29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Sarah Macarthur-King: Viongozi wanawake waepuke kutoa uamuzi wawapo katika hedhi

Mwanamke akiwa kwenye hedhi huwa na hasira zisizo za kawaida.
Mwanamke akiwa kwenye hedhi huwa na hasira zisizo za kawaida.

NA JOSEPH HIZA,

MTAALAMU wa masuala ya uongozi amesababisha utata baada ya kuandika makala akidai wanawake hawapaswi kutoa maamuzi mazito wawapo katika siku zao.

Mtaalamu huyo wa utendaji, Sarah Macarthur-King mwenye makazi yake mjini Canberra, Australia anaendesha kampuni ya mafunzo na ushauri wa uongozi na utendaji ya Invictus Coaching Solutions.

Aliandika katika la jarida la wanawake la HerCanberra kuhusu namna wanawake wanavyoweza kukabiliana na shinikizo zinazotokana na kuwa katika siku zao (PMT) wakati wakiwa katika nyadhifa za kiuongozi.

“Uwapo katika kipindi hicho, usifanye maamuzi yoyote makubwa,” Macarthur-King aliandika.

“Iwapo ni uamuzi nyeti, kusubiri kwa wiki moja si mbaya. Na iwapo unadhani kuna umuhimu wa kutoa uamuzi mara moja, hakikisha una mtu unayemwamini kupitia wazo lako kama lina maana au asaidie kutoa.”

Makala hiyo iitwayo ‘PMT: Namna ya kuziongoza hisia zako katika uongozi’, ilisababisha kelele katika mitandao ya jamii kwa mujibu ya mwandishi huyo.

Alisema mrejesho alioupata ulihusisha maneno makali mno kiasi kwamba andiko lake liliondolewa kutoka mtandao wa Facebook.

Lakini Macarthur-King alitetea makala hiyo akisema anasimamia katika kile alichoandika.

“Makala hiyo imetokana na uzoefu wangu mwenyewe na pamoja na kuwasaidia wateja wangu kwa masuala kama hayo,” alisisitiza.

“Kuna aina ya tabia niliyoanza kuiona kwangu mwenyewe na nilifikiria nini ninaweza kufanya kukabiliana nayo?’

Alilinganisha ushauri wake kwa wanawake kutofanya maamuzi nyeti wakati wakiwa katika siku zao kama mtu anayekabiliwa na matatizo fulani ya kiafya.

‘Ni kwa kiwango kile kile wakati mtu anapopatwa na kiwango cha chini cha sukari katika damu.

“Iwapo wanaamua huku tumbo likiwa tupu na huku wakiwa na kiwango kidogo cha sukari kwenye damu, hawatarajii kutoa uamuzi sahihi,” Macarther-King alieleza.

Mtaalamu huyo wa uongozi wa Canberra, anasema pengine kushambuliwa kwa makala yake kumetokana na walioisoma kutoielewa vyema maudhui yake.

“Sisemi wanawake ni wendawazimu au hawana hekima na eti hawawezi kufanya uamuzi. La hasha!

“Ni aina ya uamuzi nyeti nilikuwa nikizungumzia kuhusu kutoenda na kufanya uamuzi wa kununua nyumba iwapo hauko sawa kisaikolojia.”

“Ni suala linalowakabili wanawake na mimi mwenyewe ni mwanamke nimeliona kwangu binafsi na kwa wateja wangu walionijia kwa ushauri na hivyo sioni kwanini nisiwe mkweli,” alisema.

Hata hivyo, watu wengi walikosoa makala yake kutokana na mtazamo hasi, ambao tayari umejijenga kwa miaka mingi dhidi ya wanawake walio katika nafasi za uongozi pamoja na lugha iliyotumika katika makala hiyo.

Wakosoaji wanasema inazihalalisha imani potofu zilizopo katika jamii nyingi duniani kuhusu uwezo wa wanawake.

Makala ya Macarthur-King imekuja huku kukiibuka simulizi za wanaume kutumia programu za kompyuta kubaini mzunguko wa mwezi wa siku za wafanyakazi wenzao wa kike ili wakae mbali na ‘matatizo na kuepukana na hali zisizo na lazima.’

Lakini mtaalamu huyo anasema wanaume wanaochunguza siku za wafanyakazi wenzao wa kike wamepotoka na anaamini kuwa PMT ni suala la kawaida ambalo viongozi wa kike wanapaswa kulikubali.

Macarthur-King pia alikataa ukosoaji dhidi yake kwamba anakandamiza wanawake viongozi kupitia uandishi wake.

“Ni upuuzi kabisa, wanawake wana kila nafasi kubwa ya kuwa viongozi wazuri, lakini bado pia sisi tuna changamoto tofauti na wanaume na hili nililogusia na kukosolewa ni moja ya changamoto hizo,” anasema.

Makala hiyo pia ilipendekeza kwamba wanawake wanapaswa kuwa wazingativu, kutumia muda zaidi katika kazi zao na kuwa wepesi kukiri iwapo wanajikuta hawako sawa pindi wanapokuwa katika hedhi.

Katika makala hiyo, pamoja na mambo mengine mtaalamu anachangia uzoefu aliopitia kuhusu PMT kiasi cha kutoa ushauri huo.

Anasema; “Katika kipindi cha miezi sita niliyopita nimeshuhudia mwenendo kama wa wazimu ulionipata nikiwa katika biashara zangu.

Mwenendo huu huondoa ule wa wiki tatu za utaalamu, ubunifu, ujuzi, furaha, umakini na kufuatiwa na wiki ya kukata tamaa, shaka na uchovu, msito sito na udhaifu wa kiuchambuzi.

Wakati wa kipindi hiki kifupi, kila kitu kilionekana kwenda mrama, ubongo wangu haukuonekana kuwa na uwezo wa kutatua matatzo kwa ufanisi na nilihisi shinikizo likitaka kunipasukia.

Nilichambua nini kinanifanya kuwa katika hali hiyo na makosa ninayofanya. Nilihisi shaka, wasiwasi na kuchelewa chelewa kimaamuzi na mume wangu alinitazama kwa jicho la udadisi tayari kutoa msaada kwa tatizo lisilojulikana wakati nilipoanza kuongea bila mpangilio.

Nilifuatilia nyendo hizi kwa miezi michache ambapo ubunifu na umahiri wangu ulipoenda likizo. Nilijaribu na kupambana nao nikidhani kuna kitu hakiko sawa na kudhani kwamba uchukuaji hatua ni ufumbuzi haswa.

Lakini wakati kila kipindi hiki kifupi kibaya kilipoisha nilijihisi vyema na kila kitu kilienda sawa.

Wakati nilipohisi ilitokana na kufanya kazi sana niliamua kufanya uchunguzi na kubaini tatizo linahusiana na homoni zangu na si ubongo na hutokea tu wakati niwapo katika siku zangu.

Ni kwa sababu hiyo iliyonifanya nichangie na wenzangu na kutoa ushauri wa nini cha kufanya kwa wanawake hasa walio katika nafasi za uongozi.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles