Na Shermarx Ngahemera
TOLEO hili kwa makusudi  kabiasa tumeweka dhamira kuandika habari za kilimo na majaribu wanayoyapata wakulima wa Tanzania.
Miaka nenda rudi hakuna cha maana kwa wavujajasho hawa ambao ni asilimia 65 ya wananchi katika shughuli mbalimbali zikiwamo kilimo, ufugaji na uvuvi.
Kilimo ni lawama tu zimezagaa na kama kuna ahueni ni kidogo na ya muda mfupi, na hivyo kukatisha tamaa wengi kujihusisha na shughuli hizo.
Â
Historia
Kihistoria Saba Saba mwanzoni ndio ilikuwa sikukuu ya kuanzishwa kwa Chama Tawala cha TANU, Julai 7 mwaka 1954. Iliendelea hadi mwaka 1992 iliporudishwa demokrasia ya vyama vingi na kubadilika kuwa Sikukuu ya Wakulima, Agosti 8, ambayo awali ilikuwa sikukuu kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa pekee.
Mwaka 1993, Julai 7Â ikatangazwa kuwa si sikukuu tena kwa mwaka huo ila mwaka uliofuata ikarudishwa kama sikukuu ya kitaifa kwani uhuru hauna chama.
Sikukuu hii ya Nane Nane kimsingi huadhimishwa ili kutoa heshima na tafakuri kwa wakulima wa Tanzania ambao huzalisha Pato la Taifa kwa asilimia 30.
Isitoshe ingawa ni Siku ya Wakulima, lakini kinachoonyeshwa ni mazao ya kiwandani na si ya shambani. Mambo yamekwenda kinyume, lakini ni maendeleo vilevile kwa uchumi wa nchi.
Wakulima wanadai Serikali imewasahau ila kwa kuwavisha vilemba vya ukoka na kuwaona hawana maana kwani matatizo yao yamekuwa sugu na hakuna anayeshugulikia kwa undani na kwa huba. Bidhaa zao hazina soko na kama lipo wanalipwa bei ya chini wakati pembejeo wanauziwa kwa bei juu sana.
Misemo isiyotekelezwa
Tunasema kwa majigambo siasa ni kilimo, kilimo uti wa mgongo, mapinduzi ya kijani na kilimo kwanza! Basi imekwisha; kama njozi na umande wa asubuhi au mwezi ukifika muda wake unapotea bila taarifa.
Tuache porojo na tufanye kazi imeenda mbali zaidi hadi kwa wataalamu wenyewe wa kilimo. Lakini historia inaonesha wazi kuwa wasomi wa kilimo hawawezi kubadili kilimo ila mafundi mchundo wa taaluma hiyo ambao walifanya kazi vizuri hadi kilipoanzishwa Chuo Kikuu Cha Sokoine (SUA) ndipo ukulima wa kilimo ukafa na ukabakia ukulima wa kitabu, wa kisomi na kuishia hukohuko. Wasomi wa kilimo wabadilike ili kuleta tija katika sekta na fani hiyo.
Â
Matatizo ya kilimo
Zamani kulikuwa na vyama vya ushirika ambavyo vilikuwa vyenye sauti kwa kila zao la maana nchini. Ilipogundulika kuwa ni kosa kubwa limefanyika baada ya miaka 10 ikabakia historia tu na sio vyama. Vilibanwa na mali yake kuporwa na wajanja ambao hadi kesho hawajafanywa lolote. Moyo wa ushirika uliokuwapo awali ulikufa na kubakia na umimi uliokithiri.
Wakulima hawana uhakika wa kupata pembejeo na madawa ya viuatilifu kwa mazao yao; ama kuchelewa kupata mbolea na madawa au kuyapata mapema, lakini ni feki na hivyo kuleta hujuma kwa mkulima ambaye amelipia kwa jasho lake na fedha taslimu.
Huduma ya fedha kwa wakulima haipo. Benki zinasema wakulima hawakopesheki kwani hawana mali ya kuweka dhamana, kwamba hata ardhi wanayolima hawaimiliki kisheria na hivyo kukopesha ni sawa na kutapanya mali.
Benki chache za hapa nyumbani ndio hukopesha wakulima, zile za nje huwanyanyapaa na hivyo kukwepa mahusiano nao yoyote hata kufungua akaunti tu. Pongezi benki za NMB, NBC, CRDB, TPB na Azania ambazo kwa kiasi chao hukopesha tabaka hili la wavujajasho.
Wakulima wanauziwa mbegu zisizoota na zinazotengenezwa  hivyo makusudi kutoka nchi jirani kwani wao wana ‘franchise’ ya mbegu hizo. Kama nchi tumepoteza umiliki wa mbegu zetu na hakimiliki  wanayo Du Pont, Mosanto na Sygenta zote za Marekani na Uingereza.
Mbegu zetu asilia wamechukua bure, lakini sasa wanadai tulipe wakati mbegu zao za maabara zimeonekana hazifai na si nzuri kwa ladha. Kinachosikitisha ni kuwa mbegu hizo huwezi kuweka akiba kwa matumizi ya baadae ila kila mwaka lazima uende dukani kuzinunua. Hii ni dhambi na dhuluma kubwa tuliyofanyiwa.
Ajabu, hakuna wizara iliyojaa wasomi wa shahada ya uzamili (PhD) kama Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, lakini shehena hiyo ya vyeti haina masilahi kwa taifa hili kwani wamekosa hata kupiga kelele au kutoa taarifa ya hadhari kwa wananchi wetu. Mwalimu Nyerere aliwajali na kuwasomesha ughaibuni kwa gharama kubwa, lakini faida yake hatuioni zaidi ya kutuletea GMOs.
Â
Lakuvunda halina ubani Â
Nchi nyingine zinataka kutusaidia tuondokane na shida hizo kwa kuanzisha na kushiriki miradi mbalimbali ya kilimo chetu. Kati ya yote mradi wa SNV ndio bora kuliko.
Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV), lina zaidi ya miaka 40 tangu ililipoanza kufanya kazi nchini likishirikiana na Serikali na wadau wengine wa maendeleo. Kwangu mimi walichofanya nchini Serikali inabidi iige kwani ni kitu kamilifu, husishi na chenye dhamira ya kweli ya kumjali na kumwinua mkulima.
Shirika hilo linalenga katika kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta tatu ambazo ni kilimo, nishati rejeshi na maji, kupitia wataalamu waliopo kwenye sekta hizo.
Limesaidia upatikanaji wa chakula cha uhakika kwani linafanya kazi katika mikoa 16 kati ya mikoa 25 nchini.
SNV inatekeleza miradi ambayo inalenga katika kuongeza uzalishaji, kipato, ajira kwa wakulima wadogo, kwa kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma ya fedha na masoko.