30.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI: HATUTAKI UMEME WA MATAPELI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli amesema serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya umeme kwa kuhakikisha nishati hiyo inakuwa ya uhakika na kuachana na umeme wa matapeli.

Aliyasema hayo jana alipozungumza na wakazi wa Mkoa wa Pwani katika Uwanja wa Bwawani wakati wa ziara yake mkoani humo.

“Najua watu watanuna kwa hatua ninazochukua, tutapata shida kidogo lakini nataka niwahakikishie tutafika.

“Tuachane na umeme wa matapeli wanaowekeza kwa lengo la kutuibia na kwa kweli wezi watakoma. Awe anatoka Magharibi, Mashariki ama Kusini mwizi ni mwizi tu,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Alisema suala la umeme limekuwa na matatizo mengi na kusababisha watendaji wasio waaminifu kuingia mikataba iliyoisababishia nchi hasara.

“Wamekosa uzalendo na huruma hata kwa wazazi wao waliowasomesha. Naomba muendelee kuniruhusu hawa nilale nao mbele mpaka waikome kabisa.

“Tutaendelea kubana mianya yote iliyokuwa ikitumika kwa lengo la kulifanya Taifa kuwa masikini,” alisema.

Alisema miradi ya umeme ya Kinyerezi 1, 2 na 3 itapanuliwa na mradi mwingine uliofanyiwa utafiti tangu wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza utafufuliwa upya   kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika.

Alisema  hadi kufikia mwaka 2020 vijiji 331 vya Mkoa wa Pwani  vitakuwa na umeme ambako miradi hiyo itatekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa gharama ya Sh bilioni 30.2.

“Ukiona wachache wanalalamika ama kulia kwamba unatumbua sana waambieni hujatosha kutumbua endelea kutumbua…ujue Magufuli anachapa kazi,” alisema.

Rais Dk. Magufuli pia alitaka kila kiongozi katika nafasi yake ajitathmini badala ya kusubiri hadi waondolewe.

“Kila kiongozi ajitathimini anawajibikaje kwa wananchi wa maisha ya chini, ukishindwa kujitathmini usisubiri miaka miwili ifike, jiondoe mwenyewe ukapumzike,” alisema.

Rais Dk. Magufuli aliwataka wananchi wa mkoa huo kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kuwabaini wahalifu wanaojihusisha na vitendo vya mauaji  wilayani Kibiti.

Alisema hakuna mwekezaji atakayekwenda kuwekeza katika maeneo hayo wakati watu wanauana na kwamba wanaochelewesha maendeleo ya wilaya hizo ni wananchi wenyewe kwa sababu wanawajua wanaofanya vitendo hivyo.

“Serikali ya Awamu ya Tano si ya kuchezewa, moto wameshaanza kuupata, waache, watanyooka, hawatapita na ninasema hawapiti.

“Hakuna dini inayosema watu tuuane, tuendelee kuwaombea (wahalifu) waokoke na kujua damu ya mtu ina thamani kubwa,” alisema.

VIWANDA

Kuhusu viwanda, Rais Dk. Magufuli aliupongeza uongozi wa Mkoa wa Pwani kwa kutekeleza dhana ya Tanzania ya viwanda kwa vitendo kwa sababu  ndiyo mkoa unaoongoza kwa kuanzisha viwanda vipya vikubwa.

“Nimetembelea Pwani leo (jana) nina amani sana kwa sababu viongozi wamenikuna moyo wangu. Nikisema niamue kuzunguka kuvifungua ama kuweka mawe ya msingi nitahitaji mwezi mzima.

“Huwezi kutegemea viwanda vya nje, ukinunua nguo kutoka Ulaya unakuwa umetengeneza ajira za watoto wao,” alisema.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Pwani,   Evarist Ndikilo, alisema zaidi ya viwanda 300 viko katika hatua mbalimbali za ujenzi na vingine vimeanza uzalishaji.

“Matunda tunayaona na tunatarajia kupokea wawekezaji wengi zaidi, ajenda ya ujenzi wa viwanda katika mkoa wetu inazungumzwa kwa lugha moja,” alisema   Ndikilo.

Hata hivyo alisema mkoa unakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile kutokuwapo umeme wa uhakika, gesi, maji na ubovu wa miundombinu.

Alisema mahitaji ya umeme kwa sasa ni megawati 60 lakini unaopatikana ni megawati 40.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles