Na ELIAS SIMON-DAR ES SALAAM
Taasisi isiyo ya kiserikali ya Tanzania Peace Foundation leo (jana), tarehe 23Novemba2019 imetoa rai kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo imeongelea swala la amani kwa vyama vyote ambavyo vimeshiriki uchaguzi na ambavyo havijashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Sadicki Godigodi amesema “ Sasa ni kipindi cha kampeni, Taasisi yetu ya Tanzania Peace Foundation inapenda kutoa wito kwa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki na visivyoshiriki katika uchaguzi huu kuzingatia suala zima la uzalendo na kulinda mshikamano wetu pamoja na amani ya nchi yetu”
Aidha kwa upande mwingine Bw. Sadicki Godigodi aliwaomba wananchi kuendelea kuwa watulivu na kuacha kushabikia mambo ambayo hayana tija kwa taifa letu bali kuyafuatilia yale ya msingi ambayo yanalenga kuleta maendeleo kwa nchi yetu.
Akiongezea mengine Bw. Sadicki Godigodi alisema ni vema viongozi wa vyama vya siasa kutoa kauli ambazo zitaendelea kudumisha amani na umoja wa kitaifa, kwa kuwa sote tunajenga nyumba hakuna haja ya kugombania fito.
Kwa upande mwingine Bw. Sadicki Godigodi alitumia nafasi yake pia kumpongeza Mkuu wa nchi Mhe. Raisi Dkt JOHN POMBE MAGUFULI kwa kazi kubwa na majukumu mazito ya kitaifa anayofanya na kuiwezesha nchi kufika hapo tulipo.