Na BENJAMIN MASESE
MKUU wa Wilaya ya Magu, Khadija Nyembo amezuia waandishi wasimrekodi wakati akiomba radhi mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula.
Ilikuwa ni baada ya taarifa iliyoandaliwa na maofisa ardhi wa wilaya hiyo kutupiliwa mbali ikidaiwa kutokuwa na uhalisia na takwimu za utekelezaji wa maagizo ya Serikali.
Tukio hilo lilitokea wakati wa ziara ya Naibu Waziri Mabula wilayani humo kukagua utekelezaji wa maagizo ya serikali ya kupima ardhi, kurasimsiha makazi, kukagua mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya ardhi sambamba kujua mpango mkakati wa matumizi bora ya ardhi ya jiji na kata.
Akiwa katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Mabula alisomewa taarifa ya idara ya ardhi na Mkuu wa Idara hiyo, Wilfred Mkono.
Taarifa hiyo, pamoja na mambo mengine, ilikuwa na upungufu mkubwa kiasi kwamba waziri alikataa kuipokea na kuitupilia mbaya na kuwapa saa kadhaa aandaliwe nyingine.
Mabula alipojaribu kuwahoji baadhi ya maofisa ardhi juu ya utekelezaji wa maagizo ya Serikali, walionekana kutokuwa na majibu ya msingi ingawa idara haina upungufu wa watumishi wala changamoto ambazo zinawazuia kutotekeleza majukumu yao.
Kwa sababu hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Nyembo, alilazimika kumuomba radhi waziri Mabula huku akimzuia mwandishi wa Televisheni ya Clouds, Hamza Makuza, kumrekodi.
“Mheshimiwa Naibu waziri, nipende kuchukua fursa hii… aaaha na wewe mwandishi wa Clouds zima kamera yako, zima sitaki kuonekana kwenye televisheni,”alisema.
Baada ya zuio lake kufanikiwa alisema: “Kama navyojua mimi nakaimu wilaya mbili kwa sasa ya Ilemela kule kwako na hapa Magu, isitoshe jana wote tulikuwa huko.
“Naomba nikuhakikishie makosa yaliyojitokeza na maelekezo yako nitasimamia ipasavyo na utapata taarifa nzuri, kama ulivyoelekeza ukitoka Ukerewe utaipitia”.
Awali, Mabula ambaye alizungumza kwa hasira alisema alisikitishwa na taarifa hiyo kutokuwa na mpango wa mkakati wa matumizi bora ya ardhi, haikuonyesha kuwapo upimaji na urasimishaji makazi.
Mabula alisema taarifa hiyo haikuwa na takwimu za jumla ya viwanja vilivyopimwa katika vijiji, idadi ya vijiji vilivyo katika mpango wa matumizi bora ya ardhi.