30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

OFISI YA MSAJILI YAFICHUA KIINI CHA KUTOKWISHA MGOGORO CUF

Waandishi wetu

 

Wabunge waliofukuzwa wakwaa kisiki cha kwanza, wafuasi wazichapa mahakamani

MSAJILI Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, amesema mgogoro unaoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), umeshindwa kutatuliwa kutokana na upande mmoja kutohudhuria vikao vya usuluhishi.

Nyahoza alisema hayo jana, mara baada ya gazeti hili kutaka kujua juhudi za ofisi hiyo katika kutatua mgogoro huo.

Akijibu swali hilo, alisema mara kadhaa wamekuwa wakiziita pande mbili zinazosuguana ndani ya chama hicho, lakini ni upande wa Profesa Ibrahim Lipumba pekee ndio umekuwa ukifika, huku ule wa Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, ukishindwa kufika.

“Mara nyingi tumekuwa tukiziomba pande hizo mbili kufika ofisini hapa ili kusikiliza maelezo yao na kutafuta suluhu, lakini unakuta ni Lipumba tu ndio anafika, Maalim haji. Sasa hapo utapata suluhu gani? Tumeshindwa kupata suluhu kwa kusikiliza upande mmoja,” alisema Nyahoza.

Alisema pia kuwa, Ofisi ya Msajili inamtambua Maalim Seif kama Katibu Mkuu wa CUF na kwamba Magdalena Sakaya kwa sasa amekaimisha nafasi hiyo baada ya uongozi kudai kuwa Katibu Mkuu hafiki ofisini kutekeleza majukumu ya chama.

Kiini cha mgogoro wa CUF ni Profesa Lipumba kutangaza kutengua barua yake ya kujiuzulu nafasi ya uenyekiti aliyoiandika Agosti 2015, wakati wa kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.

Lipumba alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kutokubaliana na uamuzi wa vyama washirika wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambapo CUF ni mshirika, kumsimamisha Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kugombea nafasi ya urais.

Hata hivyo, Juni mwaka jana, Profesa alitengua barua yake na kuirejea nafasi ya uenyekiti ndani ya chama hicho na kusababisha mgawanyiko wa pande hizo mbili, huku upande wa Maalim Seif ukipinga hatua hiyo.

 

Bunge na Maalim Seif kuwafukuza kina Sakaya

Katika hatua nyingine, jana Ofisi ya Bunge, ilitoa taarifa ikielezea kupokea barua ya Maalim Seif, yenye maelezo ya kuwafuta uanachama wabunge wawili, Sakaya na Maftaha Nachuma.

Taarifa hiyo ilisema, licha ya barua ya Maalim Seif, Bunge tayari lilishapokea barua ya Profesa Lipumba Machi 22, ikiliarifu Bunge kuwa Maalim Seif ameshindwa kutekeleza majukumu yake kama Katibu Mkuu, hivyo kuanzia tarehe hiyo majukumu hayo yalianza kutekelezwa na Sakaya.

Ilisema barua ya Prof Lipumba ilikuwa na kiambatanisho cha ridhaa ya mabadiliko hayo kwa barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa na kwamba Ofisi ya Spika haikuwahi kupokea barua yoyote ikieleza tofauti.

 

 

Wabunge waliofukuzwa wakwaa kisiki cha kwanza

Katika hatua nyingine, wabunge wanane waliovuliwa uanachama na Profesa Lipumba, baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupa maombi yao ya kutaka walioteuliwa kuziba nafasi zao wasiapishwe na Bunge.

Akisoma uamuzi huo jana, Jaji Lugano Mwandambo, alisema mahakama hiyo imetupilia mbali maombi hayo kutokana na kuwapo kwa mapungufu ya kisheria.

Alisema wabunge hao waliwasilisha mapingamizi manne, lakini kati ya hayo, mahakama imeamua kujibu pingamizi moja, ambalo ni la kuitaka mahakama kupinga kutoapishwa kwa wabunge wateule.

Alisema mahakama imeamua kutupilia mbali pingamizi hilo kwa sababu kifungu kilichotumika kufungua maombi hayo si sahihi.

Alisema kutokana na hali hiyo, maombi mengine matatu hayawezi kusikilizwa.

“Mahakama imeamua kutupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na wabunge waliovuliwa uanachama wa CUF kwa sababu kifungu kilichotumika hakijakidhi matakwa ya kisheria,” alisema Jaji Mwandambo.

Katika maombi hayo madogo  namba 447 ya mwaka huu, mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo ni Katibu wa Bunge, wa pili ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), mdaiwa wa tatu Bodi ya Wadhamini wa Chama cha CUF pamoja na wabunge wateule.

Akizungumza nje ya mahakama mara baada ya maamuzi madogo ya pingamizi kutolewa  mahakamani hapo jana, wakili wa upande wa wabunge wateule na Bodi ya Wadhamini CUF, Mashaka Ngole, alisema uamuzi wa jaji unaashiria kuwa wabunge wateule wanaweza kuapishwa pindi Bunge likavyoona inafaa.

Alisema kwa sasa hakuna kinachozuia wabunge hao kuapishwa, hata kama maombi hayo yatarejeshwa upya mahakamani hapo.

Naye Naibu Mkurugenzi wa Habari, Mahusiano na Umma, Mbarara Maharagande, alisema: “Wabunge wanaandaa nyaraka nyingine kwa kurekebisha makosa yaliyojitokeza ili iingizwe mahakamani, hii kitaalamu  inaitwa Struck out Application na siyo Dismissal Application”.

Wakili wa wabunge hao waliofukuzwa, Peter Kibatala, jana saa 8:00 alitarajiwa kuwasilisha tena maombi, alisema anakwenda kuyafanyia marekebisho mapungufu hayo na kisha kuyarudisha tena mahakamani hapo.

Wabunge hao waliofukuzwa ni Niza Bakari Haji, Saverine Mwijage, Salma Mwassa, Raisa Abdallah Salum, Halima Ali Mohammed na Saumu Heri Makala.

Wabunge hao walifukuzwa pamoja na madiwani Elizabeth Alatanga Magwaja na Layla Hussein Madiba.

Wabunge hao walifungua maombi Mahakamani Kuu wakiomba itoe amri ya zuio kwa Bunge ili wabunge walioteuliwa baada ya wao kuvuliwa uanachama wasiapishwe kusubiri kusikilizwa na kutolewa maamuzi kwa kesi waliyofungua kupinga kuvuliwa uanachama wa chama hicho.

Hata hivyo, shauri la msingi namba 143, 2017 lipo palepale  litasikilizwa Agost 31, 2017 katika mahakama hiyo.

Wafuasi wazichapa

Awali kabla ya kesi hiyo kuanza, wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF) wanaodaiwa kumuunga mkono Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na ule upande unaomtii Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, walipigana nje ya Mahakama Kuu.

 

Mapigano hayo yalianza saa 4:30 baada ya kujitokeza kwa majibizano ya pande hizo mbili, ndipo askari polisi waliwatuliza na kuwaondoa katika eneo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles