NA JOHN MADUHU
MBUNGE wa zamani wa Jimbo la Busega Mkoa wa Simiyu, Dk. Raphael Chegeni, ameitaka serikali kuchunguza ajira za ukabila, upendeleo na undugu katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa vile zimetajwa mara kadhaa kutolewa kwa watoto wa vigogo.
Ametoa kauli hiyo siku chache baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kufuta ajira zaidi ya 200 zilizokuwa zimetangazwa na Idara ya Uhamiaji. Ajira hizo zilidaiwa kutolewa kwa misingi ya undugu wa wafanyakazi wa idara hiyo.
Dk. Chegeni alisema kwa vile serikali imeamua kufanya hivyo basi ni wakati muafaka kufuatilia BoT ambayo pia ilitajwa kutoa ajira kwa watoto wa vigogo kwa misingi ya kulindina.
Alionyakuwa serikali inapaswa kujenga utaratibu wa kuwajibishana badala ya kulindana ili nafasi za ajira ziwe kwa watanzania wote na siyo kikundi fulani cha watu.
Akizungumza na MTANZANIA jijini hapa, Dk. Chegeni pamoja na kuipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani kwa uamuzi huo, amesema ajira za upendeleo kwa kufuata misingi ya undugu, ukabila na udini zitaliangamiza taifa.
Alisema limekuwapo tatizo sugu kwa vigogo wa nchini kuwachomeka ndugu zao katika ajira mbalimbali zinazotangazwa bila kujali kama wana uwezo au sifa za kushika nyadhifa hizo hali ambayo inawakatisha tamaa watoto wenye uwezo lakini ndugu zao hawajulikani.
“Kuna vijana wengi wa Tanzania ambao hawana uwezo wamekuwa wakidhulumiwa haki yao ya kupata ajira. Sasa ajira zinapatikana kwa kujuana na siyo kwa uwezo wa muombaji, hii ni kansa inayolitafuna taifa lazima tujenge utamaduni wa kuwajibishana,” alisema.
Dk. Chegeni ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Busega mkoani Simiyu alisema lazima Serikali iwachukulie hatua kali wale wote waliohusika katika mtandao wa ajira za kujuana ndani ya Idara ya Uhamiaji.
Alisema Serikali inatakiwa kuwa na mikakati kabambe ya kukabiliana na tatizo la ajira nchini kwa kuiwezesha sekta binafsi kuajiri vijana wanaohitimu vyuo vikuu kwa sababu kwa sasa Serikali haina uwezo wa kuajiri.
Naunga mkono ajira za BoT zichunguzwe na taarifa ya wazi itolewe kwenye vyombo vya habari kama ilivyokuwa kwa ajira za wizara ya mambo ya ndani. Kuna ukweli kuwa wanaoajiriwa ni ndugu, jamaa na watoto wa vigogo tu, ndiyo maana hata
mishahara inayolipwa hata kwa mhudumu tu ni tofauti/iko juu kuzidi hata ile inayopendekezwa na kuombwa na TUCTA.