26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Maalim Seif aenda kufuata nyayo za Lipumba

 maalim

NA FLORENCE SANAWA, MTWARA

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Maalim Seif Sharif Hamad, leo anatarajia kuanza ziara ya siku mbili mkoani Mtwara ambako pamoja na mambo mengine, atazungumzia mwelekeo wa hali ya kisiasa nchini, kwa kuzingatia tathmini iliyofanyika hivi karibuni ya utawala wa mwaka mmoja wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli.

Hii ni ziara ya kwanza kwa Maalim Seif kwa upande wa Tanzania Bara tangu chama hicho kikumbwe na mgogoro ambao msingi wake ni uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kumrudisha katika nafasi yake ya uenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba.

Wakati Maalim Seif akitangaza kufanya ziara hiyo, zipo taarifa zinazoeleza kuwa   Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinatarajiwa kuanza mikutano ya ndani nchi nzima kwa siku 40, iliyopewa jina la amsha amsha.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Mtwara, Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma, Mbarara Maharagande, alisema ziara hiyo itajumuisha viongozi mbalimbali wa kitaifa ndani ya chama.

“Katika ziara hiyo kiongozi pia atapata nafasi ya kuzungumzia masuala mbalimbali, ikiwemo mwelekeo wa hali ya kisiasa nchini, ukizingatia tathmini iliyofanyika hivi karibuni juu ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Tano madarakani,” alisema Mbarara.

Kwa mujibu wa Mbarara, katika ziara hiyo Maalim Seif ataambatana na wajumbe wa kamati ya uongozi Taifa, wakurugenzi wa chama Taifa, wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa na baadhi ya wabunge kwa  lengo la kukagua shughuli mbalimbali za ndani ya chama.

“Viongozi hao watakagua shughuli za chama, ikiwemo kupata maoni na mapendekezo mbalimbali na namna ya kuboresha utendaji wa chama ngazi za chini na kuziwasilisha kwa wawakilishi wao, ikiwemo wabunge,” alisema Maharagande.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Taifa, Shaweji Mketo, alisema dhamira kuu ni kufanya shughuli za kimaendeleo na kuwaona wadau na kuzipokea kero hizo.

“Matatizo ndani ya chama yapo, hatuwezi kukaa kusubiri yaishe ndiyo tuanze kufanya shughuli za chama, zipo tofauti za kimitazamo katika kutatua matatizo ya Watanzania, ndiyo maana tunaendelea na shughuli mbalimbali za ndani ya chama.

“Hii issue (suala) ya Profesa Lipumba kunitengua lipo katika mahakama, hatuwezi kujadili uhalali, si sehemu ya kujadili hilo, tusubiri mahakama itoe uamuzi ili tujue nani yuko sahihi na nani hayuko sahihi,” alisema Mketo.

Maalim Seif anafanya ziara hiyo baada ya Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Lipumba, kumaliza ziara yake ya wiki mbili aliyoifanya mwanzoni mwa Oktoba, wakati ambao chama hicho kikiwa katikati ya mtanziko kutokana na mgogoro wa kiuongozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles