26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AMPELEKA DCI DIWANI KAGERA

diwani

RAIS Dk. John Magufuli ametekeleza ahadi yake ya kumpangia kazi nyingine aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai (DCI) Diwani Athuman, ambaye sasa amemteua kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.

Uamuzi huo wa Rais Magufuli umefikiwa jana, ikiwa ni siku ya 20 tangu Diwani aondolewe katika nafasi hiyo Oktoba 29, mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilieleza kuwa uteuzi huo umeanza mara moja.

Itakumbukwa wakati Rais Magufuli alipotangaza kumwondoa Diwani katika nafasi hiyo ya DCI, hakueleza sababu yoyote, lakini yaliibuka madai mbalimbali yaliyosababisha uamuzi wake huo.

Miongoni mwa madai hayo, ambayo hayakuwahi kuthibitishwa na si tu Ikulu ya Rais Magufuli, bali pia Jeshi la Polisi, ni kwamba kiongozi huyo alishindwa kutimiza wajibu wake sawasawa, hasa ya kushiriki ipasavyo katika operesheni maalumu zinazofanywa kimya kimya dhidi ya watu waliotajwa kuwa ni wahujumu uchumi, wakiwemo watuhumiwa wa ujangili wa meno ya tembo.

Wakati huo huo, Rais Magufuli alifanya uteuzi wa wenyeviti wa bodi katika taasisi tano za Serikali, huku akimteua Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Uteuzi huo wa Jaji Warioba, ambaye pia alipata kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, ulianza Novemba 16, mwaka huu.

Mbali na Warioba, Rais Magufuli alimteua Dk. Jones Kilimbe kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), huku Sylvester Mabumba akiwa Makamu wake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, uteuzi huo ulianza tangu Novemba 17, mwaka huu.

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa, Rais Magufuli alimteua Prof. Patrick Makungu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uhandisi na Usanifu Mitambo (TEMDO), ambaye uteuzi wake ulianza Novemba 16, mwaka huu, huku Martin Madekwe akiteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Fidia ya Ardhi tangu Novemba 17, mwaka huu.

Pamoja na hao, Rais Magufuli alimteua Prof. Raphael Chibunda kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wakurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kitropiki Tanzania (TPRI), uteuzi ulioanza Novemba 17, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles