23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wenzi mbilikimo wa Uingereza waliozaa ‘mbilikimo maradufu’

mbilikimo

SI mbilikimo pekee nchini Uingereza bali wenzi, ambao wamezaa mtoto pekee mwenye ‘umbilikimo maradufu’ nchini humo, na ambao hivi karibuni walifunga ndoa ya kukata na shoka mbele ya ndugu na marafiki wa karibu 50.

Ni Laura Whitfield, mwenye urefu wa futi nne na inchi mbili na mumewe Nathan Phillips mwenye urefu wa futi tatu na inchi 11, wakiwa wamechumbiana kabla ya kuzaliwa mtoto wao Nathan Junior.

Nathan Junior alizaliwa na aina mbili tofauti za umbilikimo, ‘anachondaplasia’ kama ya mama yake na pseudochondaplasia kama ya baba yake.

Kutokana na hali hiyo, madaktari walimtabiria kutoishi kwa walau saa chache baada ya kuzaliwa.

Lakini wahenga walisema; ‘Mungu si Athumani,’ kwani dogo Nathan kwa sasa ana umri wa miaka miwili na nusu na alikuwa mshika pete wa ndoa ya wazazi wake hao.

Laura (26) na Nathan (37), kutoka Sunderland, walikutana wakati wakicheza shoo ijulikanayo Snow White walifunga ndoa kanisani na kisha kufuatia hafla ya kuwapongeza katika Hoteli ya South Causey, Kaunti ya Durham.

Bibi harusi Laura alimfuata mwanae kuelekea kanisani akiwa amevalia gauni lenye thamani ya pauni 800 sawa na Sh milioni 2.4, ambalo liliburuza na kumfuatia kwa nyuma wakati akiingia mbele ya kanisa – ambako Nathan alikuwa akisubiri akiwa amevalia suti yake.

Laura ambaye kitaaluma ni mburudishaji anasema: “Tulikutana wakati tukifanya shoo mwaka 2012.

“Ilikuwa ni shoo za Snow White na Seven Dwarfs, yeye alikuwa akicheza kama mdoli Grumpy nami kama Soppy.”

“Ilifurahisha kwa sababu ulikuwa mwanzo mzuri wa maisha yetu pamoja – sasa tumeoana na ndoa yetu ilikuwa mwujiza wa aina yake.

“Hakika tulisubiri kwa muda mrefu muda ufike tuoane. Tulitoa nafasi kwanza kwa dogo Nathan aweze kuwa na umri wa kutosha kubeba pete zetu, lakini mwishowe mkebe wa pete ulikuwa mzito mno kwake.

“Aliamua kwamba hataki kuubeba tena na aliutupa pembeni.

“Kilikuwa kitu cha kuchekesha na kufurahisha na maalumu kwetu kuwa naye pale alichotaka yeye ni kucheza cheza tu na jukwaa.”

Akizungumzia namna walivyochumbiana, Laura ambaye ameonekana katika filamu kama vile Harry Potter, alisema: “Nilijua kuwa Nathan alikuwa akitarajia kunichumbia – alithubutu kwenda kwa baba yangu kuomba ruhusa.”

“Niliingiwa na wasiwasi sana na sikuweza kujizuia kucheka, lakini pia ukweli ni kwamba kunichumbia ndicho nilichotaka na binafsi nilimchekea usoni– sikupenda kuipoteza fursa hiyo.

Ilikuwa mwezi mmoja tu baada ya kuchumbiwa, msanii huyo aligundua kwamba yu mjamzito – kitu kilichowaweka katika wakati mgumu wapenzi hao

Laura alisema: “Kwanza nilishauriwa nifikirie kuitoa mimba baada ya madaktari kugundua uwapo wa matatizo machache ya kitabibu kuhusiana na mimba yangu. Hata hivyo, nilidhamiria kuona mwisho wa jambo hili, yaani nini kitamtokea Nathan maana sote tulitokea kumpenda baada ya kupewa picha ya jinsi alivyo tumboni.

“Na wakati alipozaliwa kwa sababu madaktari hawakudhani kuwa angeweza kuishi kwa saa chache kwa sababu ya ufupi wake maradufu, lakini alikuwa mpiganaji mdogo na hadi sasa anaendelea vyema.

“Madaktari baadaye walisema kwamba ijapokuwa dogo Nathan ana matatizo ya jini kulinganisha na watoto wengine, hakuna sababu ya kumfanya akose maisha kama watoto wengine wa umri wake.

“Ni sawa na mimi mwenyewe na Nathan mkubwa – nilikumbana kila aina ya dhihaka na kejeli kwa sababu tu ya hali yangu ya ufupi, lakini haikuchukua muda nilitambua kuwa ni mimi ninayetakiwa kupambana changamoto hizi na na kweli watu waliacha kunisumbua.

“Najua watu wana shaka nasi kwa sababu tu wafupi, lakini sisi ni sawa na wao, tofauti ni kimo chetu tu,” anasema na kuongeza:

“Ndoa ilikuwa jukwaa kubwa la kumuonesha kila mtu namna tulivyo na hali yetu ya kujiamini wenyewe. Hakika ilikuwa siku nzuri kabisa katika maisha yetu.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles