KATIBU Mkuu wa zamani wa CCM, Yusuph Makamba amedaiwa ndiye aliyeasisi rushwa ndani ya chama hicho.
Hayo yalielezwa na mwanachama wa Chadema, Hamisi Mgeja, ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga.
Mgeja alikuwa akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana.
Alisema Makamba aliupotosha umma alipokuwa katika Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika Dodoma wiki chache zilizopita aliposema kuwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alimuacha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika kinyang’anyiro cha urais kwa sababu ya ufisadi.
“Napinga, hiyo si sababu ya kweli. Makamba alipokuwa KatibuMkuu hakuna kikao hata kimoja kilichowahi kusema Lowassa ni fisadi. Hata alipotaka kugombea urais kupitia Chadema hakukuwa na pingamizi juu yake.
“Nyota ya Lowassa iliyong’aa ndiyo iliyomgharimu… Makamba hawezi kusimama kuwasema wengine.
“Yeye ndiye mwasisi wa rushwa ndani ya CCM. Alikuwa akiita (akiikaribisha) rushwa baada ya kupokea kijiti kutoka kwa Philip Mangula,”alisema.
Alidai Makamba aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibondo anajua alifukuzwa kwa sababu zipi.
“Naomba Watanzania wampuuze. Makamba ni kama nyoka asiye na sumu, anazeeka vibaya. Alipokuwa Katibu Mkuu CCM alikuwa jipu lililoshindwa kupasuka mpaka alipostaafu.
“Alipokuwa mtendaji mkuu ndani ya CCM rushwa iliota mizizi… hana usafi wa kuwasema wengine ni vema akajitathimini ikiwezekana akaye kimya kulinda heshima yake,”alisema Mgeja.
Makamba alipotafutwa na Mtanzania kuzungumzia tuhuma zilizoelekezwa kwake, alisema hana muda wa kubishana.
“Sina muda wa kubishana na wajinga, wapumbavu… ukibishana na mpumbavu nawe utaonekana mpumbavu, watu hawataona tofauti.
“Narudia tena mama, sina muda wa kubishana na wapumbavu, ukibishana, nawe utaonekana mpumbavu, tofauti haitaonekana,”alisisitiza.
Akizungumzia kauli ya Rais John Magufuli alipokuwa Dodoma kwamba angekuwa Rais Kikwete wote waliomshangilia Lowassa ukumbini angewapoteza, Mgeja alisema uwezo huo hana.
Alisema inawekana hata Rais Kikwete alikasirika zaidi yake lakini hakuwa na uwezo wa kufanya lolote.
Alimshauri asome Ibara ya 107 ya Katiba ya CCM imwongoze mipaka yake.
“Lugha aliyotumia ilikuwa ya kujenga hofu, hao ambao angewamaliza asilimia 85 wamo ndani ya CCM na ndiyo atakaofanya nao kazi kwa sababu miongoni mwa waliomtaja Lowassa wako mawaziri wake,”alisema.
Alisema hakuna mwenye uwezo wa kumjaribu Rais bali wanapopashana habari za siasa anatakiwa kuwa mvumilivu.
“Anasema vyama vimechoka, hakuna chama kilichochoka…kama mwanasiasa mwenzetu anatakiwa kutumia lugha ya ustaarabu.
“Iliyopita mwaka 2015 ilikuwa mvua ya rasharasha, masika yanakuja mwaka 2020. Asivibeze vyama vya siasa, aviheshimu, sote tuna haki,”alisema.
Mgeja alisema wanaohama Chadema kurudi CCM wanahama kwa matakwa yao.
Alisema yeye na wenzake wanapata ushirikiano mzuri huko waliko.