BOBI WINE NI MWANZO, MWISHO WA RAIS MUSEVENI?

0
935

 JOSEPH HIZA NA MITANDAO


KWA upande mmoja kuna Bobi Wine, Mwanamuziki maarufu mwenye bashasha anayefahamika sana nchini Uganda kama ‘Rais wa Gheto’ na upande mwingine kuna Rais halisi wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni.

Kama ilivyo kwa wanamapinduzi wengine wengi wa zamani barani Afrika, mwana wa Kaguta ameng’ang’ania madaraka kwa miongo kadhaa katikati ya miluzi inayozidi kukua ikimtaka ajiuzulu.

Museveni (73) amelitawala taifa hilo la Afrika Mashariki kwa mkono wa chuma tangu aingie madarakani mwaka 1986, akifahamika kwa kukosa uvumilivu dhidi ya wapinzani wake hasa wale wanaoonekana kutishia utawala wake wa miaka 32.

Kwa sababu hiyo, akitumia mbinu zake za kikomando zilizomwingiza madarakani, amewakatili wapinzani wake wengi ndani na nje ya chama chake tawala cha National Resistance Movement (NRM) ikiwamo kuwapoteza kabisa katika ramani ya kisiasa.

Lakini baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema Wine na kipaji chake cha muziki na siasa pamoja na kubebwa na wingi wa ujana wake unaomfanya anene kwa lugha ya kundi kubwa kabisa la wapiga kura nchini humo-vijana, ni tisho kubwa kwa kiti cha Museveni.

Kipindi cha wiki chache zilizopita, Uganda iliingia katika kiwingu cha mashaka na machafuko yaliyotokana na kukamatwa kwa Mbunge huyo wa upinzani, ambaye jinale halisi ni Robert Kyagulanyi.

Kukamatwa kwa Mwanamuziki huyo nyota wa miondoko ya Pop wa mapigo ya Afro, sambamba na wabunge wengine wanaoipinga serikali kulisababisha maandamano yaliyoambatana na vurugu katika Mji Mkuu wa Kampala na kwingineko nchini humo.

Machafuko ya karibuni yalianza katikati ya Agosti wakati Rais Yoweri Museveni, Bobi Wine na wabunge wengine wa upinzani walipokuwa wakiparurana katika mji wa Kaskazini Magharibi wa Arua katika kampeni ya uchaguzi mdogo.

Baada ya saa kadhaa kali zenye mikwaruzo na matusi kutoka pande zote, msafara wa rais ukashambuliwa kwa mawe wakati ukiondoka mjini humo.

Watuhumiwa wa kitendo hicho ni wafuasi wa Bobi Wine. Rais Museveni aliweza kuifikia helikopta yake pasipo kuumia. Lakini walinzi wake wakarudi tena Arua kwenda kutembeza mkong’oto kwa kila kiumbe walichokikuta katika umati uliokusanyika hapo.

Ni katikati ya vurumai hizo, Bobi Wine, wabunge watano wa upinzani, waandishi wawili wa habari na watu wengine 28 walikamatwa. Dereva wa Bobi Wine, – Yasiin Kawuma – alipigwa risasi na kufa. Siku zilizofuata, viongozi wengine wa upinzani pia walikamatwa.

Mara kukaja taharuki nchini humo baada ya kuibuka taarifa za kukamatwa kwa Bob, ambaye alikuwa na umri wa miaka minne wakati Museveni anaingia madarakani mwaka 1986.

Taarifa hizo na za kifo cha Kawuma, zikawafanya vijana kundi ‘lisilomjua’ Museveni kuja juu, maandamano ya mitaani yakaripuka jijini Kampala.

Maandamano na machafuko hayo awali yalijikita katika kitongoji maskini cha Kamwokya, iliko studio ya muziki ya Bobi Wine na Kyadondo Mashariki, ambalo ni jimbo analoliongoza kama Mbunge, lakini zikaja sambaa kwa kasi katika maeneo mengine.

Hali ilikuwa mbaya zaidi wakati ilipobainika kuwa Bobi Wine na wabunge wengine waliokamatwa waliteswa wakiwa mikononi mwa polisi. Wakati mwishowe alipoonekana mahakamani siku 10 baadaye alikuwa akipata shida kutembea.

Ongezeko la maandamano ya upinzani liliitikiwa vikali na vikosi vya usalama. Machafuko yakasababisha makumi ya watu kulazwa hospitali na wawili kufa. Waandishi waliokuwa wakiandika suala hilo wakitishiwa maisha.

Kukamatwa na vitisho dhidi ya viongozi wa upinzani si jambo jipya katika Uganda ya Rais Museveni. Hata hivyo, kasi na ukali wa vikosi vya usalama ilikuwa ya kushtusha mno. Mwitikio wao wa awali ulikuwa mbaya sana!.

Lakini kusambaa kwa machafuko katika miji mingi na kesi ya uhaini dhidi ya Bobi Wine kunaashiria kuna zaidi katika simulizi hizi katika mawazo ya watawala.

Na Bobi Wine ameachiwa kwa dhamana na sasa ameruhusiwa kutibiwa nchini Marekani. Lakini changamoto na matatizo kwa Museveni ndiyo yameanza.

Anazidi kukomaliwa na kizazi cha wapiga kura vijana chenye hasira naye huku mfumo wa kisiasa wa chama chake cha NRM ukichuja na kuzidi kukua kwa umaarufu na umuhimu wa mitandao ya jamii katika siasa za Uganda iliyomkalia vibaya.

Na haikushangaza suala la Serikali kuitoza kodi mitandao ya jamii ikiwamo ule wa whatsap ulivyoteka vichwa vya habari si tu nchini humo bali pia duniani kote.

Katika miongo miwili ya kwanza ya utawala wake, NRM kwa mafanikio iliendesha nchi kama chama kimoja cha siasa chini ya ‘mfumo wa vuguvugu’ ambapo wagombea wote walilazimishwa kuwania nyadhifa kama mtu binafsi badala ya kuwa wanachama wa vyama vya kitaifa vya siasa.

Zama hizo bado zipo.  Utamaduni wa mgombea binafsi katika siasa umeendelea tangu NRM kiwe rasmi chama cha siasa mwaka 2005. Wapiga kura wake muhimu ni wale wa vijijini ambao hujishughulisha na siasa za maeneo yao tu. Pia hao wana umri wa kutosha kukumbuka vita za kuogofya kabla ya ujio wa ‘mkombozi’ wao, Museveni.

Kwa wapiga kura hawa, kumuondoa rais madarakani ni wazo lisilokubalika wakiliona hatarishi na kushtusha. Utafiti uliofanyika Kusini mwa Uganda wakati wa uchaguzi wa urais mwaka 2016 umethibitisha hilo.

Ulionesha kwamba wengi wa wapiga kura wa Museveni hawawezi kirahisi kushinikizwa au kununuliwa na hawataki kusikia dhana ya kumuondoa madarakani mkombozi wao huyo!.

Kuna sababu kidogo ya kufikiri kuwa mfumo wa zamani unaanguka, bali tatizo ni kwa namba zinazomuung mkono Museveni wakiwamo wanaonufaika nao kuzidi kupungua kwa kadiri umri unavyokwenda na vizazi vipya kuzaliwa.

Hili kundi la wapiga kura vijana. Halina kumbukumbu ya vita za nyuma, lina elimu nzuri ambayo inayowaongoza kutaka zaidi ya kile kizazi cha wazazi wao walioishi maisha ya kilimo na hujihusisha zaidi katika siasa za kitaifa kuliko za nyumbani wanakotoka.

Na ndio maana Museveni katika hotuba zake nyingi ikiwamo ya karibuni kwa taifa alieleza hivi na vile katika mkoa huu na ule namna alivyopigana vita ya ‘kuikomboa’ Uganda katika kile kinachoonekana kuwasihi Waganda wakumbuke alikowatoa.

Lakini vijana nchini humo hawana ‘dili’ na dhana ya kubadili mbunge wa eneo lao, bali wanataka rais mpya.

Ni kundi la wapiga kura, ambalo kamwe halijawahi kuwa jimbo muhimu kwa Museveni ingawa kuna kipindi alimtumia mtoto wake Muhoozi Kainerubaga ‘kuwatongoza’ vijana wampigie kura, mvuto ambao ulikuwa wa muda mfupi mno na ukiishia kwa wafuasi na makada vijana wa chama hicho.

Muhoozi (44), aliyepandishwa ngazi haraka mno kufikia sasa ngazi ya Meja Jenerali, anadaiwa kuandaliwa na babake huyo kumrithi na hilo limekuwa chanzo cha uasi wa mara kadhaa wa mofisa wa ngazi ya juu jeshini.

Ukiondoa hayo, tisho la vijana kisiasa nchini humo, awali lilipuuzwa wakionwa kuwa kundi dhaifu na lililojikita katika maeneo machache ya mijini.

Lakini kwa sasa wamesambaa kote nchini humo ikiwamo katika miji ya eneo la vijijini anakotoka Museveni. Kuongezeka kwa nguvu ya mitandao ya jamii kunafanya iwe rahisi kwao kuunganisha mtandao na kuwasiliana kirahisi.

Zaidi ya hayo, idadi yao inazidi kuongezeka kwa kasi. Uganda ni miongoni mwa mataifa yenye idadi kubwa ya watu wenye umri mdogo duniani. Asilimia 48 ya watu wote nchini humo wana umri wa miaka 14 huku moja ya tano (asilimia 21.16) ya watu wote wakiwa na umri kati ya miaka 15 na 24. Asilimia mbili tu ya watu wote ni wenye umri wa miaka 65 au zaidi.

Kwa sababu hiyo, Bobi Wine (36-) si tishio kwa sababu anasema kitu ambacho hakuna kiongozi wa upinzani aliyekizungumza bali kwa vile ni mahiri, ana uwezo wa kujipanga katika kuliteka kundi hili muhimu la wapiga kura lenye damu kama yake.

Museveni hupenda kuwajengea picha wapinzani wake kama watu wagawanyishi, wakabila au vijana wa kihuni na mengineyo mabaya kama hayo.

Lakini Bobi Wine huwezi kuwaaminisha watu kuwa ana sifa kama hizo kama ilivyojionesha katika barua zake nyingi kwa umma akimchamba Museveni baada ya kuchaguliwa kwake mwaka 2017 kuingia bungeni.

Naam, Wine, amejijengea jukwaa lake lenyewe la vijana kuliko tabaka, ukanda au udini unaotumika kama silaha kwa wanasiasa muflisi!.

Na mbaya zaidi kwa Museveni na hata kupunguza umaarufu wa rafikiye aliyegeuka mpinzani mkuu, Kiiza Besigye. Mlolongo wa chaguzi ndogo za karibuni nchini humo ikiwamo Arua umedhihirisha nguvu za Bob Wine dhidi ya wanasiasa hao wawili. Ni maumivu zaidi kwa Museveni!.

Haikushangaza kuwa Bobi Wine alijikuta akikwaruzana na mikono ya sheria wakati wa maandamano ya mjini kampala akipinga sheria mpya ya kodi yenye utata ya mitandao ya jamii, ambapo mamlaka zilimtuhumu kuchochea uasi.

Na kipindi kuelekea uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arua, mitandao ya Facebook, Instagram, Twitter, YouTube na WhatsApp yote ilishuhudia ‘posti’ zilizoashiria Bobi Wine ni nani, sambamba na kukua kwa wafuasi wake kote nchini humo.

Sasa ari hiyo ya vijana kumtangaza ‘rais’ wao huyo imevuka mipaka ya taifa hilo hadi jirani Kenya, ambako wabunge vijana waliandamana kushinikiza Bobi achiwe huku Waganda waishio ugenini, yaani Diaspora wakikusanyika kupiga kelele katika balozi zao katika miji ya Berlin nchini Ujerumani, London nchini Uingereza, Washington DC nchini Marekani na kwingineko.

Ilikuwa rahisi huku nyuma kwa Museveni kutuhumu upinzani kwa ukanda na ukabila, lakini hilo linaonekana kutoweka. Taswira ya kisiasa ya Ugandan inaonekana kubadilika.

Kwa sababu hiyo Bobi Wine ni tisho la kweli kwa Museveni ambalo halijawahi kuonekana kwa miaka mingi kutokana na kuwakilisha kizazi kinachochukua sehemu kubwa ya Waganda cha vijana, ambao wengi hawana ajira na wanajiandikisha kupiga kura.

Ni kundi ambalo limechoshwa na utawala mkongwe, ambalo wanahitaji mtu mwenye uwezo wa kumwondoa madarakani na Bobi Wine ingawa hakuwahi kufikiriwa kuwania urais, anaonekana kuwa tumaini la vijana.

Lakini Wine huwa mwepesi kukataa dhana kwamba yeye ni masiha aliyeshushwa kuja kuupindua utawala wa muda mrefu wa Museveni.

Kama alivyosema hivi karibuni kupitia akaunti yake ya Twitter: “Nimeshawahi sema kabla kuwa chama chochote kinachokuambia kinaweza kuikomboa Uganda pekee ni utani!. Kwetu kumshinda Rais Museveni, itatuhitaji chama zaidi ya kimoja cha siasa, zaidi ya kabila moja, zaidi ya dini moja na ndiyo zaidi ya kizazi kimoja.”

Kabla hajawa Bobi Wine, Robert Kyagulanyi alikulia katika vitongoji maskini vya Uganda, akilelewa na mama pekee lakini akageukia muziki kama njia ya kuondokana na umaskini.

Staili ya midundo ya muziki wake na mashairi ya kugusa na kuchoma ilitawala anga za muziki na vilabuni kote Afrika Mashariki kuanzia mapema miaka ya 2000.

Akiimba mara kwa mara kwa lugha yake ya Luganda, nyimbo zake zilikuwa na ujumbe mzito mara nyingi zikijiegemeza zaidi namna jamii inavyokandamizwa nchini humo.

Alitoa mwito kwa raia kuinuka na kupaza sauti zao kupambana na ukandamizaji

“Msionee aibu kuifanyia kazi Uganda, kwa sababu ni nchi yenu wenyewe, hata kama bosi wako si chaguo lako. Tumia nafasi yako kwa sababu hii ni nchi yako, aliimba katika moja ya vigongo vyake, “Situka.”

Mwaa 2017, aliwania ubunge kama mgombea binafsi akiendesha kampeni iliyobebwa na ujumbe: “Kwa sababu Bunge limeshindwa kuja ghetoni, basi lazima tulete ghetto bungeni.”

Alichaguliwa kwa kishindo na tangu hapo akathibitisha kuwa mwiba kwa Museveni akiendesha mapambano kwa kushirikiana na wabunge wa upinzani na kuendelea na muziki hasa uliolenga kuushambulia utawala wa muda mrefu madarakani.

Umarufu  wake haukujificha kiasi cha serikali kuushuhudia ndiyo mana baadhi ya nyimbo zake ikiwamo ya ‘Freedom’ zimepigwa marufuku nchini humo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here