25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto aibua utata wa Sh bilioni 821 bomba la gesi

zittoNa Fredy Azzah, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, ameibuka tena na utata wa Sh bilioni 821 ambazo Serikali ya Tanzania imelieleza Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kwamba imezitumia katika mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Mradi huo unaogharimu dola za Marekani bilioni 1.55, kati yake asilimia 95 ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya China na asilimia 5 ni fedha zitakazotolewa na Serikali ya Tanzania.
Zitto ameibuka na utata huo zikiwa zimepita siku chache tangu alipoonyesha wasiwasi juu ya matumizi makubwa ya fedha kwenye mradi huo mwanzoni mwa mwezi huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Zitto alisema ripoti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), iliyowasilishwa kwa kamati yake Novemba 3, mwaka jana, inaonyesha kuwa fedha ambazo Tanzania ilikuwa imetoa ni dola za Marekani 31.3.
“Fedha ambazo Serikali imeahidi kutoa ni dola za Marekani 61.4, ambazo tayari ilishatoa ni 31.3, lakini barua ya Tanzania (Letter of Intent) kwenda IMF, inasema Serikali kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni mwaka 2014, ilitumia dola za Marekani milioni 464 (Sh bilioni 821), huu ni utata, inabidi tupate majibu.
“Hata kwa hizi fedha za kutoka Exim Bank ya China ni mkopo ambao unatakiwa ulipwe kati ya 2020 hadi 2040, sasa inakuwaje tena Serikali inaonekana imezitumia fedha hizo kabla hata ya muda wa kulipa mkopo haujafika?” alihoji Zitto.
Akifafanua kuhusu barua hiyo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Beno Ndulu, alisema mradi huo unagharimu dola za Marekani bilioni 1.25 ambazo asilimia 95 ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya China.
Alisema dola za Marekani milioni 464 ambazo zimeelezwa kwenye barua hiyo ya IMF ni sehemu ya mkopo huo wa Benki ya Exim.
“Ile dola milioni 464 ni disbursement (malipo) ya Exim ya China, mkopo wote ni dola za Marekani bilioni 1.25, kuna namna tatu ya kuripoti madeni, namna ya kwanza, mwaka ule tulivyokubaliana inakuwa ni commitment, kwamba mkopo ni dola bilioni 1.25, wale wakasema fedha ni hizo na zitatumika kulipa ujenzi wa bomba, lakini hawatoi cash, wanalipa makandarasi, wanalipa shughuli za ujenzi.
“Sasa disbursement ya ule mkopo inafanyika kadiri utekelezaji unavyokwenda, kwa hiyo ile dola milioni 464 maana yake ni kiasi kilichotolewa mwaka huo wa fedha 2013/14 kwa makandarasi katika shughuli ya kujenga huo mradi, siyo kwamba fedha inatolewa inakuja hapa sisi ndiyo tuwalipe makandarasi, inatolewa moja kwa moja kulingana na kazi iliyofanyika, benki hiyo inatoa hiyo fedha kwa niaba yetu.
“Kwa kuwa ule mradi hautekelezeki kwa mwaka mmoja tu, ni wa karibu miaka miwili, kadiri wanavyotekeleza ndivyo wanavyolipwa, kwa mikopo mingine wewe unapewa hela kisha unawalipa makandarasi, lakini hii wanalipa wenyewe, wanalipa kwa niaba yako, hii itaenda hadi fedha hiyo yote ya mkopo iishe,” alisema Profesa Ndulu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, msimamizi wa mradi huo kutoka TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba, alisema hadi sasa Serikali ya Tanzania imeshalipa asilimia tano ya fedha hizo ambazo ilipaswa kuzitoa.
Mhandisi Musomba alisema sehemu ya fedha hizo ni dola za Marekani milioni 31.3 zilizotumika kununua mashine (compressor) inayotumika Songosongo.
Alisema fedha nyingine ni zaidi ya Sh bilioni 20 zilizotumika kwa kufidia watu waliopisha mradi huo na vitu vingine.
“Kwa sasa hivi hapa sina takwimu zozote, lakini ninachoweza kukwambia ni kwamba ukijumlisha mambo yote, hiyo asilimia tano ya Serikali ni kama dola za Marekani 94, na zote zilishatoka,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles