32.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa wawavaa viongozi wa dini

Baadhi ya viongozi wa Ukawa wakijadiliana jambo
Baadhi ya viongozi wa Ukawa wakijadiliana jambo

Patricia Kimelemeta na Michael Sarungi

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umesema unashangazwa na hatua ya baadhi ya viongozi wa dini nchini kuwataka warudi ndani ya Bunge Maalumu la Katiba bila kuangalia hoja ya msingi iliyowafanya wasusie Bunge hilo.

Kutokana na kauli hiyo, UKAWA wamesema wamesikitishwa na hatua hiyo, huku wakisisitiza msimamo wao uko pale pale wa kutorejea ndani ya Bunge la Katiba.

Kauli ya UKAWA imekuja siku chache baada ya baadhi ya viongozi wa dini, wakiwamo wa Kiislamu kupitia hotuba za sala ya Eid El-Fitri kuwataka kurejea ndani ya Bunge hilo ili Taifa liweze kupata Katiba Mpya kwa wakati.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema viongozi wa dini wamekuwa wakiegemea upande mmoja wa kuwatetea Chama Cha Mapinduzi (CCM) bila ya kusikiliza upande wao.

“Tunawashangaa viongozi wa dini ambao wamekuwa wakitoa matamko kwa nyakati tofauti ya kutusihi turudi bungeni bila ya kutuita na kusikiliza hoja zetu.

“Tunawaheshimu sana kwa sababu ni viongozi wetu, lakini pia wanapaswa kutambua kuwa, nafasi walionayo katika jamii hawapaswi kusimamia upande mmoja katika suala hili,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema viongozi wana nafasi kubwa ya kuzungumzia suala hilo katika jamii, kwa sababu wamepewa mamlaka ya kuwaongoza kupitia imani katika dunia, hivyo UKAWA inaheshimu sana wito kwa viongozi hao, wakiwemo wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC).

Alisema ushauri wao ni mzuri, lakini katika kipindi hiki hawawezi kurudi bila kuhakikisha kuwa wajumbe wenzao, wakiwamo wa CCM wanajadili rasimu iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba.

“Unajua viongozi hawa wamekuwa na vikao mbalimbali na viongozi wa juu wa CCM vya kujadili suala hili, ndiyo maana wamekuwa wakitoa matamko, lakini hawajawahi hata siku moja kukaa na sisi na kujadiliana kuhusu suala hili wakati sisi wote tupo kwa ajili ya kujadili katiba hii,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Umoja huo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alisema sababu za UKAWA kususia vikao vya Bunge hilo ni pale walipoona wajumbe wenzao wa CCM wakijadili mambo yasiyokuwamo ndani ya rasimu ya Jaji Warioba.

Alisema sababu nyingine ni pamoja na Mwenyekiti wa Bunge hilo ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kuongoza kwa ubabe wajumbe wa Bunge la Katiba.

“Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, aliongoza Bunge kwa ubabe, ikiwa ni pamoja na kubadili kanuni kwa kumtanguliza Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba kuwasilisha rasimu ya katiba kwa wajumbe wa Bunge hilo.

“Pia Sitta alishindwa kuwadhibiti wajumbe wa CCM pale walipokuwa wakitoa kauli za matusi, kebehi, uchochezi na lugha za ubaguzi, hali iliyosababisha kususia vikao hivyo,” alisema Mbowe.

Alisema kutokana na hali hiyo, viongozi wa dini walipaswa kumuita na kumuonya kwa makosa hayo, badala yake wanatoa tamko la kuwataka warudi bungeni.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema kuwa muundo wa serikali tatu ni roho ya nchi, hivyo basi huwezi kujadili masuala mengine kabla ya kujadili muundo wa serikali.

“Huwezi kukaa kwenye kikao na kujadili mambo madogo madogo bila ya kujadili muundo wa nchi, kwa sababu ndio roho ya uongozi ndani ya nchi,” alisema Mbatia.

Alisema mpaka sasa viongozi wa CCM wamekuwa wakitoa matamko ya kuwataka warudi bungeni bila kuwaomba radhi kwa vitendo walivyofanya, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa hawana dhamira ya ukweli katika hilo.

Alisema uamuzi wa kurudi au kutorudi kwenye Bunge la Katiba utatolewa kesho (leo) baada ya kukutana na Baraza la Vyama vya Siasa, Msajili na viongozi wakuu wa CCM ili kujadili suala hilo.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. Tumefanya makosa makubwa kuwaondoa tume iliyoandaa rasimu kabla ya katiba haijakamilika. Wenye uwezo na nafasi nzuri ya kutoa mafafanuzi ya vifungu vya rasimu ya katiba ni ile tume iliyoandaa rasimu hiyo. Kuwaondoa mapema na kuwaweka pembeni kunaonyesha kuwa kuna agenda ya siri kuhusu rasimu yenyewe

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles