27.4 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Prof. Mbarawa apambana na mkandarasi anayedaiwa kukwamisha miradi mikoa nane

Na MWANDISHI WETU-SERENGETI

WAZIRI wa Maji Profesa Makame Mbarawa ameagiza mamlaka zinazohusika kuvunja mara moja mikataba na wakandarasi wawili baada ya kushindwa kukamilisha miradi  miwili ya maji wilayani Serengeti mkoani Mara.

Waziri Mbarawa alitoa maagizo hayo jana kwa nyakati tofauti baada ya kutembelea miradi ya maji katika kijiji cha Mbalibali pamoja na mradi wa ujenzi wa chujio la maji katika mji wa Mugumu ambapo hakuridhiswa na utekelezaji wa miradi hiyo.

Awali akiwa katika kijiji cha Mbalibali, waziri huyo alielezwa na Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini ( Ruwasa)  Wilaya ya Serengeti, Andrew Kisaro kuwa mradi wa maji wa kijiji hicho wenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 1.1 uliokuwa ukitekelezwa na kampuni ya Urban and Rural Engineering Services mkandarasi huyo hajaonekana eneo la kazi kwa ziadi ya miezi 11 sasa.

Kisare alisema kutokana na hali hiyo ofisi yake imejitahidi kuwasiliana na mkandarasi huyo ili aweze kufika katika eneo la kazi kuendelea na kazi bila mafanikio ambapo alisema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa  ni pamoja na kumuandikia barua sita lakini hakuna majibu wala utekelezaji.

Alisema kutokana na hali hiyo ofisi yake tayari imeanza mchakato wa kuvunja mkataba na mkandarasi huyo kwa vile ameenda kinyume na makubaliano na kwamba mchakato huo unaofanywa na wanasheria wa halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

Kisare alisema mradi huo ambao ukikamilika unatarajiwa kunufaisha zaidi ya watu 7,000 kutoka katika vijiji vya Mbalibali na Kitunguruma tayari umetekelezwa kwa asilimia 45 tu huku mkandarasi huyo akiwa amekwishalipwa zaidi ya sh. milioni 290.

Kutokana na hali hiyo Waziri Mbarawa aliigiza Ruwasa Wilaya ya Serengeti kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuhakikisha kuwa mkataba huo uwe umevunjwa kabla ya ijumaa ijayo.

Alisema baada ya mkataba kuvunjwa wizara ya maji itatuma fedha Jumatatu ijayo ili mradi uweze kukamilishwa chini ya usimamizi wa Ruwasa wenyewe na kutoa muda wa miezi miwili kwa ajili ya mradi kukamilika na wananchi waweze kupata huduma ya maji.

Kuhusu  mradi wa chujio la maji mjini Mugumu, Mkurugenzi wa wa Muwasa, Robert Lupoja alisema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 2.1 ulitarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu lakini hadi sasa bado haujakamilika.

Lupoja alisema mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya M/S PET  hadi sasa umefika asilimia 80 ingawa kasi ya mkandarasi huyo imekuwa ni ya kususasua licha ya   Muwasa kumtaka mara kwa mara mkandarasi kukamilisha kazi hiyo juhudi ambazo amedai kuwa hazijazaa matunda.

Lupoja alisema hatua mbalimbali zimechukuliwa na ofisi yake katika kumkumbusha mkandarsi umuhimu wa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati ikiwa ni pamoja na kumuandikia barua zaidi ya tano bila mafanikio.

Lupoja alieleza kuwa kutokana na hali hiyo ofisi yake tayari imeanza mchakato wa kuvunja mkataba na mkandarasi huyo ili utaratibu mwingine uweze kufanyika kwa ajili ya kukamilisha mradi huo ambao unatarajiwa kuhudumia zaidi  ya watu 53,000.

Kutokana na maelezo hayo,  Waziri Mbarawa aliitaka mamlaka hiyo kukamilisha mchakato huo kwa haraka zaidi ili mkataba huo uweze kuvunjwa kwani mkandarasi huyo hana uwezo tena wa kukamilisha kazi hiyo.

Alisema  mkandarsi huyo ameshindwa kukamilisha kazi zaidi ya nane katika mikoa tofauti tofauti na kwamba ingawa hana uwezo wa kufanya kazi lakini amekuwa akipata kazi kwa njia za rushwa kwa masaada wa baadhi ya watendaji kutoka wizarani kwake.

Alisema  mkandarasi ni miongoni mwa makandarasi wanne ambao zao ni za ubababishaji wa hali ya juu na kuwa kazi zao nyingi zinashindwa kukamilika kutokana na ujanja ujanja huku akisema kuwa mkandarasi huyo amekuwa na tabia  kuhamisha fedha kutoka katika mradi mmoja kwenda mwingine na mwisho wa siku hakuna kazi inayofanyika hivyo kuagiza mkataba huo uvunjwe haraka sana ili mradi uweze kutekelezwa na Muwasa wenyewe. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,903FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles