30.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

‘Vikundi vya kigaidi Somalia hatari kwa Afrika’

Kundi la Al-shabaab
Kundi la Al-shabaab

Na Fredy Azzah, Dar es Salaam

MWAKILISHI wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Somalia, Balozi Augustine Mahiga, amesema kuna mtandao wa kutengeneza magaidi nchini Somalia kwa lengo la kufanya uhalifu kwenye nchi mbalimbali, zikiwamo za Afrika Mashariki.

Balozi Mahiga alisema hayo jijini Dar es Salaam jana, kwenye mdahalo wa marais wastaafu wa Afrika (African Leadership Forum) ambao pamoja na mambo mengine, walijadili suala la maendeleo na usalama kwa bara la Afrika.

Marais waliohudhuria mkutano huo ni Benjamin Mkapa, aliyekuwa Rais wa Botswana, Festus Mogae, aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki na aliyekuwa Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo.

Balozi Mahiga alitoa kauli yake alipokuwa akijibu swali la mmoja wa watu waliohudhuria kwenye mkutano huo, ambaye alisema kuna baadhi ya vijana wanapewa mafunzo ya kigaidi nchini Somalia na kwenda kujiunga na vikundi kama vya Boko Haram.

Akijibu swali hilo, Balozi Mahiga alisema wamebaini kuwa vikundi hivyo vina mtandao unaovisaidia kupata vijana na kuwapa mafunzo na kwenda kutekeleza ugaidi kwenye maeneo mbalimbali.

“Mafunzo wanapatia Somalia, lakini pale siyo eneo wanalolenga kwa ajili ya kufanya mashambulizi yao, wanalenga kwenye nchi mbalimbali kama za Afrika Mashariki na tumeshuhudia hayo yakitokea na wengine wanakwenda huko kujiunga na Boko Haram,” alisema.

Baada ya kauli hiyo, Rais Obasanjo alimuuliza Balozi huyo kwa sasa ni wapi vijana vikundi hivyo vinalenga zaidi.

Hata hivyo swali hilo halikujibiwa, baada ya muongoza mjadala kumkatisha Obasanjo na Balozi Mahiga.

“Nataka nijue ili nikajipange,” alisema Obasanjo na kufanya watu waliokuwa ukumbini kuangua kicheko.

Suala la usalama na vurugu kwenye nchi mbalimbali za Afrika lilionekana kuchukua sehemu kubwa ya mjadala huo.

Katika siku za karibuni, kumekuwa na matukio ya kigaidi katika nchi ya Kenya ambayo yamekuwa yakihusishwa na kikundi cha al-Shabaab, ambacho pia mara kadhaa kimekiri kuhusika.

Katika Mkoa wa Arusha kumekuwa ya matukio ya ulipuaji wa mabomu kwenye maeneo mbalimbali, ambapo kikundi hicho kimekuwa kikihusishwa ingawa hakijawahi kukiri kuhusika nayo.

Kwa upande wa suala la uchumi, aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Mbeki, alisema kuwa nchi nyingi za Afrika zina sera nzuri, lakini tatizo ni utekelezaji.

Akichangia mada hiyo kuhusu uchumi, Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Cleopa Msuya, alisema ni vyema nchi za Kiafrika zijiangalie pamoja na mipango yake.

“Wakati nikiwa madarakani tulikuwa tunakwenda kwenye mikutano kama ya Benki ya Dunia na IMF (Shirika la Fedha Duniani), wakati wa kuwakilisha mipango unaona kabisa kuwa haina kitu, tujiulize hivi mipango yetu tunayoiwakilisha huko ni bora,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

4 COMMENTS

  1. Marais wengi wa Afrika bado ni ving’ang’anizi madarakani, ukosefu wa Demokrasia ya kweli na haki za Binadamu ndio chanzo kikuu cha kukosekana kwa usalama na kudumaa kwa maendeleo kiuchumi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles