NINI kitatokea baada ya kukamilika kwa kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuwasaidia kinamama ambao walitelekezewa watoto na wanaume waliowazalisha? Unaweza kuhisi kuwa kati ya wanawake hao, wapo ambao watakuwa wamepata nafuu baada ya wanaume kukubali kuendelea kutoa huduma kwa watoto wao lakini pia wapo ambao bado watakuwa na kesi mahakamani kuhusiana na uhalali wa wanaume wanaotajwa kuwa ndio baba wa watoto.
Lakini, wale watumishi wa Idara ya Ustawi wa Jamii na wanasheria, ambao Makonda aliwatumia katika kampeni hiyo, watakuwa wamerejea kwenye ofisi zao kuendelea na kazi kama kawaida. Kuna uwezekano kuwa huko watakutana na mlundikano wa mafaili ambayo wanapaswa kuyashughulikia. Mrundikano huo utatokana na kazi ambazo hazikufanyika katika kipindi ambacho hawakuwapo ofisini wakati wanashughulika na kampeni ya Mkuu wa Mkoa.
Wakati watumishi hawa wakihangaika na mafaili hayo, Makonda mwenyewe anaweza kuwa ameshaanza mkakati wake wa kupita nyumba kwa nyumba kuwapima tezi dume wanaume wa Dar es Salaam.
Operesheni ya kuwasaidia kinamama waliotelekezwa na wanaume waliowapa ujauzito ni moja ya mambo kadhaa ambayo Makonda ameyaanzisha akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Mambo yote aliyoyaanzisha ni mazuri kwa sababu yanalenga kupata ufumbuzi wa matatizo ambayo, baadhi yake, yamekuwa sugu.
Tofauti na wakuu wengi wa mikoa, Makonda amekuwa akibuni mikakati mbalimbali ya kukabiliana na matatizo ambayo anayaona kuwa ni kikwazo cha maendeleo katika mkoa wake. Anastahili pongezi kwa ubunifu huo.
Lakini, tangu ameanza utaratibu huo, mafanikio yanayoonekana kutokana na operesheni zake ni madogo ukilinganisha na juhudi na nguvu zinazotumika kukabiliana na matatizo hayo. Kibaya zaidi ni kuwa mikakati inalenga kutatua tatizo kwa wakati huo tu na mkakati unapokamilika hauachi mfumo endelevu wa kukabiliana na matatizo hayo.
Makonda amekuwa akitumia nguvu kubwa sana lakini anapata matokeo finyu kwa sababu hakuna suluhisho linalozaa mfumo endelevu wa kukabiliana na matatizo hayo.
Kinachofanywa na Makonda kitazaa faida pana iwapo utaratibu wa kukabiliana na matatizo hayo unabadilishwa kidogo na kulenga kukabiliana na mzizi wa tatizo na si matokeo ya tatizo. Pia, opereshani hizo zitaonesha matokeo mazuri iwapo zitalenga kuiwezesha mifumo kuwa na uwezo endelevu wa kukabiliana na matatizo hayo.
Mathalani, katika suala hili la wanawake waliotelekezwa, mkakati ungejikita kuimarisha Idara ya Ustawi wa Jamii na kitengo cha Sheria ili viweze kuhakikisha kuwa vinawasaidia kinamama hawa wakati wote. Kwa jinsi ambavyo kampeni imefanyika, upo uwezekano idadi ya kinamama wanaotelekezwa na wanaume ikaendelea kukua kwa sababu idara inayoshughulikia matatizo yao haijawezeshwa kiasi cha kutosha kukabiliana na matatizo hayo.
Siku zote Idara ya Ustawi wa Jamii imekuwa ikishughulika na matatizo ya kinamama hawa waliotelekezwa na wanaume. Lakini idadi kubwa ya kinamama waliojitokeza kwa Makonda ni ishara tosha kuwa idara hiyo haina uwezo wa kukabiliana na wingi wa matatizo hayo. Matokeo yake matatizo mengi yamebaki bila kupatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu na ndio maana wengi wameiona kampeni ya Mkuu wa Mkoa kama mkombozi wao.
Ni dhahiri kuwa kwa sababu kampeni haikuhusisha kuimarisha uwezo wa watumishi katika Idara ya Ustawi wa Jamii, idadi ya wanawake wanaotelekezwa itaanza kuongezeka na itaanza kuongezeka katika kipindi hiki ambacho watumishi hao wanahangaika kukabiliana na mlundikano wa mafaili waliyoyakuta maofisini mwao. Sidhani kama ushiriki wao katika kampeni hiyo umewapa watumishi hawa wa Idara ya Ustawi wa Jamii maarifa, nguvu na uwezo wa kukabiliana na matatizo hayo kwa ufanisi unaoweza kuwafanya waweze kukabiliana na tatizo hilo kwa ukubwa wake.