Mwandishi Wetu, Nkasi     |  Â
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amekataa kuzindua huduma ya umeme katika Kata ya Kirando na Kata ya Kate wilayani Nkasi mkoa wa Rukwa baada ya Mkandarasi kusuasua kuunganishia umeme kwa wananchi.
Tukio hilo oimetokea leo baada ya Naibu Waziri huyo kufika katika Kata hizo na kukagua miundombinu ya umeme ambapo pamoja na mambo mengine alielezwa kuwa katika Kata ya Kirando ni wananchi wanne tu ndiyo wameunganishiwa umeme na katika Kata ya Kate, wananchi wawili tu wameunganishwa.
Kutokana na hali hiyo, Mgalu ameeleza kusikitishwa kwake na kasi ndogo ya mkandarasi huyo ambaye ni Kampuni ya Nakuroi aliyepewa kazi ya kusambaza umeme katika Vijiji 111 vya Mkoa wa Rukwa hadi kufikia Juni 2019 ambapo hadi sasa ameunganisha umeme katika vijiji saba tu.
“Tangu mpewe kazi hii mwaka jana, hadi sasa ni vijiji saba tu mmewasha umeme, hili suala halikubaliki, na nitakaporudi Dodoma Mkurugenzi wa Kampuni hii na Menejimenti yake wafike wizarani kutoa maelezo,” amesema Naibu Waziri Mgalu.
Amesema pamoja na Serikali kuanza kutoa fedha kwa wakandarasi wa umeme, baadhi ya wakandarasi bado wanasuasua kutekeleza kazi hiyo kwa visingizio vya kutokuwa na vifaa.
Pamoja na mambo mengine, ametoa onyo kama kuna mtandao wa watu wanaojipanga ili kukwamisha juhudi za Serikali za kusambaza umeme Vijijini, Serikali itawabaini na watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Awali, Mbuge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy na Mbunge wa Nkasi Kusini, Desderius Mipata nao walitoa malalamiko kwa Naibu Waziri kuhusu kampuni ya Nakuroi kuwa na kasi ndogo katika kuwasambazia umeme wananchi.