Polisi wahaha kuwasaka waliomteka Mo

0
507

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

WATUHUMIWA wanaosakwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhusika kumteka mfanyabiashara Mohammed Dewji  ‘Mo’ hawajapatikana na upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Hayo yalibainishwa jana na Wakili wa Serikali, Daisy Makakala wakati kesi hiyo inatajwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Makakala alidai upelelezi wa kesi hiyo unaendelea, hivyo aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa.

Alidai wanaendelea kuwatafuta washtakiwa wengine ili waunganishwe katika kesi hiyo, ambapo imepangwa kutajwa  Oktoba 15.

Mshtakiwa ambaye ameshafikishwa mahakamani hapo ni dereva wa teksi, mkazi wa Tegeta, Mousa Twaleb.

Watuhumiwa wengine ambao upande wa mashtaka unawatafuta ni raia wanne wa Msumbiji na mmoja wa Afrika Kusini wanaodaiwa kumteka mfanyabiashara huyo.

Washtakiwa hao ni Phila Tshabalala raia wa Afrika Kusini, Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior wote raia wa Msumbiji.

Katika kesi hiyo, inadaiwa Mei Mosi na Oktoba 10, mwaka jana, katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na Johannesburg nchini Afrika Kusini, kwa makusudi washtakiwa wote kwa pamoja waliendesha genge la uhalifu.

Pia inadaiwa Oktoba 11, mwaka jana maeneo Hoteli ya Colloseum wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb pamoja na watu wengine ambao hawapo mahakamani, walimteka nyara Mo kwa nia ya kumuhifadhi kwa siri na kumuweka maeneo ambayo ni hatari.

Inadaiwa Julai 10, mwaka jana maeneo ya Mbezi Beach wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Twaleb alitakatisha fedha Sh 8,000,000 wakati akijua fedha hizo ni kosa la kushiriki genge la uhalifu na makosa ya kupanga.

Mo alitekwa nyara Oktoba 11, mwaka jana alfajiri maeneo ya Hoteli ya Colloseum wakati akienda kufanya mazoezi, na alipatikana Oktoba 20, mwaka huo huo katika eneo la Gymkhana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here