Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MITANDAO ya kijamii ni mojawapo ya mawasiliano ambayo yamekuwa yakitumika kuwasaidia watu kujua habari mbalimbali.
Mitandao hiyo imekuwa ikiwasaidia watu kupata taarifa za jambo fulani kwa wakati tofauti na miaka ya nyuma.
Pia inawasaidia watu kurahisisha kufanya biashara za papo kwa papo, kuwasaidia wanafunzi kutafuta taarifa zinazowasaidia kusoma kwa bidii.
Hata hivyo baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mitandao hiyo vibaya kwa kuweka taarifa chafu na wakati mwingine kutoleana maneno ya kashfa na kusababisha uvunjifu wa amani.
Hivi karibuni katika mahafali ya tisa ya kidato cha nne kaika Shule ya Sekondari Victory iliyopo Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Mkurugenzi Msaidizi masuala ya elimu mtambuka kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Venance Manori, aliwasihi wahitimu na wanafunzi kuwa makini hasa katika mitandao ya kijamii kwani imekuwa tishio na chanzo cha kuharibu malengo hasa kwa vijana.
Anasema kuwapo kwa mitandao ya kijamii ni mojawapo ya utandawazi ambao utawasaidia watu kupata habari kwa wakati.
Anasema kuna baadhi ya watu wamekuwa si wazuri katika matumizi ya mitandao hiyo na kusababisha kundi kubwa la vijana kupotea kimaadili.
“Mitandao ya kijamii itumike kusaidia wananchi kupata taarifa kutoka pande mbalimbali za nchi na dunia na si kuitumika katika mambo yasiofaa,”anasema Manori.
Manori anasema kuwa ni wajibu wa kila mwanafunzi kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii ili asije akaharibikiwa kimaisha.
Kuhusu masomo ya sayansi, anasema nchi inakabiliwa na uhaba wa wataalamu wa sayansi, hivyo akazishauri shule zingine kuiga mfano wa shule hiyo ili wapatikane wataalamu wengi wa sayansi.
Anampongeza mmiliki wa shule hiyo, DK. Thadei Mutembei, kwa kutambua mchango wa walimu na wanafunzi na kuamua kutoa motisha kila mwaka.
Mkuu wa shule hiyo, Emmanuel Thompson, anasema wamekuwa wakiwahamasisha wanafunzi kwa kuwatia moyo, wapende masomo ya sayansi na kuacha dhana potofu kuwa masomo hayo ni magumu.
Anasema wamejenga maabara za kisasa za masomo ya baiolojia, kemia na fizikia zenye vifaa vya kutosha ikiwamo pia maabara ya kompyuta.
Anasema kuanzia mwaka 2013 hadi 2015, wanafunzi wote waliosajiliwa kufanya mitihani ya kidato cha pili walifaulu kwa kupata asilimia 100 ambapo wote waliingia kidato cha tatu.
Kwa upande wa kidato cha nne anasema wanafunzi wote walifanya vizuri na kuingia kidato cha tano.
Akizungumzia motisha anasema walimu wanapelekwa nchini Dubai kwa ajili ya ziara za masomo, kupatiwa fedha tasilmu na kupatiwa usafiri.
“Mmiliki wa shule amekuwa na moyo wa kizalendo katika kuwekeza katika elimu ambayo ndio msingi wa maendeleo katika jamii,” anasema.
Kwa upande wa wazazi anasema kwa mzazi mwenye mtoto zaidi ya mmoja hupata punguzo la ada kwa asilimia 50, wanafunzi wanapatiwa vifaa vya shule pamoja na kupunguziwa ada.
Pia anasema shule yao imeweka mkakati wa kuwatambua na kuwasaidia kwa ukaribu zaidi wanafunzi wenye uwezo wa chini.
Anaongeza kuwa kutoa mazoezi ya kutosha kwa wanafunzi na kufanya marudio na kuhakikisha walimu wanakuwepo ili kuwahudumia watoto hao.
Anasema wanafunzi zaidi ya 200 wanatarajia kufanya mitihani mwishoni mwa mwaka huu.
Mwalimu huyo amewataka wahitimu hao wanapotoka shule na kurudi nyumbani kuyaendeleza yale waliyofundishwa na wasijiingize katika makundi yasiyofaa.