MACHINGA, MAMALISHE, MA-MC RASMI KULIPA KODI

0
797

NA KULWA MZEE-DODOMA


SERIKALI imetangaza rasmi kuanza kukusanya kodi kwa wafanyabiashara ndogondogo (machinga), watoa huduma za chakula na washereheshaji (MC) katika mwaka wa fedha 2017/18.

Hayo yalisemwa jana bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango alipokuwa akihitimisha hotuba ya bajeti yake ya mwaka 2017/18 baada ya kupitia hoja na mapendekezo mbalimbali ya wabunge.

“Ili kuwahamasisha wafanyabiashara wadogo kurasimisha shughuli zao, Serikali iweze kukusanya kodi, utaratibu nilioutangaza kuwatambua wafanyabiashara wa aina hii na kuwapa vitambulisho utahusisha wafanyabiashara ndogondogo, watoa huduma za chakula, washereheshaji (MC) na wafanyabiashara ndogondogo wasio rasmi wanaofanya biashara maeneo yaliyo rasmi,”alisema.

Serikali kwa kuzingatia ushauri imefuta kodi kwa magari ya kubebea wagonjwa, leseni na vibali vya uwindaji, ada ya tathmini ya mazingira kwa wawekezaji wote wa viwandani na tozo kwa shule binafsi.

Waziri Mpango alisema katika mjadala wa bejeti, michango yote yenye afya serikali imeichukua na kuifanyia kazi katika bajeti hiyo na mingine itashughulikiwa bajeti ijayo.

“Tumependekeza kufuta kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika magari ya kubebea wagonjwa kwa kutambua mahitaji ya wananchi hasa wa vijijini.

“Serikali imeamua kufanya marekebisho  kusamehe VAT katika magari hayo, hatua hii itahusisha magari yanayoingizwa nchini yakiwa yametengenezwa kwa kubebea wagonjwa kwa ajili ya hospitali na vituo vya afya vilivyosajiliwa.

“Seriali itatumia Hazina katika kusamehe kodi na kodi inayosamehewa Serikali italipa Hazina   kudhibiti msamaha,”alisema.

Alisema   kodi katika ada na leseni za uwindaji imeondolewa   kuhamasisha sekta ya utalii na   ada ya tathmini ya mazingira kwa wawekezaji wote wa viwandani nayo imeondolewa.

Alisema kulikuwa na hoja  kuwa Serikali ifanye marekebisho kwenye sheria ya mitandao ya simu, baada ya kutafakari imefanya marekebisho ya sheria hizo.

Waziri lisema  hisa asilimia 25 zitakazouzwa, ziuzwe kwa umma ili kujumuisha Watanzania au kampuni yoyote ya Watanzania wanaoishi nje, hisa zimilikiwe kwa pamoja na Watanzania na watu wa nje kwa vile  sharti lililopo kwa sasa hisa husika kuuzwa kwa wale waliopo nchini tu.

Serikali pia imeziondoa kampuni ndogo za mawasiliano katika sharti la kuuza hisa katika soko la hisa na kubaki na kampuni kubwa ambako itakayoshindwa kufikia mauzo ya asilimia 25, waziri mwenye dhamana atatoa maelekezo ya namna kampuni husika itakavyoweza kutoa hisa hizo.

“Utozaji wa tozo katika vyombo vya uvuvi, wavuvi wanatozwa tozo mbalimbali kwa fedha za kigeni na kampuni zilizosajiliwa nchini, naagiza kampuni ziache utaratibu huo na zianze kutoza kwa kutumia shilingi ya Tanzania.

“Tulipokea ushauri, Serikali iangalie uwezekano wa kukusanya kodi katika sekta ya michezo ya kubahatisha, kwa kuzingatia ushauri huo tumeona kuna uwezekano wa kupata mapato mengi katika sekta hiyo.

“Kuanzia Julai Mosi mwaka huu, mapato yote yatokanayo na michezo ya bahati nasibu yatakusanywa na TRA, yatapelekwa mfuko mkuu wa Serikali…baadaye Serikali itaangalia jinsi ya kuyarejesha,”alisema.

Alisema kulikuwa na hoja ya kodi na tozo 16 ambazo zinatozwa shule binafsi, Serikali imesikia maoni na kuondoa baadhi ya tozo.

“Serikali imesikia kilio hicho na kuamua kuondoa tozo ya kuendeleza mafunzo ya ufundi na ada ya zimamoto, lengo kuziwezesha shule kutoa elimu kwa gharama nafuu.

“Wamiliki watapokea dhamira njema ya Serikali na kupitia ada wanazotoza   kuzipunguza ili watoto wanaotoka familia masikini waweze kumudu ada,”alisema.

Akizungumzia kiwango cha utegemezi, Waziri Mpango  alisema kimeendelea kupungua kwa sababu  fedha za nje katika bajeti ya mwaka 2011/12 zilikuwa Sh trilioni 3.9, mwaka 2012/13, Sh  trilioni 3.1, mwaka 2013/14  Sh trilioni 3.8, mwaka 2014/15  Sh trilioni 2.9, mwaka 2015/16 zilikuwa Sh trilioni 2.3 na mwaka 2016/17  fedha kutoka nje zilikuwa Sh trilioni 3.6.

“Kulikuwa na hoja ya malimbikizo ya madeni mbalimbali  yakiwamo ya wazabuni na wakandarasi, Serikali inaendelea kuhakiki madai hadi Juni 2016, madai yaliyofikishwa yalikuwa zaidi ya Sh trilioni 2.9 baada ya kuyahakiki madeni halali yalikuwa zaidi ya Sh trilioni 1.9.

“Serikali ilifanikiwa kulipa Sh bilioni 796.5, jumla ya deni lililobakia ni Sh trilioni 1.2. Katika bajeti ya mwaka 2017/18 Serikali imetenga  a Sh trilioni moja  kwa ajili ya kulipa madai hayo,”alisema.

Akizungumzia tozo ya Sh 50 kwa mafuta, alisema Serikali ilishauriwa kuongeza tozo ya Sh 50 kwa kila lita ya mafuta.

“Hii ilikuwa hoja mama ilitawala mjadala wa bajeti 2017/18, Serikali ilipotafakaari ikafuta ada ya leseni ya magari ambayo ilikuwa ikilalamikiwa na wenye magari kwa sababu  magari yamekuwa yakitozwa ada hiyo hata yasiyotembea hivyo tukaamua kuongeza Sh 40 kwa kila lita ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa,” alisema.

Baada ya ongezeko hilo, wabunge waliwasilisha michango mbalimbali ambako wengine walisema ongezeko hilo lingesababisha gharama za maisha kupanda kutokana na bei hiyo ya nishati kuongezeka.

Alisema kuongezeka   Sh 40 katika   petroli, dizeli na mafuta ya taa inalenga kuwalinda Watanzania na uchakachuaji wa mafuta.

Alisema kama haitaongezwa Sh 40  katika mafuta ya taa tofauti itakuwa Sh 93 kwa lita, tofauti ambayo itachangia uchakachuaji na itasaidia kupata mapato ya kuhudumia huduma muhimu kama afya.

Alisema tozo za kodi za nyumba Sh 10,000 kwa nyumba za kuishi na Sh 50,000 kwa nyumba ya ghorofa inatozwa kwa mujibu wa sheria za mamlaka za miji.

Kodi hiyo,itatozwa katika majengo yaliyojengwa katika mamlaka za majiji, miji na majiji madogo lakini nyumba za vijijini hazihusiki katika kodi hiyo.

“Kwa mujibu wa sheria, wananchi wenye umri wa zaidi ya miaka 60 hawapaswi kulipa kodi ya majengo wanayoyatumia kama makazi yao wenyewe,”alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here