28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

LOWASSA JUKWAA MOJA NA KENYATTA

NAIROBI, Kenya

MIEZI kadhaa tangu Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),  kitangaze kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika kampeni zake za kutaka achaguliwe tena, Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Lowassa, ameamua kupanda jukwaani kumpigia debe katika kampeni za lala salama.

Baadhi ya tovuti za magazeti na mitandao ya Kenya jana ziliandika habari na hata kutoa picha zinazomwonyesha Lowassa akihutubia maelfu ya Wakenya katika mkutano wa kampeni za urais huko Suswa, katika Kaunti ya Narok, nchini Kenya.

Lowassa, ambaye alikuwa ameambatana na Uhuru, habari ambazo MTANZANIA Jumamosi limezikusanya kutoka katika mitandao hiyo zinaeleza kuwa, alitangaza kumuunga mkono Uhuru katika kinyang’anyiro hicho mbele ya jamii tano za Kimasai zenye asili ya Tanzania.

Lowassa anatokea katika jamii ya Masai na kwa muda mrefu alikuwa mbunge wa Jimbo la Monduli, linalokaliwa kwa wingi na watu wa jamii hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo, ambao pia Rais Kenyatta alihutubia, Lowassa alisisitiza kuwa Wakenya wote wanatakiwa kulinda amani katika kipindi chote za kampeni za uchaguzi.

Awali, Rais Kenyatta alitembelea nyumbani kwake katika Kaunti ya Kiambu na kufanya mkutano wa kampeni katika uwanja wa Kiringiti, na kuwasisitiza wakazi wa eneo hilo kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Jumanne ijayo ya Agosti 8, ili kuweka historia ya kuchaguliwa mara ya pili katika kiti cha urais.

Taarifa nyingine zinaeleza kuwa, Lowassa anatarajiwa kutoa hotuba ya kampeni za uchaguzi katika Uwanja wa Kasarani, jijini Nairobi.

Chadema kilitangaza tangu mwanzoni mwa Mei, mwaka huu, kuwa kinamuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Agosti 8, mwaka huu.

Msimamo huo ulitangazwa pia na Lowassa, ambaye aligombea kiti cha urais kwa tiketi ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu uliopita.

Akizungumza katika mahojiano maalumu mapema mwezi uliopita wakati akiwa nchini Kenya kushiriki mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani wa Kenya, Joseph Ole Nkaissery, Lowassa alisisitiza kuwa, Kenyatta ni chaguo bora la demokrasia nchini Kenya.

 

Katika mahojiano hayo, Lowassa alimtaja Kenyatta kama mtu mzuri anayeunga utangamano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na anawaheshimu viongozi wa upinzani.

Weledi wa mambo wanaamini kuwa, Chadema kinamuunga mkono Rais Kenyatta kutokana na uhusiano wa karibu uliopo kati ya Rais Dk. John Pombe Magufuli wa Tanzania na kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga.

 

Freeman Mbowe, Mwenyekiti Taifa wa Chadema, alinukuliwa Mei mwaka huu akimtaja Raila Odinga kuwa ni msaliti, kutokana na kumuunga mkono Rais Magufuli.

 

Mbowe alinukuliwa akisema kuwa, katika uchaguzi wa mwaka 2013 nchini Kenya, walimuunga mkono Odinga, lakini walishangazwa mno katika uchaguzi wa mwaka 2015 nchini Tanzania wakati Odinga alipotangaza kumuunga mkono mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles