Na FARAJA MASINDE,
KUSOMA nje ya nchi mara nyingi kunampa mwanafunzi fursa adimu ya kujifunza mambo mbalimbali yanayoendelea duniani, hasa kwenye mataifa yaliyopiga hatua kubwa kiuchumi na kitaaluma.
Hata hivyo, wengi wamekuwa wakishindwa kufikia ndoto zao hizo za kuchukua taaluma zao nje ya nchi kutokana na kushindwa kumudu gharama kubwa zinazotozwa na vyuo husika, jambo ambalo limekuwa likichangiwa pia na kuporomoka kwa thamani ya shilingi.
Inaelezwa kuwa mara nyingi unapohitaji kusoma nje ya nchi basi huna budi kuhakikisha kuwa unaangalia gharama za masomo pamoja na zile za kumudu maisha ya nchi unayotaka kwenda kusoma. Hii ni sababu mojawapo inayobadili uamuzi wa wanafunzi kusoma nje ya nchi.
Kwa mwaka huu wa 2016 kuna orodha ya miji ambayo ni rafiki kwa mwanafunzi kumudu gharama zake za maisha ikilinganishwa na miji mingine duniani.
Kuala Lumpur, Malaysia
Kwa kawaida wanafunzi wengi wanapokuwa wakisoma nje ya nchi kwenye mji fulani hupenda kuzunguka sehemu mbalimbali kwa ajili ya kujifunza tamaduni na mambo tofauti tofauti nje ya kupata elimu.
Mji huu Kuala Lumpur ni kati ya miji ambayo maisha yake ni nafuu kwa wanafunzi.
Unafuu huu unaanzia kwenye ada ya vyuo vyake ambayo iko chini tofauti na mataifa mengine, lakini pia bei za bidhaa mbalimbali ni nafuu mno ikilinganishwa na nchi nyingine ikiwamo gharama za kulipia pango.
Tunaelezwa kuwa unapokuwa kwenye mji huu una uhuru wa kufanya mambo yako bila kuingia madeni ya aina yoyote kutokana tu na unafuu wake.
Berlin, Ujerumani
Kama lengo lako ni kwa ajili ya kujifunza pia utamaduni wa nchi unayotaka kwenda kusoma bila kutumia gharama kubwa, basi mji wa Berlin ni nafuu ambao unasifika barani Ulaya kwa kuwa na kiwango kidogo cha ada kwenye kozi mbalimbali utakazo taka kusoma.
Toulouse, Ufaransa
Paris, Ufaransa ni mji bora kwa kwa ajili ya kusoma nje ya nchi lakini unagharama kubwa za maisha, hivyo kama nia yako ni kusoma nchini humo basi mji unaokufaa ni Toulouse.
Brisbane, Australia
Unapokuwa unasoma kwenye mji huu ni sawa na kuwa kwenye kitovu cha Ausralia na hii inatokana na kiwango cha chini cha gharama za masomo ambacho kinatajwa kuwapo kwenye mji huu na hata Australia kwa ujumla. Kwa ujumla gharama za kuishi kwenye mji huu ni nafuu mno.
Ukiwa nchini humo unaweza kutembea kwenye miji mbalimbali ukiwa mwanafunzi kutokana gharama za usafiri na vitu vingine kuwa ndogo.
Miji mingine mbayo mwanafunzi unashauliwa kwenda kusoma iwapo lengo lako ni kuokoa kiasi cha fedha kwa maana ya kutotaka kusoma kwa mateso ni pamoja na Warsaw, Poland ambao unaweza kuokoa kiwango kikubwa cha fedha hasa siku za mwisho wa wiki.
Pia kuna miji kama Munich ambao ni wa pili kwa Ujerumani kuwa kwenye orodha hii. Valencia, Hispania, Philadelphia, Pennsylvania, Marekani, Taipei, Taiwan, Vienna, Austria.