31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

BROOKLYN: Shule huru isiyo na mtaala wala mtihani

wakicheza* Wanafunzi hujiongoza wenyewe kwa kila kitu

POPOTE pale katika maisha ya mwanadamu kuna sheria na miongozo inayosaidia kufanya mambo yaende kwa taratibu zinazokubalika.

Sheria au kanuni popote uendapo utazikuta zimewekwa kuanzia juu kabisa ngazi ya kimataifa hadi kikanda, kitaifa hadi katika familia.

Katika ngazi hizo pia kuna kampuni, mashirika, taasisi zikiwamo za elimu hadi vikundi rasmi na visivyo rasmi vikiwa na sheria na miongozo yake.

Yote hayo ni kuhakikisha kila kitu kinaenda vyema na kuadhibu wale wanaokiuka taratibu hizo ili wasirudie kuvuruga mwenendo unaokusudiwa.

Kwa sababu hiyo, shuleni ni miongoni mwa maeneo ambayo yana sheria na taratibi zikiwamo zile kali ili taasisi husika ya elimu ifikie malengo ya kitaaluma iliyojiwekea ikiwamo katika suala zima la nidhamu ya mwanafunzi.

Wakati hali halisi ikiwa hivyo, katika shule hii makusudio ya safu yetu hii; Shule Huru ya Brooklyn, hali ni tofauti.

Kama ambavyo jina lake linavyojieleza, katika shule hii wanafunzi wako huru mno kufanya chochote kile wanachojisikia au kitaka.

Ni wanafunzi, ndio wanaohusika kutengeneza sheria wao wenyewe kwa namna wanavyoona inafaa badala ya wao kuzikuta shuleni wanapojiunga.

Kwa manano mengine ni shule ya demokrasia huru, ambayo iko huko Fort Greene, Brooklyn, ikiwa imeanzishwa mwaka 2004.

Shule imegawanyika katika vitengo viwili, ambavyo ni kama darasa la awali na la juu.

Kitengo cha kwanza ni kwa ajili ya wanafunzi wenye umri wa miaka kati ya minne na 11.

Kingine ni cha wanafunzi wenye umri wa miaka 11 na 18.

Katika shule hii hakuna mtaala na iwapo wanafunzi hawajisikii kuja shule, ni ruksa kubaki nyumbani.

Naam, wanafunzi hufanya lolote wapendalo, lolote wanalotaka.

Baadhi huamua kusoma wenyewe, au kucheza katika viwanja vya shule, au kuishia kutanga tanga tu bila malengo yoyote na hata kujitupa kitandani kulala.

Kama hiyo haitoshi, katika shule hii hakuna mitihani, wala kazi za nyumbani ama alama za ufaulu.

Iwapo wanafunzi wanataka kuamua kitu fulani, huitisha kikao na wanafunzi au na walimu.

Madarasa pia huendeshwa na wanafunzi wenyewe, ambapo walimu hubakia kama wasimamizi tu.

Pamoja na yote hayo ya kushangaza, shule hii imeelezwa kufanikiwa katika malengo yake, ijapokuwa imekosolewa mno kwa kukosa mtaala.

Ilianzishwa kwa kutumia falsafa ya uhuru ya miaka ya 1960/70 ya vuguvugu huru za shule. Farsafa hiyo huhimiza uhuru wa kujiongoza na kujifunza mwenyewe pamoja na kulinda uhuru wa harakati za mtoto katika makuzi yake bila kuingiliwa.

Shule hii ilikuwa ya kwanza huru jijini New York tangu mwaka 1975. Ilianza katika jengo la kukodisha la kanisa la Methodist la Park Slope, lakini ikahamia Fort Greene.

Wanafunzi huhudhuria katika madarasa ya ubunifu na katika uongozi wa shule, ambao hufanywa katika mkutano wa lazima wa kila wiki wa kidemokrasia.

Mada kuhusu mikutano huhusisha kuanzia wasiwasi wa kukithiri kwa nidhamu mbovu hadi matumizi ya kompyuta.

Mwenyekiti wa mkutano huchaguliwa mwanzoni mwa mkutano huku mtu yeyote anayetaka kujadili suala linalohusu shule, huwa na uwezo wa kuitisha mkutano.

Walimu na wanafunzi wana kura sawa mikutanoni. Shule hujiendesha kwa kutegemea ada za shule, ruzuku na misaada ya wafadhili.

Mwaka 2012, mwandishi wa Gazeti la The Huffington Post, Lucas Kavner aliita shule hii kuwa bila ubishi ndiyo kituo chenye maarifa makali na makini zaidi ya kujifunzia.

“Tunajaribu kukuza watoto wakue  wenyewe. Hicho ndicho wanachotaka kukileta duniani kuishi wakiwa na mafanikio na maisha ya furaha, anasema Alan Berger, mwasisi na mkuu wa shule hiyo.

Berger awali alikuwa mwalimu wa shule ya kawaida, kabla ya kujiondoa kuanzisha shule hii baada ya kusoma kitabu cha farsafa uhuru wa kujiamulia mambo bila kuingiliwa.

Madarasa ya shule yanahusisha pamoja na farsafa katika semina, kuonja jibini, kujadili vitabu, biashara, unajimu, saikolojia, upigaji picha mnato na video na kadhalika.

Baadhi ya madarasa yanafundishwa na watu wanaojitolea.

Kuna kanuni ndogo ambayo huwataka wanafunzi kuhudhuria saa 5.5 kwa siku.

Berger anasema shule hiyo hutoa elimu bora inayoendana na zama hizi za intaneti ikienda na wakati na mabadiliko ya kiuchumi.

Kufikia mwaka 2015, shule hii ilikuwa na wanafunzi 80 na 24 walishahitimu.

Nusu ya wanafunzi hao ni Wamarekani weusi na wale wenye asili ya Amerika ya Kusini.

Katika shule hii wanafunzi wapya huingizwa kwa njia ya wingi wa kura unaopigwa na kamati inayohusisha walimu, wazazi na wanafunzi.

Kamati kwanza huangalia kama wazazi wa waombaji wanaunga mkono watoto wao kujiunga na shule iwapo kweli shule ni muafaka kwa mahitaji ya mwanafunzi husika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,586FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles