19.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 4, 2022

Waziri asimulia taarifa ya Ebola Kigoma ilivyomshtua

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesimulia jinsi alivyopokea kwa mshtuko taarifa kuhusu kuwapo kwa mtu aliyehisiwa kuwa na ugonjwa wa Ebola huko mkoani Kigoma.

Akizungumza Dar es Salaam jana mara baada ya kuhitimisha matembezi ya kwanza ya hisani ya kuelimisha jamii kujikinga dhidi ya ugonjwa huo, Waziri Ummy, alisema taarifa hiyo ilisabababisha augue tumbo ghafla.

“Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma alinipigia akanijulisha kuwa amepatikana mtu anayehisiwa kuwa na maambukizi ya Ebola mkoani humo, niliugua ghafla tumbo la kuharisha. Lakini nashukuru kwamba jioni siku hiyo alinipigia na kuniambia vipimo vilionesha ‘negative’.

“Binafsi naogopa, naomba Mwenyezi Mungu ugonjwa huu usiingie nchini nikiwa Waziri na hata nikiwa si Waziri, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonesha tangu ulipogundulika nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) hadi sasa watu wapatao 111 wamegundulika kuwa na ugonjwa huu, 75 kati yao wamefariki dunia ikiwa ni sawa na asilimia 67,” alisema.

“Hiyo inamaanisha ikiwa itatokea Tanzania kati ya watu 100 watakaougua watu 50 tutawapoteza, ndiyo maana tunaweka nguvu katika kuelimisha jamii kujikinga dhidi ya ugonjwa huu.

“Kwa msingi huo nazidi kuwahamasisha wakuu wa mikoa kuhakikisha wanafuatilia kwa ukaribu na watenge maeneo yatakayotumika kuwatenga wahisiwa,” alisema.

Aliwasihi viongozi wa dini zote nchini kutumia dakika kadhaa katika mahubiri yao kutoa elimu kwa jamii, jinsi ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ebola.

“Leo (jana) tunazindua wimbo maalumu unaotoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huu, nawasihi pia wasanii watunge nyimbo za namna hiyo, licha ya kwamba kweli tunapenda nyimbo za mapenzi na za burudani, aidha, kila mmoja wetu wakiwamo viongozi wenzangu kwa ujumla tutumie vema majukwaa mbalimbali tunayopata kufikisha ujumbe huu.

“Tunakusudia kutengeneza ‘reflector’s’ ambazo tutawapatia madereva wa bodaboda, vitakuwa na ujumbe wa kuelimisha jamii kujikinga,” alisema.

Pamoja na hayo, Waziri Ummy alizindua rasmi Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Ebola nchini.

Awali akizungumza Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammed Kambi, alisema hadi sasa hakuna mtu aliyepatikana kuwa na ugonjwa huo nchini.

Naye Mwakilishi Mkazi wa WHO – Tanzania, Dk. Adiele Onyeze, alisema shirika hilo litaendelea kushirikiana kwa ukaribu na Serikali kudhibiti.

“Kuna timu ya wataalamu wanne wa WHO ambao walikuja kujumuika nasi kuongeza nguvu, lakini pia kule DRC kuna watumishi wapatao 200 wamekwenda kudhibiti usienee,” alisema Dk. Onyeze.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,660FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles