25.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 6, 2022

Contact us: [email protected]

Nyerere alianza, wengine walishindwa JPM malizia

jpmama1

Na Tobias Nsungwe

KATIKA tawala zote zilizopita  vitendo vya ukabila, rushwa na upendeleo kazini vilikuwapo.

Hii ina maana kuwa hata wakati wa utawala wa awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere vitendo hivyo vilikuwa vinazungumzwa na kutolewa matamko kadhaa. Pengine kwa wakati huo ilitokana na uchanga wa taifa letu ambalo ndio kwanza lilikuwa limetoka kwenye makucha ya wakoloni.

Mwalimu Nyerere alikwishaziona dalili za wachache kujineemesha matunda ya uhuru huku wananchi wengi wakibaki masikini wa kutupwa, mwaka 1967 akaanzisha Azimio la Arusha kupitia chama cha TANU (Tanganyika African National Union).

Kwa kuwakumbusha tu vijana wetu hiki ndicho chama kilichoanzishwa mwaka 1954 na kufanikiwa kuipatia Tanganyika Uhuru Desemba 9, 1964.

Mashirika mengi yalitaifishwa zikiwemo shule za sekondari ambazo zilifanywa kuwa mali ya Serikali. Wengi hawakufurahishwa na uamuzi ule wa TANU akiwemo marehemu Oscar Kambona aliyekuwa mmoja wa makada muhimu wa chama hicho.

Waziri huyo wa zamani  wa ulinzi katika Serikali ya Tanzania hakuzipenda kabisa sera za ujamaa alizokuwa akiziimba Mwalimu Nyerere akisaidiana na Mzee Rashid Kawawa.

Kufuatia sera za kutaifisha mali, baadhi ya wachambuzi wa mambo ya historia ya TANU na Tanzania wanatueleza kwamba hata mali Kambona zilichukuliwa. Hadi kufikia mwaka 1966, inadaiwa Kambona alikuwa na mali nyingi kwa wakati huo.

Alidaiwa kumiliki majumba katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Ruvuma. Sera za ujamaa na utaifishaji zilikuwa na lengo zuri.

Hata hivyo baadhi ya viongozi wa mashirika yaliyofanywa ya umma walizifanya taasisi hizo kuwa vichaka vya rushwa, upendeleo na ukabila.

Inadaiwa moja ya sababu za kuzorota kwa maendeleo ya Shirika la Taifa la Bima ilikuwa ni ukabila uliokuwa umekithiri ndani ya shirika hilo.

Wafanyakazi wengi wa shirika hilo walikuwa wanatoka katika kabila moja hususani analotoka mkurugenzi. Hata NBC ya zamani nayo ilikuwa na matatizo hayo hayo mpaka ikadhaniwa kwamba ukabila ndio nembo ya shirika hilo.

Hivi karibuni Rais John Magufuli amewapasha ukweli wakuu wa mashirika ya umma na kuwataka waache tabia ya kutoa upendeleo kwa viongozi na jamaa zao.

Rais Magufuli alitoa onyo hilo wakati wa uzinduzi wa ndege mbili zilizonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kulifufua Shirika la Ndege la ATCL

Kama alivyosema Rais Magufuli tabia ya matumizi mabaya ya mali za umma imeua mashirika mengi.  Bila kumung’unya maneno Rais alisema mmoja wa wafanyakazi wa shirika hilo ambalo limekuwa likituhumiwa kwa ubadhirifu kwa muda mrefu, ni mke wa mmoja wa mawaziri. (aliyepo madarakani au mstaafu) Mazingira kama haya ambayo mke wa mkubwa ameajiriwa kwenye shirika hilo yanaleta migogoro mikubwa ya migongano ya kimasilahi nchini.

Si ajabu kwa ‘mke wa waziri’ kushinikiza ndugu na jamaa zake kuajiriwa kwenye shirika hata kama hawana sifa. Hapa ndipo mazingira ya ushemeji yanapotengenezwa kwenye mashirika na taasisi za umma.

Rais Magufuli alitahadharisha na kusema;

“Bodi na wizara msimruhusu kiongozi asafiri bure, hata kama ni mimi, mnitoze nauli’’.

Akasisitizia kuwa wakuu wa mashirika wakijenga mazoea ya kujipendekeza kwa viongozi watajikuta wanatoa huduma ya bure, na kutolewa kwa wake, waume, jamaa au mahawara zao nao watashinikiza wapewe ‘vimemo’ ili wasafiri bure kwa kudhaminiwa na vigogo. Wakati wa kufanya mali za umma kama shamba la bibi umeisha.

Viongozi wanapoleta ushemeji na urafiki kwenye mali za umma ndio mwanzo wa miradi ya umma kuhujumiwa. Hata ripoti ya Serikali kuingia hasara ya Sh bilioni 23.4 katika mwaka wa fedha wa 2015/16 inatokana na baadhi ya viongozi kupeana tenda za Serikali kwa kujuana.

Hii inatokana na udhaifu wa Watanzania wengi wanapopata nafasi ya kuongoza kutaka kumfurahisha kila mtu. Anataka atumie dhamana aliyopewa kusimamia shirika au kiwanda kumfurahisha mkewe, mjomba, rafiki, dada, kaka na hata mpenzi.

Kwa muktadha huo Rais Magufuli anaonyesha kuwa na nia ya wazi ya kukabiliana na tabia ambazo Mwalimu Nyerere alizikemea.

Ikiwa Rais Magufuli atafanikiwa kutokomeza vitendo vyote vinavyosababisha mali za umma kuhujumiwa na kuondoa mfumo wa kupeana nafasi au kupandishana vyeo kwa misingi ya ukabila, udugu, ujamaa au uswahiba atakuwa anaumalizia mfupa alioucha Mwalimu Nyerere ambao watawala waliopita wameshindwa.

Mwalimu Julius Nyerere katika moja ya wosia wake aliwahi kuelezea sifa za ziada za uongozi. Miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Mwalimu Nyerere alipata kusema mbali ya sifa nyingine za uongozi mtu anapochaguliwa kuwa kiongozi lazima awe na uwezo wa kuhimili mashinikizo na changamoto kutoka kwa ndugu na marafiki zake.

Mwalimu Nyerere alikemea mara nyingi tabia ya baadhi ya viongozi kutumia nafasi zao kujinufaisha wao na familia zao. Akizungumzia urais, Mwalimu alisema mtu akichaguliwa kuwa rais lazima awe na uwezo wa kuwaambia marafiki na jamaa zake kwa kauli thabiti: Ikulu ni mahali patakatifu.

Msimamo uwe ni huohuo kwa viongozi wa taasisi na mashirika ya umma. Viongozi wajue wamekabidhiwa mali za umma ili wazilinde kwa niaba ya Watanzania wote.

Mtu akiteuliwa kuwa kiongozi lazima awe na na uwezo wa kuhimili usumbufu kutoka kwa ndugu na jamaa zao. Sifa za vyeti pekee hazitoshi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,606FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles