26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ATETA NA MAASKOFU

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam


RAIS Dk. John Magufuli, amewataka maaskofu kufanya kazi kwa kujiamini na kwa uhuru wakati wote.

Alitoa kauli hiyo, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais Magufuli aliwahakikishia viongozi hao yuko pamoja nao na wakiwa na jambo lolote wamjulishe atalishughulikia.

“Nawahakikishia mimi nipo pamoja na nyinyi, nendeni mkafanye kazi kwa kujiamini na kwa uhuru, mkiwa na jambo lolote nijulisheni nitalishughulikia, wahubirieni Watanzania amani, upendo, mshikamano na kuipenda nchi yao,” ilisema taarifa hiyo.

Rais Magufuli, alishukuru kukutana na viongozi hao na kufanya nao mazungumzo, huku akiwahakikishia kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa madhehebu ya dini na taasisi zake.

“Serikali itaendelea kushirikiana nanyi kuwahudumia na kuwaletea maendeleo wananchi, kupitia taasisi kama zenu,” ilisema taarifa hiyo.

Pia aliahidi kufanyia kazi changamoto ambazo madhehebu ya dini yanakutana nazo, huku akiwaomba viongozi hao kuendelea kuliombea taifa kudumisha amani, upendo na mshikamano.

Viongozi wa CCT waliokutana na Rais Magufuli ni Mwenyekiti Askofu Anilikisa Cheyo, Makamu wa Kwanza wa Mwenyekiti, Askofu Fredrick Shoo, Makamu wa Pili wa Mwenyekiti, Askofu Jacob Chimeledya na Katibu Mkuu, Mchungaji Moses Matonya.

Kwa upande wa viongozi wa TEC, ni Rais Askofu Gervas Nyaisonga, Makamu wa Rais, Askofu Flavian Kasalla na Katibu Mkuu, Padre Charles Kitima.

Viongozi hao, wamemshukuru Rais Magufuli kwa kukubali ombi lao la kukutana naye kwa lengo la kujitambulisha na kufanya nae mazungumzo kuhusu uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya makanisa wanayoyaongoza na Serikali.

Walimhakikishia utayari wao wa kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Serikali, kuyasimamia makanisa yao ili yaendelee kutoa huduma ya kiroho na kijamii kwa manufaa ya Watanzania wote na kufanyia kazi changamoto mbalimbali zinazojitokeza.

Viongozi hao, walimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yake katika kuleta maendeleo na kuimarisha huduma za kijamii, ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya usafiri na majengo, kuleta nidhamu katika utumishi wa umma, mapambano dhidi ya rushwa, kuimarisha usimamizi wa rasilimali za taifa, hasa madini, kupambana na wizi na ufisadi wa mali za umma, kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo, kuimarisha huduma za afya na kuwapigania wakulima.

Wamewaomba Watanzania wote kumpa ushirikiano wa kila aina kwa kuwa wanatambua na wameona kazi nzuri ambayo anafanya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles