Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BENKI ya Biashara ya Akiba (ACB) imeahidi kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wanamichezo wa Mtandao wa Wasanii Tanzania (Shiwata) waliojenga nyumba katika kijiji chao cha Mwanzega, kilichopo Mkuranga mkoani Pwani.
Akizungumza kwenye mkutano wa wanachama wa Shiwata wanaomiliki nyumba 185 zilizojengwa katika kijiji hicho, Meneja wa Benki ya ACB tawi la Ilala, Mary Haule, aliwahakikishia kuwapatia mikopo ya ujenzi na ufugaji kwa muda mfupi.
Alisema mikopo hiyo itawawezesha wanachama hao kujenga mabwawa ya kufuga samaki, kufuga kuku na kuboresha nyumba zao kuwa za kisasa zaidi.
Mwenyekiti wa Shiwata, Cassim Taalib, akimtambulisha Meneja Masoko wa Kampuni ya kuuza vifaa vya umeme wa jua, kutoka Kampuni ya Steps, Maulid Said, wanachama hao walihakikishiwa kuingiza umeme wa jua kwa gharama ya Sh 250,000 kila nyumba.
Msanii Faridu Taratibu, aliwaambia wenzake kuwa safari ya kuhamia kijijini alikuwa ameianzisha na sasa anahamia baada ya huduma zote za awali za jamii kama umeme zitafikishwa kijijini.
Shiwata katika mkutano huo ilitoa nafasi nyingine kwa wawekezaji kujenga shule, zahanati na maduka mbalimbali ya vifaa vya ujenzi na vyakula.
Mtandao huo unaomiliki eneo la ekari 300 za makazi na ekari 500 za kilimo imepata baraka za Serikali ya Wilaya ya Mkuranga katika jitihada za kuwakomboa wasanii wake.
Mwenyekiti Taalib alisema Shiwata, imeweka mikakati kwa wanachama wake watakaohamia kijijini kupewa ekari moja bure ya kulima mazao yatakayowawezesha kupata mboga mboga na mazao ya muda mfupi.