Mwandishi Wetu- Dodoma
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amewataka wananchi wafuate sheria kwa kujiepusha kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya Hifadhi ili kujenga uhusiano mzuri baina yao na wahifadhi.
Aliwataka wananchi kuwachukulia wahifadhi hao kama rafiki wa umma na watendaji waliotumwa na Serikali kulinda maliasili kwa niaba yao.
Akizungumza na watumishi wa pori la akiba la Swagaswaga katika Wilaya ya Chemba jijini Dodoma jana, Waziri Kanyasu alisema wahifadhi wamepewa jukumu la kulinda hifadhi za Taifa na wamekuwa wakifanya kazi nzuri ya kuifanya Tanzania iendelee kuwa na maeneo mazuri yaliyohifadhiwa.
”Sisi ni wa moja hakuna haja ya kujengeana uhasama kati yetu,wananchi wafuate sheria za uhifadhi na wahifadhi fuateni sheria wakati mnapokabaliana na wananchi,” alisema.
Aliema wahifadhi wa wanyamapori na misitu wanazilinda rasilimali hizo kwa ajili wote, vitu kama mvua, hali ya hewa safi pamoja na mvua ni moja ya faida za moja kwa moja zinazopatikana kutokana na maeneo yaliyohifadhiwa vizuri.
Alisema wahifadhi wameajiriwa kwa mujibu wa sheria hivyo hutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili ya kazi zao na pale wanapokiuka sheria mamlaka zinazohusika huwachukulia hatua.
“Sisi kama wizara tunaamini wahifadhi wetu wanafanya kazi nzuri, pale ambapo wamekuwa wakilaumiwa kwa kuwapiga na kuwanyanyasa watu kwa namna yoyote ile tumetuma tume maalumu kuchunguza na kuchukua hatua,” alisema
Alisema uchunguzi unapofanyika na ikathibitika kuwa tukio lililofanyika halikuongozwa na matumizi ya sheria na kuwepo kwa haki wizara imekua ikichukua hatua.
Alisema wahifadhi ni watu muhimu saba kwa vile bila wao hakuna uhifadhi unaoweza kuendelea nchini akibainisha kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakipinga juhudi za uhifadhi kwa kuwatetea watu wanaovunja sheria.
“Kuna watu wanatamani kuona misitu na wanyamapori wote tunawamaliza ili wapate maeneo ya malisho na kilimo, nawambieni tukithubutu kufanya hivyo huu ndo utakuwa mwisho wetu wa maisha,” alisema.
Alisema yapo madhara makubwa yanayoweza kutokea kama hakutakuwa na uhifadhi imara ikiwemo maeneo mengi ya nchi kugeuka kuwa jangwa kutokana na uharibifu wa misitu, ukosefu wa mvua, ukosefu wa maji, chakula na ukosefu wa hewa safi.
Kwa upande wake, Meneja wa Pori la Akiba la Swagaswaga, Alex Choya alisema kumekuwa na tuhuma za vitendo vya ukatili dhidi ya raia vinavyofanywa na baadhi ya askari wa hifadhi za Taifa na kutoa wito kwa wananchi wote wenye ushahidi na taarifa juu ya vitendo hivyo kuziwasilisha ili hatua stahiki zichukuliwe.