30.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Muhongo aitwisha mzigo Bodi ya Tanesco

Pg 3 jan.19Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amezindua rasmi Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuipa vipaumbele vitano vya utekelezaji wa majukumu yake.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Dar es Salaam jana, ilisema uzinduzi wa bodi hiyo ulifanyika makao makuu ya Wizara ya Nishati na Madini na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wizara hiyo.
Alisema bodi hiyo ina jukumu kubwa la kuliongoza shirika hilo kwa ufanisi na kuhakikisha linajitegemea ili kupunguza utegemezi wa fedha kutoka serikalini.
“Kwa kipindi kirefu, Serikali imekuwa inatoa fedha nyingi kuisaidia Tanesco kutekeleza miradi katika maeneo ya uzalishaji,usafirishaji na usambazaji wa umeme,bodi ionyeshe jinsi mtakavyolibadilisha shirika hili ili hii misaada kutoka serikalini ipungue na ifike mahala lijitegemee,” alisema Profesa Muhongo.
Kuhusu madeni ambayo Tanesco inadai kutoka kwa taasisi za umma, binafsi na watu binafsi, Waziri Muhongo aliiagiza bodi hiyo kulisimamia suala hilo na kuja na mkakati utakaoliwezesha shirika kukusanya madeni hayo, kwani lengo la serikali ni kuona shirika hilo linakusanya madeni kutoka kwa wadeni wake wakubwa na wadogo ili liweze kulipa madeni linalodaiwa na wadau wake.
Suala la wananchi kufungiwa umeme ndani ya siku 30 mara wanapopeleka maombi Tanesco, lilionekana kumkera Profesa Muhongo na kuiagiza bodi hiyo kulishughulikia ili siku hizo zipungue.
“Bodi simamieni maombi ya kufungiwa umeme ambayo sasa yanaelezwa kushughulikiwa ndani ya siku 30, hii lazima ibadilike, Watanzania lazima wapewe umeme ndani ya wiki moja, zaidi ya hapo haikubaliki.
“EWURA waelezwe kuhusu suala hili ili kuona namna ya kupunguza hizi siku sababu wao wanahusika katika suala la upangaji wa siku husika,” alisema Profesa Muhongo.
Aliiagiza bodi hiyo, kuhakikisha shirika hilo linashirikiana na sekta binafsi katika miradi yake ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme ili kufanikisha lengo la Serikali la kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
Alisema kulingana na sera zilizopo, uendelezaji wa sekta ya umeme unahitaji ushirikishwaji wa sekta binafsi kwa kuwa uwekezaji unahitaji kiasi kikubwa cha fedha za kigeni.
Alisema Tanesco inapaswa kuonesha nia thabiti ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kukamilisha majadiliano na wawekezaji na waendelezaji wa miradi bila kuwakatisha tamaa.
Naye Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dk. Mighanda Manyahi alisema majukumu waliyokabidhiwa ya kuisimamia Tanesco ni makubwa, lakini kwa kutumia taaluma zao watahakikisha wanayatimiza.
Wajumbe wa bodi hiyo, ni Kissa Vivian Kilindu, Mhandisi Juma Mkobya, Dk. Haji H. Semboja, Shaaban Kayungilo, Dk. Mutesigwa Maingu, Mhandisi Boniface Muhegi, Felix Kibodya na Dk. Nyamajeje Weggoro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles