30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Watoto 20 kupasuliwa moyo kwa milioni 40/-

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

KAMPUNI ya mafuta ya Puma Energy, imeunga mkono kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ya kuokoa maisha ya watoto wanaogua ugonjwa wa moyo kwa kuchangia Sh milioni 40 ili kufanikisha upasuaji kwa watoto 20.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa mashindano ya michoro ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa mkoa huo kwa mwaka 2019, Mkurugenzi wa Puma Energy, Dominic Dhanah, alisema hatua ya kuunga mkono kampeni hiyo ni kuhakikisha wanaokoa maisha ya watoto ambao wazazi wao hawana uwezo wa kugharamia matibabu.

Akizungumzia mafunzo ya usalama barabarani kwa watoto wa shule za msingi, alisema yamesaidia kupunguza ajali maeneo ambayo wametoa mafunzo, hivyo wanaamini kwa kufanya hivyo wanaokoa kizazi cha sasa na kijacho kwa kuwa elimu ya matumizi bora ya barabara inaendelea kusambaa.

“Lengo kubwa la mpango huu ni kuwafanya watoto hawa kuwa na uelewa wa matumizi ya barabara wakiwa bado wadogo. Tunaamini kwa kufanya hivyo tunaongeza uelewa kuhusu dhima nzima ya usalama barabarani kwa Watanzania wengi zaidi,” alisema Dhanah.

Alisema kazi hiyo kwa mwaka huu imefanyika katika mikoa ya Dodoma na visiwani Zanzibar na kwamba jumla ya shule 34 zitafikiwa kwa mpango huu kwa mwaka huu.

“Lengo letu kama kampuni ni kuongeza wigo ili kufikia shule nyingi zaidi nchi nzima.

“Pia tutaendelea kuwekeza katika kampeni ya usalama barabarani tukishirikiana na Serikali kupitia Jeshi la Polisi ili kuokoa maisha ya Watanzania,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema Kampuni ya Puma imetoa Sh milioni 40 ambazo zinagharamia matibabu ya watoto 20 ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo, lakini wazazi wao hawana uwezo wa kulipia matibabu.

“Puma wameonyesha njia ya kujali na kutusaidia kwenye moyo. Niliomba msaada huo katika mkutano wa SADC. Nina watoto 500 pale Muhimbili wanaumwa moyo.

“Mimi nikialikwa mahali ninaomba msaada kwa wananchi wangu. Dominick wa Puma nilimuomba na gharama za matibabu kwa kila mtoto ni Sh milioni 2.

“Kwa kiasi hiki cha fedha Sh milioni 40 sasa tunakwenda kurudisha tabasabu kwa watoto 20. Watapata operesheni…

“Hata nilipokutana na Balozi wa Dubai baada ya kumweleza hili, yeye alikwenda kuleta madaktari ambao walifanya upasuaji wa matibabu kwa watoto 50.

“Mwezi ujao nitaunda kamati ya watu saba kwa ajili ya kusaka Sh bilioni 1, ili mpaka tukifika Desemba mwaka huu watoto wote wawe wamefanyiwa upasuaji,” alisema Makonda.

Akizungumzia idadi ya watu wanaopata ajali za barabarani, alisema kwa sasa imepungua kutokana na elimu ya usalama barabarani.

“Tuna imani watoto milioni moja watakuwa na uelewa iwapo wataelimishwa na wenzao.

“Watumia vyombo vya moto watambue kila mmoja ana jukumu la kufuata usalama barabarani.

“Kabla ya Desemba kutakuwa na ‘check up’ ya bure kwa wanaotaka kwenda likizo.

“Mafundi wa bure watakuwapo, nataka waende vizuri kula likizo na warejee tena Dar wakiwa salama. Trafiki kwenye mwendokasi inafanya vibaya,” alisema.

Makonda pia aliagiza kukamatwa kwa madereva wanaotumia barabara za mwendokasi.

“Wanaotumia barabara ya mwendokasi wakamatwe, hakuna gari, pikipiki wala mtu anayepaswa kuitumia, Mwakyoma (RTO) apeleke trafiki hapo,” alisema.

Hadi sasa wanafunzi zaidi ya 20,000 wa shule za msingi katika shule tisa za Dar es Salaam wamepata mafunzo ya usalama barabarani.

Katika mashindano hayo, Shule ya Msingi Kibamba iliibuka mshindi wa kwanza na kuzawadiwa Sh milioni nne.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles