Na Samwel Mwanga
WAGANGA wa tiba asili wilayani Busega wamekemea tabia ya baadhi ya wenzao wanaotumia viungo vya albino kupiga ramli.
Wamependekeza watu wa aina hiyo wakikamatwa wanyongwe hadharani bila kufikishwa mahakamani.
Mapendekezo hayo yalitolewa jana na Mwenyekiti wa Chama cha Waganga wa Tiba asili wilayani humo, Peter Magubu, katika mkutano wa wanachama wa chama hicho.
Mkutano huo ulikuwa na lengo la kuhakikisha vitendo vya kuuawa albino vinatokomezwa katika Wilaya ya Busega.
Alisema njia nyingine ya kutokomeza vitendo hivyo ni pamoja na serikali kuhakikisha inawasajiliwaganga wote wa tiba asilia.
Magubu alisema hatua hiyo itarahisisha kuwatambua ni yupi anayejihusisha na ukatili wa namna hiyo aweze kuchukuliwa hatua kali za sheria.
Alisema kwa sasa matapeli ni wengi ambao wamevamia na kufanya shughuli hizo kwa lengo la kutaka kujipatia fedha.
Alisema kwa sababu hiyo inabidi serikali isiwafumbie macho kwa sababu hakuna ukweli wowote kuhusu jambo
hilo la viungo vya albino kuwatajirisha watu.
“Tunaiomba serikali iwanyonge watu hao wanaobainika kutumia viungo hivyo vya binadamu wenzetu iwe fundisho kwa walio na imani hizo za kijinga,” alisema.
Mratibu Mkuu wa Wilaya wa Tiba asili, John Balele aliwaomba waganga wote wa chama hicho na wale wasio wanachama wilaya humo kuonyesha umoja na mshikamano.
Alisema hiyo itakuwa ni katika kuhakikisha wanakomesha jambo hili la udanganyifu wa matumizi ya viungo vya albino nchini.
“Kwa sasa serikali inatakiwa kupiga marufuku vituo vya kuwalea albino jamii iweze kukaa nao majumbani.
“Wnapozidi kukaa katika vituo hivyo wanajionakutengwa jambo ambalo linawafanya kutokuwa na amani,”alisema.