UONGOZI wa klabu ya Simba, umepanga kuvunja benki kwa kuwaongezea mkataba mnono wachezaji wake mahiri na muhimu, akiwamo Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Ibrahim Ajibu, kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Desemba 17 mwaka huu.
Simba imefikia uamuzi huo baada ya kuona wachezaji hao wakinyemelewa na mahasimu wao Yanga, huku mikataba yao ikiwa inaelekea ukingoni
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Haji Manara, alisema hakuna mchezaji muhimu watakayempoteza msimu huu kwani wana mpango kabambe wa kuhakikisha wanawapa mikataba wachezaji wote waliomaliza na walio mbioni kumaliza mikataba yao.
“Mengi yatazungumzwa, lakini mpango wetu ni kuhakikisha tunawapa mikataba wachezaji wote tunaowahitaji na ukiona hadi tunaanza mzunguko wa pili mchezaji hajapewa mkataba mpya, ujue huyo hatuna mpango naye.
“Kila kitu katika klabu yetu kinakwenda kwa utaratibu maalumu, hivyo haraka sana tutahakikisha suala la mikataba linakuwa hadithi,” alisema Manara.
Mbali na Tshabalala na Ajibu, wachezaji wengine wanaotarajia kupewa mkataba ni Abdi Banda na Jonas Mkude, huku Awadhi Juma akiwa na hatihati ya kutemwa na klabu hiyo.