26.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

NITAHAKIKISHA VYOMBO VYA USALAMA VINAWAJIBIKA KUWAPATA WAUAJI

NA ANDREW MSECHU


KATIKA siku zake za mwisho, kabla hajafariki dunia mwaka 2013, aliyewahi kuwa Rais wa Kwanza Mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela aliacha ujumbe, ambao ni nukuu isiyokufa.

AIlikuwa kama akitafakari na kuhitimisha safari yake duniani, kisha kuanza safari yake ya Akhera akieleza kwa ufupi tu kwamba muda wake umekwisha, pamoja na mateso yote aliyopitia enzi za serikali ya kibaguzi, kukaa gerezani kwa miaka 27 kisha kuachiwa, maisha yake hayakuwa bure kwa watu wa Afrika Kusini.

Baada ya kipindi kirefu cha taabu, hatimaye alikuwa ndiye mtu pekee kati ya wote walioshiriki katika harakati dhidi ya serikali ya kibaguzi, aliyepata nafasi ya kuandika historia na kuwa Rais wa Kwanza mzalendo na kuleta ahueni ya kiutawala, kwa ajili ya kumaliza zama za ubaguzi wa rangi

Kwa kauli yake, Mandela alisema, nanukuu: “Mtu anapofanya kile anachokiona kuwa wajibu wake kwa watu wake na nchi yake, mtu huyo anaweza kupumzika kwa amani,” Mwisho wa kunukuu.

Kauli ya Mandela inaweza kuwa na maana katika kipindi hiki ambacho kijana, Ofisa wa Polisi wa Uganda, ambaye katika kipindi chake kifupi cha kuhudumu alionesha tofauti, analazimishwa kupumzika akiwa amefanya mambo tofauti na ilivyozoeleka.

Kwa Mohammed Karumira, kifo chake kinatia simanzi, ila anapumzika salama akiacha deni kwa wananchi wa Uganda, kwa wauaji waliokatiza uhai wake kikatili na kwa nchi jirani pia.

Karumira anakuwa kati ya maofisa wa vyombo vya ulinzi nchini Uganda akiwamo Meja Mohammed Kigundu na aliyekuwa Msemaji wa Jashi la Uganda, Felix Kaweesi waliouawa katika hali kama hiyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita,

Machi mwaka 2017, Kaweesi aliyekuwa msemaji wa jeshi la polisi nchini Uganda aliuawa kwa kupigwa risasi alipokuwa akiendesha gari kwenda nyumbani kwake. Wauaji wake bado hawajapatikana.

Mwezi Juni, Mbunge Ibrahim Abiriga aliuwawa pamoja na mlizi wake karibu na nyumbani kwake nje ya mji wa kampala, hakuna mtu aliyekamatwa kufuatia mauaji hayo.

Kabla ya kuuwawa mwishoni mwa wili iliyopita, Kirumira alisema alikuwa akiishi kwa hofu kwa sababu ya vitisho vya kuuwawa alivyokuwa akipata, lakini kwamba hilo halikumzuia kusema ukweli.

“Tunawafichua waovu ili tuliokoea taifa. Ukizungumza unakufa, ukinyamaza unakufa basi ni bora uzungumze na ufe wakati ujumbe umewafikia watu.

“Basi ujumbe wangu kwa wauaji wanaoshika bunduki ni kwamba, mkiniua ni bure tu. Kwa sababu kama mjumbe nimetekeleza lengo langu la kuwasiliana na jamii,” Kirumira aliwaambia waandishi wa habari Uganda wakati fulani.

Pamoja na kutoa malalamiko ya vitisho dhidi yake na kuwapa ujumbe washika bunduki ambao alijua tayari wanamwinda, kutokana na kuingilia maslahi batili ya wakubwa, hawakumwacha, mwishoni mwa wiki wakamuua kwa bunduki zao, tena wakiamua kumuua na mkewe, ili hata wanawe wakose wa kuwatunza na kuwalea.

Katika baadhi ya kumbukumbu, Kirumira anaonekana akiwa mtu aliyejiamini, akijaribu kupigania wanahabari kutekeleza wajibu wao na hasa katika moja ya video akionekana kupambana na askari wa usalama waliokuwa wakiwazuia kuchukua taarifa za mahakamani kuhusu askari waliokuwa wakituhumiwa mahakamani hapo.

Akiwa askari aliyejiamini, alisema watu wa namna hiyo hawatakiwi kufichwa, kwa kuwa wamekuwa wakishiriki katika makosa ya jinai kwa kutumia vyeo vyao, tofauti na dhamana waliyopewa ya kuhakikisha wanasimamia haki.

Malalamiko ya aina hiyo, ya watu kutishiwa kuuawa kisha kushambuliwa aidha kuuawa au kujeruhiwa yamekuwa yakitokea mara kadhaa, ikiwamo hapa nchini ambapo mwanasiasa wa upinzani, Tundu Lissu aliwahi kulalamika hadharani na hatimaye alishambuliwa akiwa katika eneo lenye ulinzi, hadi leo waliomshambulia hawajapatikana.

Bahati yake nzuri, katika namna ambayo hakuna aliyetarajia alinusurika kufa, baada ya zaidi ya risasi 27 kuingia katika maeneo mbalimbali ya mwili wake na kwa mwaka mmoja sasa anaendelea kupata matibabu nje ya nchi.

Ni kwamba, wauaji hawa wanaopewa jina la wasiojulikana, ambao hawahitaji mali yako wala chochote ulichonacho, ila roho yako, hata kama ukiwaanika hadharani, hawatakuacha, kama ambavyo hawakumwacha Kirumira, hawakumwacha Lissu pia.

Kwa Uganda, ikumbukwe kwamba ni muda mfupi tu, uhalifu wa kutumia silaha uligharimu maisha ya dereva wa Mwanasiasa wa upinzani, Robert Kyagulanyi (Bobbi Wine) katika shambulio lililokuwa limemnuia mwanasiasa huyo ambaye alianza kuonekana kuwa kikwazo kwa Rais Yoweri Museveni.

Wiki tatu zilizopita, Uganda ilikumbwa na maandamano kufuatia kukamatwa na kuteswa wabunge Bobbi Wine na Francis Zaake na vikosi vya Uganda vilijibu kwa kuwapiga risasi watu sita na kuwajeruhi wengine kadhaa.

Katika mazingira ya mashambulio yote ya aina hiyo, hakuna muhusika yeyote wa uhalifu huo aliyewahi kukamatwa, hatua inayoonesha ni uhalifu wa kupangwa, kama sivyo inaonesha vyombo vya usalama vinavyohusika katika kuhakikisha wahalifu wanapatikana ni dhaifu katika kuwapata wahalifu stahiki, ila imara sana katika kukamata na kuadhibu watu wema.

Kweli, nitafanya tofauti iwapo nitakuwa na mamlaka ya juu ya nchi, kuhakikisha kwamba ninasimamia na kuonesha kuwa vyombo vyangu vya usalama vinaonesha uwezo wake kwa kuwanasa wahalifu wa aina hii, ili kuudhihirishia umma kwamba serikali yangu haina mkono wake.

Ninaikumbuka tena nukuu nyingine ya Mandela, iliyosema: “Chuki hufunga akili,inazuia ubunifu wowote wa mbinu, viongozi hawana nafasi ya kuchukia,” mwisho wa kunukuu.

Naiona nukuu hii ikijidhihirisha, hasa kutokana na haya yanayoendelea. Kweli chuki inapowakumba viongozi  huwapotezea uwezo wa kuwa wabunifu.

Yanayoendelea ni dhahiri, kwamba kila anayeonekana kuonesha kukosoa au kurekebisha viongozi hushughukiwa na chuki ya viongozi hao, ambao hutumia nguvu kubwa kuhakikisha wanapoteza uhai wao, ikiwa ni njia pekee wanayoona itawasaidia kubaki salama, hicho ndicho kikomo cha upeo, kutokana na kukosa ubunifu kunakosababishwa na chuki.

Hakika, nitafanya tofauti, sitaruhusu chuki dhidi ya wale wanaotumia haki yao kidemokrasia, kutekeleza majukumu yao katika kunyoosha nchi, nitawapa nafasi, nitahakikisha ninawapa hata nafasi ya kukaa nao pamoja,kujenga urafiki, nipewe heshima niwape heshima.

Katika kumuenzi Mandela, kama kiongozi wa mfano aliyeweka historia na anayeenziwa na watu wake na Afrika, ninakumbuka mwendelezo wa nukuu zake, akisema: “Kama wanaweza kujifunza kuchukua, basi wanaweza kufundishwa kupenda, kwa sababu kwa kawaida ni asili yake upendo kuja kwa moyo wa mwanadamu kuliko kinyume chake,”

Nitafanya tofauti, sitawachukia wapinzani wangu, sitatumia mamlaka niliyonayo kukatiza uhai wao. Sitawadhuru kwa risasi au kwa namna yoyote, bali nitasimama kwa hoja na kuwapinga pia kwa hoja, nikiwa na uhakika kwamba ninafanya kila jema kwa kujiamini na kuweka kando woga.

Tabia hizi za kushambulia na kuwatoa uhai wale wanaoonekana kuwa na fikra chanya dhidi ya Serikali imekuwa mtindo ulioanza kuzoeleka sasa katika nchi za Afrika Mashariki, Nitafanya tofauti na kuwakosoa kina Trump ambao waliwahi kupata hata jeuri ya kuzitukana nchi za Afrika kwa kusema nchi zote katika bara hili ni ‘shit hole’.

Wakati wa maadhimisho ya miaka 100 ya Nelson Mandela Julai mwaka huu, katika hotuba yake ya kwanza tangu aondoke madarakani, Rais aliyepita wa Marekani, Barack Obama alieleza kuhusu alichokiita ‘Siasa za umimi’ zinavyoshika kasi katika nchi za Afrika.

Alieleza kuhusu namna wanasiasa wanaoingia madarakani wanavyojikuta wakiingia katika mkumbo wa kujenga ‘siasa za chuki, woga na vitisho’ kwa wale wanaoitwa wapinzani wao ili kujihakikishia uhakika wa kutawala watakavyo kwa kudhibiti taasisi zote katika mfumo wa demokrasia ambao inaonekana wengi hawauwezi, hasa katika miaka ya hivi karibuni.

Sijawahi kufikiria kuwa mwanasiasa, ila ninaona ipi njia ya kufanya tofauti, nitafanya tofauti kwa kufuta siasa za woga na kujenga mfumo utakaoruhusu uwajibikaji kwa viongozi, kuhakikisha demokrasia inatamalaki na sheria za nchi zinaheshimiwa.

Nitafanya tofauti, kwa kuhakikisha kwamba hata wale wanaozungumza ubaya kwa Afrika hawapati nafasi ya kunihusisha katika ujumla wao, kwa kuwa nitakuwa katika nafasi nzuri ya kuwaonesha kwamba hata wao wanakosea pale wanapotaja kwa ujumla, kwa kuwa mimi si samaki katika kapu la hao waliochina.

Pamoja na majukumu mengine, nitafanya tofauti kuhakikisha kwamba kila anayehusika katika mauaji ya kisiasa, awe kutoka katika vyombo vyangu vya usalama au mhalifu kutoka makundi ya wahalifu ambao si majambazi, wasio na nia ya kuiba mali wala kujeruhi bali kuua na kuondoka wanapatikana na kushughulikiwa kikamilifu na vyombo vya sheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles