27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

JK: Ukawa unabadilika kama upepo

Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS Jakaya Kikwete, amesema sababu zinazotolewa na Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA), zimekuwa zikiongezeka na kubadilika kadri siku zinavyosonga kama upepo wa kisiasa unavyokwenda.

Pamoja na hali hiyo, amewataka warejee bungeni naye yupo tayari kutoa ushirikiano pale unapohitajika ili kuweza kunusuru mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Kauli hiyo aliitoa jana katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi ambapo alisema hivi sasa UKAWA wamekuwa wakizungumzia mambo mawili ikiwemo Bunge Maalumu kukosa uhalali na mamlaka ya kuifanyia mabadiliko yoyote Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Mbali na hili, alisema kuwa wamekuwa wakidai kuwa kazi ya Bunge Maalumu la Katiba ni kujadili na kupitisha tu Rasimu ya Katiba ya Tume na siyo kubadili chochote pamoja na kutoa sharti la wao kurudi bungeni ni kuhakikishiwa kwamba, kitakachojadiliwa ni Rasimu ya Tume.

“Mimi nimehusika katika kubuni wazo la kuwa na mchakato wa kuandika Katiba Mpya na katika maandalizi ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya kuongoza na kuendesha mchakato huo. Kwa kweli sikumbuki wakati wowote katika vikao vya Baraza la Mawaziri kujadili Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba tulipozungumzia Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa haiwezi kufanyiwa marekebisho na Bunge Maalumu la Katiba.

“Mimi siyo mwanasheria na hivyo nakiri kwamba naweza kuwa na upungufu katika kuelewa maana ya baadhi ya maneno ya kisheria. Hata hivyo, sikumbuki kuwepo kwa kifungu chochote katika sheria kinachosema kuwa Bunge Maalumu la Katiba halina mamlaka hayo. Tangu tulipoyasikia maneno hayo yakisemwa nimeuliza nithibitishiwe ukweli wa madai hayo bado sijaambiwa vinginevyo kama ukweli huo upo naomba nisaidiwe,” alisema Rais Kikwete.

Alisema anashangazwa na kauli zinazodai kwamba, maneno yaliyotumika katika sheria hayaakisi dhana inayotolewa kuwa kazi ya Bunge Maalumu la Katiba ni kubariki Rasimu na siyo kufanya vinginevyo.

Alisema amekuwa akijiuliza na kupata shida kuelewa mkanganyiko unatokea wapi na hasa wale wanaoongoza kuhoji mamlaka ya Bunge Maalumu kuwa ni wale wale waliotunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba tena hatua kwa hatua.

Rais Kikwete alisema anashangazwa zaidi na waliotunga Kanuni za Bunge Maalumu ndiyo wanaoongoza kuhoji uhalali wa kile walichokitunga.

Alisema hivi sasa kuna madai yanayotolewa na kuenezwa na UKAWA kwamba, kinachojadiliwa bungeni siyo Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ndiyo maana wanaweka sharti la kujadiliwa Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba ndipo warudi bungeni.

Alisema madai hayo yanampa tabu kuyaelewa kwao wajumbe hao nao walikuwepo katika siku zote 19 za Kamati 12 zilipokutana kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita za Rasimu ya Tume.

“Haya maneno ya sasa kwamba kinachojadiliwa bungeni siyo Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba, bali nyingine kabisa ambayo wanadai eti ni ya CCM yanatoka wapi.

“Mimi nadhani kuwa huenda katika kamati kumefanyika marekebisho kwenye rasimu ambayo hayakuwapendeza. Kama hivyo ndivyo, wawe wakweli kuhusu jambo hilo kuliko kusema mambo yasiyowakilisha ukweli halisi wa rasimu inayojadiliwa,” alisema.

“Matokeo yake ni kuwafanya wafuasi wao na wapenzi wao na hata watu wengine waamini kuwa kinachojadiliwa siyo Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba bali nyingine tena ni ya CCM. Jambo hilo si kweli na wenyewe wanajua, ila sijui kwanini wameamua kupotosha ukweli,” alisema Rais.

Kutokana na mkanganyiko huo, alisema kinachomshangaza zaidi kama hawakuridhishwa na yaliyofanyika, kwanini wasingetumia mifumo waliyojitengenezea wenyewe kwenye Kanuni kumaliza tofauti zao.

“Kilicho muhimu ni kwa pande zote kuwa na dhamira ya dhati ya kutoka hapa tulipo sasa. Kama utashi wa kisiasa upo kwa kila mmoja wetu, hilo ni jambo linalowezekana kabisa. Narudia kuahidi utayari wangu wa kusaidia kadri inavyowezekana tusonge mbele,’’ alisema.

Alisema ikiwa utaacha mifumo ya maridhiano ndani ya Bunge ukaenda nje kwa wananchi au vyombo vya habari na mitandao si jawabu la tatizo.

“Ndiyo maana nashawishika kuunga mkono wale wote wanaowasihi wajumbe wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na wengine warejee bungeni. Watumie mifumo maalumu ya Bunge iliyowekwa na kanuni kutafuta maridhiano.

“Hali kadhalika, wasichoke kuwa na mawasiliano na vyama vingine vya siasa na hasa CCM kutafuta maelewano. Mimi niko tayari kusaidia pale watakapoona inafaa kufanya hivyo kama ambavyo nimekuwa nikifanya siku za nyuma.

“Nililolisema mwanzoni kabisa mwa mchakato na nalirudia tena leo kwamba, ili tuweze kufanikiwa kupata Katiba Mpya ambayo sote tunaitaka, maelewano baina ya wadau wakuu wa kisiasa ni jambo lisilokuwa na badala yake. Vinginevyo kupata theluthi mbili kwa pande zote mbili za Muungano haitawezekana.”

Aidha, alimpongeza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kwa uamuzi wa kuvikutanisha vyama vinne vikuu vya siasa kujadili namna ya kuondoa mtihani uliopo sasa katika mchakato wa Katiba.

Aliwataka viongozi wa vyama hivyo kuitumia vyema fursa ya majadiliano kuukwamua mchakato kwa masilahi ya nchi yetu na watu wake.

Alisema hivi karibuni kumekuwepo pia madai yanayoelekeza lawama kwake kwamba mambo yalikuwa yanaenda vizuri mpaka pale alipotoa hotuba ya ufunguzi wa Bunge Maalumu ndipo yalipoharibika.

“Pili nalaumiwa kwamba nawezaje kuikana Rasimu ya Katiba ambayo na mimi ni mmoja wa watu waliotia sahihi katika Rasimu hiyo. Niruhusuni nianze na hili la pili. Nadhani ndugu zetu wanaotoa madai haya yametafsiriwa isivyo sahihi yangu katika Gazeti la Serikali lililotangaza rasmi Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Alisema alichokifanya ndani ya Bunge la Katiba ni kutoa maoni yake kuhusu baadhi ya vipengele vya Rasimu hususan uandishi na dhana mbalimbali zilizokuwamo. Ambapo hakuona kosa kwa kufanya hivyo.

“Lakini pia mimi ndiye Rais wa nchi yetu, ninayo dhamana ya uongozi na ulezi wa taifa letu. Itakuwaje kwa jambo kubwa la hatima ya nchi yetu nilinyamazie kimya,’’ alisema.

Mashambulizi ya mabomu

Akizungumzia mashambulizi ya mabomu jijini Arusha, alisema watuhumiwa waliokamatwa safari hii wanaelekea kutoa sura nzuri zaidi ya mtandao wa watu wanaofanya vitendo hivi vya kikatili Arusha na kwingineko nchini.

Alisema watu 38 wameshafikishwa mahakamani, wengine 8 watafikishwa mahakamani leo na uchunguzi na msako unaendelea kote nchini kuwapata watuhumiwa wengine.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. pamoja na maelezo marefu sana kinachotakiwa ni kujadili rasimu ya Warioba ambayo inabeba maoni ya wananchi. Pia kuacha matusi, kejeli, madharau na matumizi ya vitisho.Hata hivi Rais anajaribu kujinasua kutoka katika mtego huu lakini haitakuwa rahisi, kwa sababu hayo anayosema yamechelewa sana.Shida moja ni pale yeye mwenyewe anapoona hakufanya kosa wakati jamii inaona amefanya kosa. je, mtu wa namna hii utamsaidia vipi ili aweze kuona kosa lake? UNyenyekeve ndiyo silaha kubwa na kutafuta masilahi ya taifa siyo ya chama chake CCM. Haya tukiyaeleza baadhi ya wanachama tawala wanafikiri mara moja ni chuki, fitina, na majungu, lakini “Ukweli utatuweka huru.” Suala siyo Ukawa waende kwanza sivyo, kwanza Rais na wajumbe wa Bunge la katiba waandikishane kwamba hizo kazosoro hazitarudi, wakienda bungeni wajue kinachoendelea na siyo kufika huko waanze tena mchakato wa kusuluhisha, na mbona kipindi chote cha likizo ya bunge la katiba jitihada hizo zilikuwa si za moto?

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles