30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Butiku: Mwalimu Nyerere alituachia matatizo

BUTIKU*Asema CCM ni gwiji wa rushwa

Na ELIZABETH HOMBO

LEO ni miaka 17 tangu Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aiage dunia Oktoba 14, 1999, katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, iliyoko jijini London, Uingereza.

Mwalimu Nyerere anakumbukwa kwa mengi katika kipindi chake cha uhai duniani, kutokana na mchango wake mkubwa kwa taifa lake.

Pia anakumbukwa sana barani Afrika kwa kuwa kiongozi aliyesimamia kikamilifu harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika kutoka ukoloni mkongwe.

Oktoba 14 kila mwaka ni siku ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Gazeti hili limefanya mahojiano ya ana kwa ana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, ambaye aliwahi kuwa katibu wa Mwalimu kwa miaka mingi.

Pamoja na mambo mengine, Butiku anazungumzia miaka 17 ya Tanzania bila kuwepo kwa kiongozi huyo, huku akisema taifa bado lina umoja, japo kuna minong’ono kidogo ya ubaguzi.

MTANZANIA: Ni miaka 17 sasa tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere afariki dunia, ukiwa mmoja wa watu waliokuwa karibu naye, unadhani ni jambo gani limekosekana?

BUTIKU: Nyerere hayupo lakini mambo aliyoainisha karibu yote yapo. Kwanza tunalo taifa ambalo lina umoja na makabila 126, lakini Watanzania hatuulizani makabila wala hatubaguani.

Alitambua tofauti zetu kama watu, mfano elimu, jinsia, lakini hajatuachia ubaguzi. Bado Watanzania hatuna tatizo kubwa la kubaguana kama yalivyo mataifa mengine, hata jirani zetu.

Lakini kuna minong’ono kidogo sana na hasa ikifika wakati wa uchaguzi mtu akiona ameelemewa na hoja za wenzake ataanza oohh sijui mimi nimetoka kwa Nyerere huko mnichague ni uongo mtupu…sijui mimi dini fulani ni ujinga mtupu.

Kwa mfano zamani hakukuwa na ubaguzi wa maeneo ya kugombea kama ilivyo sasa kwamba mtu akitaka kugombea ubunge au udiwani lazima aende katika eneo lake alikozaliwa, hapo kidogo tumerudi nyuma. Ukienda nyumbani kwenu ni vizuri zaidi lakini zamani haikuwa hivyo.

Kuhusu sera zetu; msingi wake ni kuhakikishia hazibagui, zinasimama kwenye usawa, haubagui, kwa mfano elimu lazima kila mtu apate, afya kwa wote, japo tunachangia kidogo.

Pamoja na mambo mengi mazuri aliyoyafanya Mwalimu Nyerere, bado katuachia matatizo makubwa mawili ambayo ni rushwa na umasikini.

Rushwa bado haijakwisha, hasa wakati wa uchaguzi, kwa mfano kuna uchaguzi fulani kuna waziri mmoja alikuwa akigombea ubunge, akaja kwangu ananiambia kwamba ametumia fedha zake zote kwa kuwa amehonga lakini hakushinda. Ni vitu kama hivi rushwa imekuwa ni jambo la kawaida wakati wa uchaguzi.

MTANZANIA: Pengine nini kifanyike sasa ili tatizo hilo liweze kwisha?

BUTIKU: Kwanza kikubwa katika rushwa ni maadili, kwamba Watanzania wakatae rushwa, hasa viongozi waache kutafuta uongozi kwa kuhonga.  Lazima rushwa imalizike pale wote tutakaposema ni mbaya.

Rushwa ni ukimwi wa maadili, ukiugua usipoangalia huwezi kupona, hata taifa akipewa aongoze anayenunua uongozi kwa rushwa ipo siku nchi atauziwa mtu.

Inawezekana rushwa haiwezi kwisha kwa sababu ya umasikini, hiyo ni tabia mbaya tu. Kwa hiyo lazima rushwa imalizike, rushwa inatuondolea uhuru wa kuchagua viongozi wazuri, badala yake tunachagua wabovu ambao hawana sifa yoyote ya kuwa viongozi zaidi ya wala rushwa. Basi mkifika hapo mmepoteza taifa…tazama nchi zote zenye matatizo ni kutokana na rushwa.

Nitakupa mfano, najua ni kesi iko mahakamani, najua wapo wengi kesi haziishi wanabishana wee.. kwa sababu wamenyang’anyana haki kwa sababu ya kuhonga.

Na chama changu CCM ndicho gwiji wa rushwa na sioni aibu kusema jambo hili…narudia tena chama changu CCM ni gwiji wa rushwa.

Naamini CCM ikibadilika tutapata viongozi wazuri. Si hawa kila mahali anakopita JPM anakuta uchafu uchafu tu, wengine vyeti feki wamepataje? Rushwa!

Ajali ya nchi yenye rushwa ni kubwa na baadaye inaishia kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

MTANZANIA: Taasisi ya Mwalimu Nyerere tangu ilipoanzishwa ni jambo gani imelifanya ambalo mpaka sasa inajivunia?

BUTIKU: Tunasimamia maadili na amani, taasisi ilipoanzishwa haikupendwa sana au tuseme haikueleweka, wapo waliosema na wala si watu wadogo kwamba ilianzishwa kama hila na Mwalimu Nyerere, kwamba ni janja ya kuanzishwa chama mbadala.

Kitu kikubwa Mwalimu alichotuachia alisema anzisheni mdahalo ambao utawawezesha  watu kuzungumza watoe maoni yao, watu walipoanza kutoa maoni Serikali ikaogopa kwa sababu wananchi walikuwa wakitoa malalamiko yao viongozi wakaona ni upinzani.

Nakumbuka hata kiongozi mmoja alilalamika katika Kamati Kuu ya chama, alifanya taasisi hii isipendeke sana.  Sisi tumeendelea na midahalo ya Katiba, hata pale wengine wote waliponyamza sisi tuliendelea kusimama, unakumbuka mikutano tuliyofanya hata alivyotupiga Makonda (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda) lakini hatukuacha tuliendelea.

Jambo jingine ni amani, mfano msingi mmoja wa amani ni wananchi kuelewana, nadhani unakumbuka mwaka 2001 Zanzibar walivyopigana, ilipotokea ile vurugu bodi yetu ilikaa tukasema sisi hatuna tabia ya kupigana na polisi wetu hawana tabia ya kupiga wananchi mateke.

Tukaandaa taarifa kwamba, hii si tabia yetu na si nzuri, bahati mbaya hatukueleweka, tukaonekana tunaingilia utawala na tangu wakati huo kulikuwa na minong’ono mikubwa kwamba tunaingilia utawala, lakini sisi tulikuwa tunatetea msingi wa amani.

Kutokana na unyeti wa jambo hatukuacha kwenda kwa viongozi wetu kuwaambia hili si sawa kabisa, tukakwenda hadi kwa viongozi wa dini.

Baadaye tukawaita viongozi mbalimbali, wengi hawakuja, akaja Maalim Seif, Pius Msekwa akiwakilisha CCM, maaskofu mbalimbali…tukazungumza, lakini tatizo tuliloligundua ni kwamba viongozi hawazungumzi. Sasa taasisi yetu inaonekana kama hatufanyi kazi ila tunafanya.

MTANZANIA: Umegusia suala la Zanzibar, ambapo hata baada ya kufanyika uchaguzi wa marudio inaelezwa bado mambo hayako shwari, pengine mna jitihada gani za kuliweka sawa jambo hili?

BUTIKU: Nimekwenda huko nimeonana na Amani Karume, Makamu wa Pili na wakati mwingine tulikwenda na mapendekezo na tulipokelewa tukawaeleza kwamba je; hii hali vipi…lakini kiukweli hali si nyepesi kiasi hicho.

Kama viongozi hamuaminiani hata kuzungumza ni shida, hali ya viongozi kutoelewana mnamalizaje matatizo yenu.

Hamzungumzi kwa uwazi na ni dhahiri kwa mwenendo huu tatizo haliwezi kwisha.

Kutokana na haya yote, ndiyo maana sisi wakati mwingine tunaropoka kwa sababu ukweli tunaujua na nikichokozwa nitasema.

Tungoje uchaguzi ujao, tume itakuwa ile ile, taratibu zitafuatwa na kila mtu, kwa maana uchaguzi utakuwa wa huru na haki? Sisi tutaendelea kuzungumza kwa sababu haki huwa haipotei, kinachotakiwa ni subira. Demokrasia lazima izingatie historia ya watu.

Zanzibar kuna tatizo lakini wote tumekubaliana kwamba, fujo hazina maana na viongozi kule wamewatuliza wananchi na baadaye viongozi watagundua kwamba Watanzania hawataki fujo.

MTANZANIA: Pamoja na hayo, je, taasisi inakumbana na changamoto gani?

BUTIKU: Changamoto kubwa ya taasisi yetu ni kutoeleweka, wapo wanaoamini kwamba, ilikuwa mbinu ya Mwalimu Nyerere ya kuacha chama chake.

Changamoto nyingine hatuna fedha, kazi yetu ni ombaomba kwa sababu hatupo katika bajeti ya serikali, hivyo huwezi kusimamia mambo ya msingi wakati wewe ni ombaomba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles