya 2015, Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar namba 4 (2018)Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa namba 4 ya mwaka 1979 namba 292 kama ilivofanyiwa marekebisho mwaka 2010 na mwaka 2015)Sheria ya Serikali Za Mitaa ( Mamlaka za Wilaya Sura 287 kama ilivyorekebishwa 2002) na ile ya serikali za Mitaa za mmlaka za miji sura ya 288 na mamlaka za wilaya sura ya 287.
“ Lengo la Mkutano huu ni kuwezesha wanahabari kupata taarifa za kina zilizotokana na uchambuzi wa sheria zilizochambuliwa kwa mrengo wa Jinsia. Kimantiki, wanahabari ni muhimu sana kwenye ujenzi wa demokrasia shirikishi na kwenye harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi,”
“Aidha wanahabari ni kiungo kinachounganisha jamii, wanaowania kuomba dhamana ya uongozi kwa wapiga kura au kuwasilisha madai ya wapiga kura kwa wale wanowania kuomba dhamana ya uongozi.” aliongeza prof Meena.