NA MANENO SELANYIKA, DAR ES SALAAM
KADIRI dunia inavyobadilika ndivyo malezi ya watoto nayo yanabadilika.
Miaka ya nyuma walezi au wazazi walitumia njia ya kuwachapa viboko watoto kama adhabu pekee inayoweza kumrekebisha mtoto kitabia.
Hivi sasa kada mbalimbali wakiwamo watoto wenyewe wanaona adhabu ya viboko si nzuri kwa madai kuwa inamjengea mtoto woga, usugu na ujeuri.
Akizungumza na TOTO kona mapema wiki hii Rahma Mfaume (10), anayeishi na wazazi wake maeneo ya Kinondoni Msisiri, Dar es Salaam anasema kumpiga mtoto si adhabu sahihi kwa karne hii.
“Ni kweli wakati mwingine sisi watoto tunafanya makosa yanayostahili adhabu lakini, mnafahamu kwamba mkituchapa viboko mnaweza kutusababishia matatizo makubwa kuzidi hayo makosa kama vile visasi, usugu na hata ujeuri,” anasema Rahma
Mtoto huyo anasema ni bora walimu, wazazi na watu wengine wafanye mazungumzo na watoto na si kutumia jazba, vitisho na kuwachapa bakora kwani watawaathiri kisaikolojia.
“Mimi pia nimeshawahi kuadhibiwa na wazazi na walimu shuleni napewa adhabu ya kumwagilia maua au kufanya usafi hii pia ni fundisho kwangu na siwezi tena kurudia kosa lile,” anasema.
Rahma anawaasa watoto wenzake kuacha kiburi pia wasijihusishe na marafiki wabaya watakao waingiza kwenye vishawishi viovu vinavyosababisha wazazi au kuwachapa viboko.