26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Tunavyoweza kujenga urafiki imara na watu – 2

friends

Na CHRISTIAN BWAYA,

WIKI iliyopita tuliona marafiki wa karibu walivyokuwa hitaji muhimu katika maisha yetu. Tuliwagawanya marafiki katika makundi mawili; marafiki tegemezi, wanaotuhitaji, na marafiki wainuaji, wale tunaowahitaji. Kadhalika, tuliona kuwa urafiki wa karibu unazaliwa kwa hatua za makusudi zinazochukuliwa kama vile kuaminika na kujitahidi kuwasilikiliza wengine. Katika makala haya tunatazama nguzo nyingine muhimu za kuanzisha urafiki.

Kuvumilia mapungufu ya wengine

Kama tunataka kujenga urafiki wa karibu na watu, kwa kweli, tunalazimika kuyakubali mapungufu ya wengine kwa upendo. Haiwezekani, mara zote, watu wakawa kwa namna ile tunayotaka wawe. Tunatofautiana kimtazamo, kiimani na kiuelewa hivyo ni makosa kujaribu kulazimisha mitazamo yetu, imani zetu na hata uelewa wetu uwe wa watu wote.

Kwa kawaida binadamu hatupendi watu wanaojiona wako sahihi muda wote ambao hujikuta wakiwa na tabia ya kukosoa na kuona upungufu wa wengine. Tunapokuwa na tabia ya kuwaponda watu kila mara tunajipunguzia alama za kuaminika.

Yapo mazingira ambayo tofauti za kimisimamo na watu hazikwepeki. Mathalani, kuna masuala kama imani za kidini na itikadi za kisiasa. Kila mtu anayo haki ya kuwa na misimamo yake. Hata hivyo, tofauti kubwa wakati mwingine zinaweza kuathiri urafiki kwa sababu kuna hulka ya watu kuvutiwa na wale wanaofanana nao.

Lakini pamoja na kulazimika kutofautiana na wengine, bado tunaweza kabisa kufanya hivyo kwa upendo bila kuwafanya wengine wajisikie kudharauliwa. Kwa hiyo, kukosoa wengine kupita kiasi, kudhihaki na kukejeli wale tunaotofautiana nao ni tabia zinazoweza kuzorotesha urafiki.

Kushiriki furaha, huzuni zao

Tunahitaji kufurahi wenzetu wa karibu wanapokuwa na furaha. Hilo linawezekana kama tunaweza kuhesabu mafanikio ya rafiki zetu kama mafanikio yetu badala ya wivu na husuda pale tunapohisi kuzidiwa.

Upo ukweli kwamba kadri tunavyofurahia mafanikio ya wengine, ndivyo furaha inavyoturudia mara dufu. Lakini pia, watu wana kawaida ya kufurahi pale wanapoona tunafurahia mafanikio yao kwa dhati pasipo unafiki. Kwa hiyo tukitaka kuwa na marafiki wa karibu, tunalazimika kuwa na tabia ya kufurahia mafanikio ya wengine.

Kadhalika, zipo nyakati ngumu katika maisha. Kuna matukio mazito hutokea yanayotufanya tuwahitaji wengine kutusaidia kubeba mizigo yetu. Mfano, kufiwa na watu wa karibu, kupoteza kazi na changamoto nyingine za kijamii.

Katika nyakati hizi, tunahitaji kuwa tayari kubeba mizigo ya wenzetu na kuifanya kama yetu. Waswahili walishasema mapema, akufaae wakati wa shida, ndiye rafiki wa kweli. Kuhesabu matatizo ya wengine kama matatizo yetu wenyewe, ni sehemu ya kujitambua na husaidia kujenga kuaminika kirafiki.

Urafiki ni kujitambua

Jitihada za kujenga urafiki wa karibu na watu zina gharama kubwa kama tulivyoona. Jitihada hizi zinadai muda wa kutosha kupatikana, kujenga kuaminika sambamba na ukomavu wa kuvumilia wengine. Lakini faida zinazoambatana na urafiki wa karibu kiasi hicho zinaweza kabisa kuhalalisha gharama hizo za lazima. Wanasema, hakuna kizuri kisicho na gharama.

Tunaweza kutoa visingizio vingi leo kuonesha kwanini haiwezekani kufanya jitihada hizi, lakini ukweli unabaki pale pale kuwa maisha hayawezi kukamilika bila urafiki wa karibu na watu fulani fulani. Uwezo na jitihada za kujenga urafiki wa karibu na watu ni sehemu ya maisha ya kujitambua kwa mwanadamu.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Anapatikana kwa [email protected] na 0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles