27.6 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

Bodi ya Utalii yapiga kambi India

Na ELIYA MBONEA-ARUSHA


MAONYESHO ya utalii yanayoshirikisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya utalii nchini India, yanatarajiwa kuongeza watalii kutoka nchini humo kutembelea Tanzania.

Mwaka 2017 Tanzania ilipokea idadi ya watalii 39,115 kutoka nchini India.

Tayari Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), imepiga kambi kwenye maonyesho hayo ukiwa ni mkakati wake kupenya kwenye masoko ya utalii nchini humo na kuwashawishi watalii waifanye Tanzania kuwa chaguo namba moja la utalii barani Afrika.

Akizungumzia mikakati hiyo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TTB, Devota Mdachi, alisema maonesho hayo yatatoa fursa kwa wadau wa utalii India kufahamu kwa kina kuhusu utalii na kushirikiana kibiashara na wadau wa utalii nchini.

“Pamoja na kuuza vivutio, tunatarajia wadau hawa wataitumia vizuri ndege yetu mpya 787-8 Dreamliner kuwaleta watalii Tanzania. Na juhudi zinazofanywa na Serikali zitaongeza idadi ya watalii kutoka soko la utalii la India,” alisema Mdachi.

Alisema tayari wamefanya maonyesho mji wa Ahmadabad, Crowne Plaza,  ambapo Septemba 21, mwaka huu wanatarajiwa kufanya maonyesho katika mji wa Mumbai, Hotel Orchid.

“Tulianza Septemba 17, mwaka huu katika mji wa Delhi, kwa hakika maonyesho haya yametoa fursa kwa wadau wa utalii India kuvijua vivutio vya utalii vya Tanzania,” alisema Mdachi na kuongeza:

“Lakini pia kutangaza safari mpya za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwa kutumia ndege aina ya 787-8 Dreamliner ambapo Novemba, mwaka huu wanatarajia kuanzisha safari za moja kwa moja kutoka Tanzania kwenda Mumbai, India,” alisema.

Alisema TTB kwa kushirikiana na ATCL wamefanya matangazo maalumu (roadshow) katika miji mashuhuri mitatu nchini India, ambapo kwenye ziara hii ya utangazaji, TTB iliwaalika wakala wa utalii na usafirishaji wa anga 15 kwenda India ili kufanikisha azma hiyo.

Kundi hilo kutoka Tanzania linaongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Alyoce Nzuki, ambapo ujumbe huo unatarajiwa kurudi nchini Septemba 24, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles